Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, ambaye kwa kweli, amekuwa na maono makubwa na msikivu. Tulimshauri kwa muda mrefu kwamba, aongeze uwekezaji kwenye sekta za uzalishaji, na kwa kweli, amedhihirisha kwa namna alivyowekeza na ambavyo bajeti imeongezeka. Hongera sana. Pia nampongeza, kwa kutoa usafiri kwa Maafisa Ugani na zaidi ya hapo kwa kutenga fedha, kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa na kuongeza sekta ya umwagiliaji. Ametenga fedha nyingi, ambayo kwa kweli, haijawahi kutokea, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naipongeza sana Wizara. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Watendaji wote walioko katika Wizara yake. Kwa kweli, sisi tumedhihirisha leo kwamba, wanasema mzigo mzito mpatie Mnyamwezi, na kweli, haya yamejidhihirisha kwa namna ambavyo mmesimamia vizuri sana Wizara ya Kilimo. Tunaona jinsi ambavyo mnachacharika na tunaamini, hata wananchi wale, wapigakura wenu kwa kweli, watawarudisha katika nafasi zenu ili muweze kuendelea kuongoza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nawapongeza sana kwa kuanzisha Benki ya Ushirika. Benki muhimu sana ambayo tunaamini itatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu nampongeza, kwanza kupitia Bodi ya Kahawa kwa kutuchimbia visima kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba ya kahawa. Kwa kweli tunakupongeza sana, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo wameifanya, lipo jambo ambalo tunalo kama ombi. Tunajua wamefanya mengi na wanaendelea kuyafanya, lakini pale Mbozi tulikuwa na yale maghala ambayo yalianza kujengwa tangu mwaka 2017. Yale maghala ambayo tunaita vihenge, vilikuwa ni vihenge vizuri sana, na mpaka sasa hivi, tangu viliposimama mpaka leo wananchi wanasubiria vile vihenge vikamilike ili viweze kutoa mchango mkubwa katika kutunza mazao yetu ya nafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vihenge tunaomba vipewe uzito. Tunaelewa kwamba zilikuwa ni fedha za mkopo kutoka huko nchi ya Poland, sasa tumeanza kulipa mkopo, lakini bado yale maghala hayajakamilika. Ni vizuri wakiyasimamia, yakiweza kukamilika itakuwa vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tunawapongeza kwa bei nzuri ya upande wa kahawa na namna ambavyo wamefanya. Kwa kweli kahawa sasa hivi bei mwaka huu imekuwa ni nzuri sana. Sasa tunaomba BBT ambayo wanayo, ambayo inakwenda kwenye halmashauri, wale vijana na watu wengine wahamasishwe kwenda kuwekeza kwenye zao la kahawa ambalo ni muhimu sana katika maendeleo ya wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, tumepata changamoto sana mwaka huu kuhusu soko la mazao ya parachichi. Parachichi tumepata changamoto kubwa sana. Tulihamasisha wananchi wakalima parachichi kwa wingi, wakazalisha kwa wingi, lakini soko mwaka huu baada ya kuyumba kwa kweli wamekosa mahali pa kwenda kuuza. Tunaombeni msaada tusaidiwe ili kutafuta masoko zaidi tuweze kulima zaidi tuweze kuongeza kwenye maembe na maeneo mengine. Hii tunaamini kwamba itatoa mchango mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne, soko la nje kuhusu mahindi na mazao mengine, tunaomba, tunajua sasa hivi kuna changamoto ya mahusiano ya Zambia, Malawi, na maeneo mengine; tunaomba yaimarike ili masoko yale yafunguliwe na wananchi wa maeneo yale waweze kuuza. Tuuze kama ni mahindi tuweze kuuza kule, kama ni kuuza mbegu tuweze kuuza, kama tunapata mbegu kutoka kwao, basi ziweze kutusaidia; na hii itatusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo nilitaka kulisemea ni kuhusu kiwanda cha kuongeza thamani. Tunacho kiwanda cha kahawa pale Mlowo. Tungeomba kile kiwanda sasa kipige hatua zaidi kianze kutengeneza kahawa mpaka hatua ya mwisho badala ya kuongeza tu thamani ile. Sasa tutengeneze kahawa ambayo inatengenezwa instant coffee kutoka kule Mbozi. Hiyo itakuwa kwa kweli ni msaada mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri ameifanya katika Wizara, tunaamini sisi; na bado naendelea kuimba na wao nimesikia kwamba wanaimba wimbo huo, kwamba kilimo ni chakula, ni viwanda, ajira, uchumi, na fedha. Hili sisi tutaendelea kulisimamia, tutaendelea kuhamasisha kuungana na juhudi za Wizara ili mambo yaendelee kwenda mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni kuhusu lile bwawa la pale Msia. Bwawa lile tulitengewa fedha mwaka juzi, lakini hazikuweza kwenda. Naliomba lile bwawa basi mwaka huu fedha zingeenda pale ili bwawa lile liweze kukamilishwa, na ili wananchi wa Wilaya ya Mbozi na wa eneo la Msia waweze kumwagilia. Hii itatusaidia sana katika kuweza kuchangia uchumi mkubwa wa eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, nawapongeza timu nzima, wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)