Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie hii Wizara ya Kilimo. Nianze kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta suluhu ya changamoto kubwa iliyokuwa inawakumba wakulima; changamoto ya pembejeo pamoja na viuatilifu. Kwa nini nasema ameleta suluhu ya changamoto hiyo ya pembejeo? (Makofi) 
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa sababu katika jimbo langu kwa miaka mitatu mfululizo, 2022/2023, zao la korosho tulipata tani 15 peke yake. Mwaka 2024/2025 tumevuna takribani tani 31 na zaidi. Hii yote imeletwa na wakulima wale kupewa pembejeo, kwanza kwa wakati; na pili, bure kabisa. Kwa hiyo, utagundua mwanzoni tulikuwa tunapata uzalishaji mdogo kwa sababu ya kukosa Sulphur na viuatilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili. Naomba nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Bashe, yeye na Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia jambo langu la pili Wilaya ya Tunduru, sisi uchumi wetu unachagizwa na kilimo. Kama unachagizwa na kilimo, mazao yale ili tuweze kupata tija ni lazima yaongezewe thamani. Tunayaongezaje thamani? Maana yake ni korosho zile zinazovunwa zinapaswa kubanguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduru tuna Kiwanda cha Ubanguaji Korosho. Kiwanda kile kilikuwa kinafanya kazi vizuri sana kwa ufanisi mkubwa. Pia, kilikuwa kinatoa ajira kwa akina mama zaidi ya 600 na vijana zaidi ya 200, ambapo walikuwa wanafanya kazi ya vibarua pale, wanapokea posho ama mishahara yao kwa kila mwezi. Sasa ninavyosema hivi sasa, kiwanda kile kimesimama kwa muda mrefu sana, hakifanyi kazi. Maana yake ni nini? 
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba ajira zile za akina mama na vijana zimekwenda kuyeyuka, na kwa bahati mbaya sana wakati kiwanda kile kinasimama, kilisimama na madeni ya wale vibarua. Wale wamama na vijana wanadai fedha nyingi, wamejaribu kufuatilia na mpaka hivi sasa hawajalipwa fedha zao. Kwa hiyo, Serikali ilikuwa ina nia njema sana ya kujaribu kutafuta wawekezaji ambao watawekeza viwanda vile ili waweze kuviendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi, mwekezaji wa kiwanda kile pale Tunduru tunaona kabisa ameshindwa kukiendeleza, kwa lugha nyepesi, hana uwezo wa kukiendeleza kiwanda kile. Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali ione namna ya kuweza kukirejesha Serikalini na hatimaye apewe mwekezaji mwingine mwenye uwezo, ili sasa kiweze kufanya kazi, wakulima na wananchi wa Tunduru wanufaike; akina mama zaidi ya 600 pamoja na vijana wale waendelee kupata ajira ya muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwenye Jimbo langu tulipata Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ambao una thamani ya shilingi bilioni 6.4, lakini yule mkandarasi wa skimu ile mpaka sasa tunavyozungumza, ilipaswa awe ametekeleza mradi ule kwa zaidi ya 50%, lakini ametekeleza kwa 18%. Kwa hiyo, tunaona speed yake ni ndogo. Tunaomba speed iongezeke na kama kuna tatizo lolote, basi Wizara ikae chini ione namna ya kuweza kutatua mradi ule uweze kuendelea kwa sababu, Tunduru tunategemea sana Kilimo cha Mpunga na kilimo kile kinalimwa msimu hadi msimu. Mradi ule wa skimu ya umwagiliaji ukikamilika tunakwenda kulima bila kutegemea msimu na hatimaye tutaendelea kulisha mchele Lindi, Ruangwa, Nachingwea na Mtwara pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la tatu ni ukomo wa uongozi wa Bodi za Vyama Vikuu. Mheshimiwa Waziri viongozi wale wa vyama vikuu, muda wao wa uongozi ni miaka mitatu. Kama ni miaka mitatu, tafsiri yake ni nini? 
Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni kwamba, baada ya mwaka mmoja atafanya kazi, lakini mwaka wa pili ataanza maandalizi tena, kwa maana hiyo atakosa ufanisi. Kama alikuwa ni kiongozi bora, kiongozi mzuri, ataishia njiani kwa maana muda mwingi anakwenda kuandaa uchaguzi na hatimaye anashindwa kuboresha kazi yake. Kwa hiyo, nashauri muda huu uweze kuongezwa, badala ya miaka mitatu, iwe mitano. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiri kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Hassan, muda wako tayari umeisha.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)