Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi nami kuwa mtu wa mwisho kuchangia.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa anza mchango wako, acha kushukuru. (Kicheko)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuna mambo mengi sana yanaendelea ndani ya Afrika Mashariki na Tanzania kwa ujumla, hasa katika masuala ya biashara ya kilimo. Biashara za mazao ya kilimo kumekuwa kuna matatizo katika mipaka yetu ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo limetokea, tumeona mfano bidhaa zetu zimezuiwa kuingia South Africa, zimezuiwa kuingia Malawi; lakini imekuwa ni kampeni kubwa sana, na kampeni hizi zinaendeshwa na wanaharakati ili kuhakikisha kwamba Tanzania hatuwezi kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanaharakati hawa wamekuwa sasa wanataka kuingilia hata msimamo na masuala yetu ya siasa za ndani ya Tanzania. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kuwa-lock hawa watu ambao walikuwa wanataka kuingia kupitia Uwanja wetu wa Ndege wa Dar es Salaam, na wakarudishwa kwao. Tunatakiwa Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono jitihada za Mheshimiwa Rais kulinda nchi na mipaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo limeongelewa mpaka na Wabunge wenzetu wa Kenya, kwamba kuna watu wanaofanya chokochoko za kwenda katika nchi nyingine. Kwa hiyo, maamuzi yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais yanatakiwa kuungwa mkono kwa nguvu kubwa sana na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala mengi ambayo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu, ni kwamba masuala yoyote yatakayokuwa Mahakamani, sisi hatutakiwi kuyajadili hapa. Sasa kumekuwa kuna watu ambao kwa kupitia baadhi ya NGO, wanataka kutumika vibaya kuja kuharibu usalama wa nchi yetu na usalama wa biashara zetu za kilimo na mazao haya tunayoyalima hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo ambalo ni baya zaidi ni kwamba, sasa wanaanza kutumika hawa watu katika masuala mengi sana ya kuhusiana na mazao yetu ya kilimo pamoja na mifugo. Sisi Tanzania kama nchi, maamuzi anayoyachukua Mheshimiwa Rais, kwa ajili ya nchi yetu, tunatakiwa tuwe imara na Bunge lako pia limuunge mkono kwa maamuzi ya kuilinda nchi. Siyo lazima tuilinde nchi kijeshi, tunaweza tukailinda katika mipaka yetu, kuzuia watu wanaokuja kuharibu taswira na amani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaanza kuchangia. Tuna mazao yetu ya kilimo, hasa zao la pamba katika Mkoa wa Mwanza, Simiyu, Geita, Tabora, Katavi, Singida, na Kagera kidogo na sasa hivi Kigoma, zao la pamba linalimwa kwa kiwango cha juu sana. Zao hili la pamba limekuwa likipata bei za mkanganyiko mpaka kiasi ambacho pamoja na Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, imesema zao la pamba ifikapo 2025 tuwe tuna uwezo wa kuzalisha tani milioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo halitawezekana kama zao la pamba na lenyewe halitachukuliwa kwa uzito mkubwa kama ilivyochukuliwa korosho. Unajua kabisa wakati Mheshimiwa Bashe, amekaa katika kiti hiki ambacho mimi nipo hapa sasa hivi, nilikuwa namwangalia sana wakati huo mimi sijawa Mbunge, anazungumzia pamba. Pamba imekuwaje? Amesahau haya maneno ya pamba, au mkishaingia ndani ya game mnasahau haya mambo? Naye bahati nzuri ni mtoto wa Wasukuma anatokea Nzega, anajua kabisa mambo ya pamba yalivyo. Pamba inavyokuwa na shida. Ulimaji wa pamba una shida kwa kiwango cha juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ifikie mahali ambako tunashukuru, pamoja na kuweka kwamba Igunga peke yake iwe ndiyo pilot ya kulima kwa ajili kupata mbegu za pamba, lakini pamoja na Igunga kuwa ndiyo inayotakiwa kuzalisha mbegu za pamba, zisambazwe zifike kwa wakulima. Sisi ruzuku bado haijatufikia na tunachotaka, uundwe mfuko wa pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aje awaeleze Watanzania wanaolima pamba zaidi ya mikoa 17, awaambie kwamba, “pamba sasa itapata ruzuku, limeni pamba tufikishe tani milioni moja, tuinue uchumi wa nchi yetu.” Leo tunakuwa tunavaa mashati, ukilivaa tu unapigwa shoti. Unavaa shati unapigwa shoti! Sijui haya mashati ni ya nailoni, wakati sisi tuna pamba hapa. Kwa nini tuvae nguo za namna hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nguo zote yaani unapigwa shoti. Yaani kama vile umepigwa shoti ya umeme, kumbe unavaa shati. Sasa haya mashati haya na sisi tunalima pamba, hebu tulilinde hili zao la pamba lisije likapotea katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninavuka Daraja la Magufuli sasa ninaingia jimboni Sengerema; ninamshukuru Mwenyezi Mungu daraja limekwisha, sasa sijui Mheshimiwa Bashe ana kizuizi gani cha kuja Sengerema? Kwa sababu alikuwa anaogopa ferry, sasa je, atakuja Sengerema kuona tuna Kiwanda chetu cha Buyagu, tuna ginnery ipo Buchosa kule kwa mdogo wangu Mheshimiwa Eric Shigongo, na yenyewe kule ilikuwa inazalisha mafuta, lakini tuna viwanda vipo Nyambiti kule vyote vinakufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tuna kiwanda kipo Manawa kule Misungwi, tuna kiwanda kipo Ukerewe, na viwanda vingine vipo Magu. Naomba Mheshimiwa Waziri aje aangalie namna ya kufufua hivi viwanda. Nyanza ina zaidi ya shilingi bilioni mbili, sasa hivi bilioni mbili na nusu. Kama kuna bilioni mbili na nusu, waruhusiwe hizi pesa wakanunue ginnery mpya kule India au hata wakanunue used ambazo zina hali nzuri kwa sasa hivi, ili tufufue zao la pamba, tuanze kulima pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Nyanza inaanzishwa Mheshimiwa Bashe, mwaka 1972 wananchi wa Mkoa wa Mwanza walikuwa 840,000 leo wananchi wa Mkoa wa Mwanza wapo zaidi ya shilingi milioni 2.7. Sasa kwa hali hiyo, sasa hivi Mheshimiwa Bashe anatakiwa amwambie huyu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika aje naye kule, tupige mkutano awasikilize Wanamwanza wanataka nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Wilaya ya Mwanza ambayo ilikuwa Wilaya ya Mwanza ina Ilemela na Nyamagana, hawana hata sehemu plot ya kuchimba choo. Hawa bado wanahitaji, wao ni wakulima wa pamba, hawa wanahitaji sasa hivi kufuga samaki, wanahitaji kufuga kuku, kufuga ng’ombe na huu ushirika ulianzishwa kwa ajili ya kulima pamba, lakini pamoja na hali hiyo, Geita tayari imeshakatwa, wameanzisha mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna wilaya nyingine na yenyewe tena tumewaazima watu wa Simiyu Busega, tukawapa kule, kwa hiyo yaani Nyanza inaendelea kukatwa katwa tu hivyo hivyo. Sasa kwa hali hiyo ukubwa wa Nyanza sasa hivi na ma-godown yaliyopo na viwanda vyetu, vyote sasa hivi wameanza kuweka stoo, wanaweka mbolea, wanaweka cement, wanakodisha wanaweka magodoro...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Tabasam, mchango wako ni mzuri sana, ahsante.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Bashe, akija hapa atuambie, sasa huu Ushirika wa Nyanza, je, bado utaendelea kuwa ushirika wa pamba?

NAIBU SPIKA: Haya, mengine utamfuata baadaye utamwambia. Mheshimiwa Tabasam, utamfuata kwenye meza utamwambia.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)