Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia mjadala wa hii Bajeti ya Kilimo. Mimi ni Mbunge ambaye natoka Jimbo la Ludewa ambalo wakulima ni wengi sana. 
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini sekta ya kilimo. Napongeza pia Kiti chako na Bunge lote kwa kuidhinisha bajeti kubwa kwa miaka zaidi ya mitatu mfululizo kwenye Wizara ya Kilimo. Hali kadhalika, nampongeza sana Mheshimiwa Hussein Bashe kwa uthubutu, vilevile kufanya maamuzi mengi kwa kutumia takwimu na kuzingatia teknolojia kwenye kilimo. Hii kwa kweli, inatuvutia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nashukuru sana kwa ruzuku ya mbolea. Kwa kweli, wananchi wa Ludewa, hasa wakulima, wameweza kuongeza mavuno. Tangu muanze kutoa hii ruzuku mavuno yameongezeka na wakulima wamepata fedha nyingi, wamelipa ada za watoto na kujenga nyumba za kisasa. 
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu 2025 Ludewa tuna mahindi mengi sana. Kwa hiyo, wanaiomba Serikali, kupitia NFRA, iweze kujipanga. NFRA, kupitia Mkurugenzi Komba, mwaka 2024 walifanya kazi nzuri; walinunua mahindi kwenye vituo vingi Ludewa, wananchi walifurahi sana na mwaka huu pia, wanaomba ajipange. Namshukuru pia, ameweza kumlipa Mkurugenzi, zile SES zimeweza kusaidia sana kukwamua miradi ya wananchi ambayo ilikuwa imekwama. Kwa hayo, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lile ombi letu wananchi wa Ludewa kuweza kuwa na godown kwa ajili ya kuhifadhi, hasa mahindi, tuweze kufikiriwa na Serikali. Pale Ludewa Kijijini kulikuwa na godown, sasa limechakaa, lilikuwa linahudumia wakulima kutoka Kimelembe, Ibumi, Kata ya Ludewa na lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani nyingi sana. Kwa hiyo, mwaka 2024 walishindwa kununua zaidi, kwa ajili hiyo. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mlangali kuna godown ambalo linahitaji tu ukarabati wa ile sehemu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kupitia SCR, Watu wa NFRA waweze kwenda kukarabati hilo eneo kupunguza tope na vumbi, ili mazao yale yanunuliwe katika mazingira ya usafi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna Kituo kingine kile cha Amani, wale wanachoomba tu ni ule mradi ambao mlikuwa mnashirikiana na watu wa TAMISEMI, ninadhani ni RISE, ambao ulikuwa unaboresha barabara za vijijini kwenda kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa. Ludewa, ule mradi bado tunauhitaji kwa sababu tuna uzalishaji mkubwa sana. Unavyozungumzia Kata ya Ibumi, mkulima mmoja anapata magunia 8,000 ya mahindi. Kwa hiyo, kule ukisema lori la tani 10 liende ni kuwapa hasara wakulima, kuwaingizia gharama na kuwakimbizia masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba ule mradi ambao ulikuwa unashirikiana na watu wa TARURA kuboresha barabara za vijijini. Kule tuna uhitaji wa barabara inayoanzia pale Madope kwenda Madilu – Ilininda mpaka Kata ya Mundindi. Ile barabara ina uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo. 
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba pia, kule kuna wakulima wa viazi, kuna zao wanalima ule msimu wa umwagiliaji, wanaita kipalila. Wale wananchi wanahangaika wenyewe kwa teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, Mheshimiwa Waziri, atume wataalam kutoka umwagiliaji waweze kwenda kujifunza, kile kilimo kinaitwa kipalila, kwenye Kata ya Madilu, Milo, Lupanga na Mlangali, ili waweze kuwasaidia kuboresha ile teknolojia ya umwagiliaji kwa sababu, vile viazi vinawawezesha sana kiuchumi. Naomba sana watu wa umwagiliaji waweze kuwatembelea kuboresha kile kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, barabara nyingine ambayo ni ya ukanda wa uzalishaji mkubwa inaanzia Kigasi, inakwenda Milo – Ludende mpaka Kata ya Mundindi, kupitia Amani. Kwa hiyo, ule mradi wa RISE utusaidie, hata kama hawataweka lami, waweze kuweka changarawe ambayo malori mpaka ya tani 30 yatapita msimu wote na ile barabara inayoanzia Ludewa kwenda Ibumi kuja kuunganisha Mundindi. Huu ni ukanda wa uzalishaji mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba ule mradi ufuatiliwe uweze kutusaidia kwenye barabara za ukanda wa uzalishaji. Kama mkulima analima mazao, anashindwa kuyafikisha kwenye masoko kwenda kwa walaji, sekta ya kilimo tutachelewa kuweza kupunguza umaskini kwa sababu, hadi sasa sekta ya kilimo imechangia 26% ya pato la Taifa na kuajiri zaidi ya 65% ya Watanzania. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kile kitendo cha Waziri wa Kilimo kugawa minazi bure, ule ni uwezeshaji mkubwa sana wa kiuchumi kwa wananchi unaofanywa. Wale wakulima wakianza kuvuna zile nazi watapata mapato mengi sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Kamonga.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru kwa Miradi ya Umwagiliaji Lihuu na Ivumi. Naunga mkono hoja. (Makofi)