Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi, na ninamtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Waziri wa Kilimo kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (National competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Katika kipindi chake akiwa Waziri wa Kilimo, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na taarifa ya Wizara ya Kilimo, Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha mazao, kwa wastani hekta milioni 10.8 tu sawa na 24% ndizo zinazolimwa kila mwaka. Sekta hii kwa mwaka 2024/2025 imeendelea kuchangia takribani 26.1% kwenye pato la Taifa, imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa 65% na imechangia 65% ya upatikanaji wa malighafi za viwanda. 
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya kilimo ni mhimili wa uchumi wa nchi na inachangia pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla. Sekta ya kilimo na hususan sekta ndogo ya mazao imechangia 15.4% katika pato la Taifa na zaidi ya 100% ya upatikanaji wa chakula kinachozalishwa nchini na kupelekea utulivu wa mfumuko wa bei kwa takribani 59%.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kujitosheleza kwa chakula na kuchangia katika uchumi wa Taifa, takribani mazao yote yanazalishwa kwa tija ndogo katika eneo husika. Uzalishaji wa mahindi wa chini ya tani mbili kwa hekta moja ni 29% tu ya uzalishaji unaotegemewa wa tani sita kwa hekta moja. Uzalishaji huu wa chini kwa mazao yote kwa kiasi kikubwa unatokana na ukosefu wa ushauri wa watalaamu wa kilimo ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine. 
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii, kilimo hakijamsaidia mkulima, kwa kiasi kikubwa tunajinasua kwenye umaskini na kimeendelea kutoa mchango mdogo kwenye pato la Taifa. 
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii ya takribani 65% ya Watanzania kuchangia 26% tu ya pato la Taifa, inahitaji kuweka mikakati ya kimageuzi ili sekta ya kilimo ichangie zaidi ya mara mbili ya sasa. Pia, kuwepo na mkakati wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na wakati huo huo kupunguza asilimia ya wananchi wanaotegemea kilimo kwenda kwenye sekta nyingine za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa mbolea nchini hadi Februari, 2023 ulikuwa tani 748,890 ambayo ilikuwa juu ya mahitaji ya tani 667,730. Pamoja na bei za mbolea kwenye Soko la Dunia kuwa juu, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa ruzuku ya karibu 50% na kupelekea tani 300,179 kununuliwa kwa bei ya ruzuku. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hii muhimu ni mafanikio makubwa katika safari ya kuleta tija kwenye kilimo nchini na napendekeza kuendelea na ruzuku ya pembejeo pamoja na kuanzisha Price Stabilization Fund kwa pembejeo hasa mbolea ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo.
 
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iendelee kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kununua na kuhifadhi nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Kutokana na vita inayoendelea ya Urusi na Ukraine kunaashiria kuendelea kuwa na upungufu mkubwa wa nafaka na kwa kuzingatia gharama kubwa za uzalishaji wa karibu 100%.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali ichukue hatua za makusudi kusaidia wakulima wapate bei nzuri ya NFRA badala ya kuuza kwa walanguzi na kutorosha chakula nje ya nchi. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, kufikia mwaka 2030, biashara ya mazao ya chakula inakadiriwa kufikia Dola za Kimarekani trilioni moja. Serikali ichukue hatua za makusudi kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula kutosheleza soko la ndani na nje. Uzalishaji wenye tija kwenye kilimo utaongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kupunguza pengo la urari wa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie fursa za Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kuanza uzalishaji wa viuatilifu inayotokana na pareto ambayo inazalishwa hapa nchini na imekuwa inauzwa nchi za nje kama semi-finished product kwa bei ndogo ya kutupa. Viuatilifu kutokana na pareto ni suluhisho la soko la pareto na pia suluhisho kwa upotevu wa mazao kushambuliwa na wadudu (post-harvest losses).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ianze mchakato wa kuanzishwa viwanda vya mbolea kwa kutumia madini (calcium carbonate, agricultural lime, phosphates, natural gas etc.) yanayopatikana kwa wingi hapa Tanzania, kuanza uzalishaji wa mbolea hapa nchini. Kutokana na athari za vita ya Urusi na Ukraine zinazoendelea, iwe fursa kwetu kwa kuanza kutumia rasilimali zinazopatikani nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi 834,382,834,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo sehemu kubwa ilielekezwa kwenye miundombinu ya umwagiliaji. Utekelezaji wa miradi hadi kufikia Februari, 2023 hasa utekelezaji kwa fedha za nje uko chini sana. Sehemu kubwa ya miradi inategemea kuchukua miezi 24 na kuna matumaini ya utekelezaji kwenda kama ulivyotarajiwa. Matumaini pekee ni hatua zilizooneshwa kwenye bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali iweke mikakati madhubuti kuhakikisha ufanisi wa utekelezaji wa bajeti hii ya umwagiliaji. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali iangalie utelezaji wa miradi ya mabwawa kuunganisha uratibu kwa mahitaji ya jumla kama vile mahitaji ya Wizara ya Mifugo na hata Wizara ya Maji, kunaweza kuwa na tija kuwa na chombo kimoja chenye nguvu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hii pia iweke nyongeza za ujenzi wa mabwawa hasa maeneo yenye mafuriko makubwa ikiwa ni pamoja na kuzuia mafuriko. Pia, napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyomo kwenye Mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. 
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi, ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine, yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ichukue hatua za haraka kuleta Bungeni mapendekezo ya Sheria ya Kilimo ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kutokana na changamoto za tabianchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji mkaa na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji. 
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo kwa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchanga na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.