Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Mheshimiwa Waziri utakumbuka miaka ya nyuma kidogo nilikuwa nikichangia hapa ninakuwa mkali sana, na wewe unajua sababu ya ukali wangu wakati huo, lakini leo nachangia hapa nikiwa na furaha kwamba mambo mengi ambayo nilikuwa nikiyasema umeyawezesha. Nakushukuru sana.
Mheshimiwa Waziri, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kukupatia jukumu hili na kwa miradi mingi aliyotuletea katika Wilaya yetu ya Hai. Mheshimiwa Bashe, nakupongeza sana kwa ujenzi wa Soko la Mula. Pale Mula najua tayari mkandarasi ameshapatikana na wako kwenye hatua za kuanza ujenzi. Kwa hiyo, niwaambie wananchi wanaotumia Soko la Mula, kuweni wapole Mheshimiwa Rais ameshatupatia fedha, Soko la Mula linaenda kujengwa soko la kisasa kabisa, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde. Kule Hai wanamwita Mzee wa Makeresho. Namshukuru sana Mzazi kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha Wilaya ya Hai inapata miradi mikubwa. Leo ninavyozungumza tuna mradi wa shilingi bilioni 19 kwenye Skimu ya Mtambo; tayari Bwawa la Bolutu, Makeresho, Metromu vinafanyiwa feasibility study; Kiladedea A tayari wanafanya feasibility study ili waweze kujenga. Nawashukuru sana kwa kazi hii kubwa mliyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, sasa haya ninayokwambia ni machache sana, nami najua watu wa Nzega wanakupenda sana. Kwa hiyo, nina hakika Bunge lijalo uko hapa nami watu wa Hai wameshaniambia mimi hapa narudi, na Mungu ameshanipa kibali. Kwa hiyo, mimi na wewe Bunge linalokuja tutakutana hapa. Sasa haya yafuatayo naomba uyaweke vizuri ili tuelewane, urafiki huu tuliouanza Bunge hili la mwishoni mwishoni, hilo Bunge linalokuja tuanze vizuri tusianze vibaya kama tulivyoanza Bunge lililopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Bwawa la Mto Mbuguni pale, nilikwambia linatoa maji kuja kuhudumia Kawaya, Longoi, na Mkalama. Haya maji yakipatikana, Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye hotuba yako umeeleza kuna changamoto. Hizi changamoto zilizopo pale, hii inaenda kutibu. Wewe unajua watu wa Hai huwa tunafanya kilimo cha biashara, nasi ndio walimu wazuri. Kwa hiyo, tupate haya maji pamoja na maji ya pale kwenye Bwawa la Kibashukeni iliyoko kwenye eneo la Lyamungo, Kilanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata Bwawa la Kwa Tito, hili ni Bwawa muhimu sana. Tukilipata litatusaidia. Urara pale kuna bwawa la muda mrefu, limeharibika, limetelekezwa. Hili Bwawa la Urara na lenyewe litatusaidia, lakini najua Mheshimiwa Waziri wewe mtu bingwa mmeshanunua magari. Nakuomba haya magari yako hebu yaanzie Mkoa wa Kilimanjaro na yaweke kambi pale Hai yapige kazi pale kama miezi miwili halafu ndiyo yaende.
Mheshimiwa Waziri, kule Kiyeri niliongea na wewe ukaniambia nenda kwa watu wa Kiyeri kawaahidi kwamba utawachimbia visima vya umwagiliaji. Nakuomba, magari haya yazinduliwe pale, nami ninakuandalia sherehe na ndafu nzuri, magari yaende yakazinduliwe pale Hai, baadaye ndiyo yaelekee kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine hili, Mheshimiwa Waziri unisikilize kwa utulivu kabisa. Tuna mashamba ya Ushirika, haya mashamba yapo 17. Umenisaidia, tumepunguza changamoto japo hazijaisha, lakini naomba nikushauri. Kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuna shida gani kama tukiamua sehemu ya ardhi kwenye mashamba yale mazuri, kwa mfano, lile Shamba la Kikafu Mrososangu pale anapokaa James kwenye makazi yake, tukachukua pale ekari mbili tu tukajenga hoteli za kitalii?
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani ekari mbili hizi hazina madhara yoyote. Tutaendelea kulima kahawa, tutaendelea kufanya shughuli nyingine ili angalau kuwe na package kidogo ya kuongeza fedha. Mheshimiwa Waziri sisi kule kwetu ardhi imekwisha. Tukipata fedha inayotokana na uwekezaji kwenye hoteli za kitalii zitatusaidia kwenda kule Nzega kununua maeneo angalau na sisi tuanze kusogea huko taratibu kwa sababu, ardhi yetu imekwisha. Nakuomba sana, hili Mheshimiwa Waziri linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimezungumza na Kamishna wa PPP, inawezekana. Tunafanya valuation ya zile ekari mbili tu au hata ekari moja bila kuathiri shughuli zozote za kilimo. Mheshimiwa Waziri, nikuhakikishie, kama ukinipatia wataalamu wako nikakaa nao, nimeshazungumza na Katibu wa Maliasili amekubali jambo hili. Wilaya ya Hai ardhi imekwisha, kwa hiyo, lazima tutafute alternative ya kuweza kuhakikisha Wilaya yetu inapata uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri alituahidi hapa Barabara ya Kwasadala kwenda Longoi kupitia mpango ule wa kilimo kwenda kwenye Soko la Kwasadala. Kumbuka Mheshimiwa Rais ameshatutengea shilingi bilioni 11.6; kwa utaratibu wako tumeongea asubuhi, naomba sana, endelea kuliweka kwenye kumbukumbu zako.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, leo sitaki kugongewa kengele. TARI wapeni fedha ya kutosha. Imewekwa kwenye bajeti, ndiyo, lakini hampeleki hizi fedha. Naomba TARI wapewe fedha ya kutosha ili wafanye kazi yake. 
Mheshimiwa Naibu Spika, naounga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)