Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge; Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ernest Silinde, Mbunge; Katibu Mkuu wa Wizara hii Ndugu Mweri, Naibu Katibu Mkuu; Wakurugenzi; na watumishi mbalimbali waliopo chini ya Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wamekuwa wasikivu na wenye kutekeleza. Pale wanapokuwa wanapelekewa hoja wanakuwa ni watu wa kufanya maamuzi kwa wakati na kutoa majibu yanayoleta tija; na amekuwa akifanya kazi kwa weledi na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wanampenda na wanasema kuwa Wizara yake wameiweka kiganjani. Hii yote ni kwa sababu ya usikivu wake na utii kwa Waheshimiwa Wabunge pale wanapompatia hoja zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nitumie fursa hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta hii ya kilimo. Tumeona kwa miaka mitatu mfululizo bajeti ya Wizara ya Kilimo inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka hadi kufikia shilingi trilioni 1.2. Hii inaashiria maono makubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais juu ya sekta hii na tija yake imeshaanza kuonekana katika ukuaji wa sekta ya kilimo, mchango mkubwa katika pato la Taifa na ongezeko la uzalishaji kwa mazao mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wakulima wa korosho tunamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais jinsi alivyotoa kipaumbele kwenye tasnia ya korosho; kwanza kwa kutoa Export Levy ambayo Wizara na Bodi ya Korosho (CBT) imesaidia kupatikana kwa pembejeo za kilimo kwa wakulima wa zao. Pia kutuwezesha kupata kongani ya viwanda pale Maranje ili kuongeza thamani ya zao la korosho. Wanamtwara wameahidi kumpatia kura za kutosha ifikapo Oktoba, 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuishauri Serikali mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza ni kuhusu suala la kuweka utaratibu maalumu kwa wenye viwanda vya ndani kupata malighafi ya kutosheleza kwa mwaka mzima; na pili kupewa motisha mbalimbali kama vile motisha ya kikodi ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi na kuwapatia mikopo yenye riba nafuu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali ifanye hivyo kwa sababu watu hawa wanatoa ajira kwa akina mama na vijana. Nchi kadhaa wametengeneza utaratibu huu, mfano Benin, Msumbiji, Burkina Faso na Ivory Coast, wamefanya hivyo na wamefanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali itoe fedha Za Export Levy kwa Wizara ya Kilimo kwa wakati ili zitumiwe kama zilivyopangwa. Fedha za Export Levy za msimu uliopita hadi leo hazijatolewa, hivyo kuleta malalamiko kwa wazabuni ambao wamesambaza pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naiomba Serikali itoe fedha hizo kwa wakati ili wazabuni walipwe mapema, na tusipofanya hivyo watashindwa kuleta pembejeo za msimu ujao na kuathiri uzalishaji wa korosho kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Wizara na Waziri Bashe kwa ubunifu, uzalendo na uchapakazi wake. Allah aendelee kumhifadhi na kumpa afya njema. Nawasilisha.