Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye hoja ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa nchi yetu. Mimi nitakuwa na section mbili. Kwanza, tunaishukuru Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia vitu vifuatavyo; kutoa pembejeo za mikorosho bure kwa wakulima wetu; pili, kutoa ruzuku kwenye mbolea; na tatu, kusimamia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani vizuri, pamoja na TMX, ambao unawafanya wakulima waneemeke kwa kupata fedha nyingi na bei nzuri kutokana na mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashauri kwenye mambo yafuatayo: Ushauri wangu wa kwanza, naomba Mheshimiwa Bashe anisikilize kwa makini sana kwa sababu, mimi ni mkulima ambaye natoka kijijini. Mfumo wa ugawaji pembejeo una kasoro kidogo, ni kwamba, hakuna uwazi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, wamefanya vizuri, wameandikisha wakulima, kila mmoja anajua analima kiasi gani? Ila wakati wa kugawa, mkulima anaenda pale ghalani, hajui anapata kiasi gani? Hili linasababisha wakati mwingine malalamiko kuwa mengi kwamba, wamepunjwa. Kwa hiyo, naomba sana, kwa sababu, tayari tumeshawaandikisha hawa wakulima, basi ni vizuri tukabandike yale yaliyotoka kwenye research yetu, ili kila mmoja ajue anapata mifuko mingapi na kwa wakati gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kugawa huku, kuna kalenda ya uzalishaji wa korosho, namna ya kuhudumia. Tufuate kalenda jinsi inavyotaka, ili hizi dawa zinapokwenda zikahudumie mazao yetu vizuri. Tofauti na hivyo, unapeleka Sulphur wakati inahitajika dawa ya maji, kwa kweli, tunayumbisha uzalishaji wa zao la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye hili la ugawaji wa pembejeo, ni suala la kuangalia ratio. Sasa hivi jinsi wanavyogawa inaonekana kwamba, mfuko mmoja unahudumia mikorosho 100, kitu ambacho siyo jambo la kawaida. Kwa hiyo, naomba wakati wanagawa ile Sulphur, watuoneshe mgao wa kwanza utapata mifuko kadhaa na mgao wa pili utapata mifuko kadhaa, ili mkulima naye aweze kufanya adjustment ya namna ya kupulizia shamba lake, na kama kuna haja ya kuongeza mifuko mingine, basi aongeze ili aweze kuhudumia mashamba yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye ugawaji ni suala la kuangalia wakati na muda maalum wa kugawa. Mara nyingi umbali kutoka kwenye ghala unasababisha wengine wakose hizo pembejeo. Basi tujiahidi maghala yaliyo mazuri ya vyama vya msingi na vijiji yatumike yote ili mkulima asiende mwendo mrefu kufuata hizi pembejeo, jambo ambalo linamkatisha tamaa wakati mwingine kufuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, lingine ambalo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hii ni mara ya pili naliongea, kuna kero kubwa sana ya wakulima kuhusu akaunti zao kwenye benki zetu za biashara. Niliomba mwaka 2024 kwamba, Wizara ya Kilimo ikae na Wizara ya Fedha warekebishe Sheria ya Fedha inayohusiana na akaunti za wakulima kuwa dormant ndani ya miezi sita. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo linasumbua sana wakulima, kila mwaka wanakuwa kama wanaenda kufungua akaunti mpya. Mkulima ameuza korosho zake, hana habari, hapati message, anakaa mnada wa kwanza, wa pili, wa tatu, kumbe hela imeshaenda benki, imegonga ukuta kwa sababu akaunti yake imekuwa dormant. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, hebu wasaidieni hawa wakulima waondokane na hii kero kwa sababu, ipo ndani ya Sheria ya Fedha. Basi mjitahidi BoT warekebishe kuhakikisha kwamba akaunti za wakulima zisiwe na muda maalum wa kuzifunga kabla hawajaanza kufanya operesheni. Hili jambo litatusaidia sana kupunguza kero. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la maghala. Naomba kila siku, ubora wa korosho unatokana na ubora wa maghala. Stakabadhi Ghalani pamoja na TMX, kama hakuna ubora wa zao, kwa kweli inakuwa ni shida. Tunaomba sana tutengeneze programu maalum ya kujenga maghala kwenye vijiji vyetu, ili vyama vya msingi vitumie maghala maalum, badala ya nyumba za watu ambazo hazina ubora ule unaotakiwa kwa ajili ya kutunza mazao yetu. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mpakate, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)