Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nimpongeze sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein M. Bashe, Mbunge; na Naibu wake Mheshimiwa David Silinde, Mbunge; Katibu Mkuu, Ndugu Gerald G. Mweli; Naibu Makatibu Wakuu, Dkt. Hussein Mohamed Omar na Dkt. Stephen Nindi; na wataalamu wa Wizara na taasisi zote zinazosimamiwa na Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwenye uhitaji wa miche bora ya kahawa na miradi ya umwagiliaji katika Jimbo la Moshi Vijijini ambako hulimwa kahawa, ndizi, mpunga, mahindi, maharage, mbogamboga na matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa kulipatia jimbo langu miche ya ruzuku ya kahawa. Naiomba Serikali iendelee kutoa miche bora ya kahawa kwa njia ya ruzuku kwa wakulima. Bado kuna uhitaji mkubwa wa miche ya kahawa katika Jimbo la Moshi vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha umwagiliaji Tanzania ni mbinu ya kilimo inayotumia mifumo ya kusambaza maji ili kumwagilia mazao badala ya kutegemea mvua pekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kilimanjaro na hasa wakulima wa Jimbo la Moshi Vijijini hujihusisha na kilimo cha mpunga (ukanda wa tambarare), mahindi, maharage, mbogamboga, matunda, ndizi (kanda zote) na kahawa (ukanda wa milimani). Jimbo hili limebarikiwa kuwa na vyanzo vya maji vya uhakika vya asili vinavyotumika kumwagilia mashamba ya wakulima wadogo na wakubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa maji katika kulima kwa tija, naiomba Wizara itusaidie kwenye miradi ya umwagiliaji jimboni kwangu. Nina uhakika tukijengewa miradi nitakayopendekeza, sisi wa Jimbo la Moshi Vijijini tunaweza kubadilisha uzalishaji wa mazao, kipato cha wakulima, na kuchangia kwenye kuleta usalama wa chakula na kuzalisha mazao ya biashara kama kahawa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Umwagiliaji wa Lower Moshi Irrigation Scheme (LMIS) ulijengwa kwa msaada wa Serikali ya Japan mwaka 1987. Mradi huu ni maarufu hapa Tanzania na umesaidia kuongeza tija ambapo uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka kati ya tani 1.8 - 2t/ha za mpunga hadi tani 5.5. Mradi huu una miaka 38 na miundombinu imezeeka, maji yanapotea njiani. Naiomba Serikali ije kufanya uwekezaji kwa kuboresha miundombinu iliyopo na kutafuta chanzo kingine ili maji yaongezeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi wa ukanda wa milimani katika kata 14 kati ya kata 16 za Moshi Vijijini wanatumia skimu za umwagiliaji za asili na wengi wanakabiliwa na tatizo sugu la ubovu wa skimu hizo. Naiomba Serikali ije kukarabati na kujenga mifereji yote ya asili katika Jimbo la Moshi Vijijini ili wananchi wa ukanda wa milimani na kati wanufaike na umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Kibosho Magharibi, kuna kero kubwa ya kukosekana kwa huduma ya maji ya mifereji kumwagilia mazao yao ya kahawa, migomba na mbogamboga. Kwa ujumla, kuna ukosefu mkubwa wa maji ya kumwagilia. Shida hii imesababisha kuchelewesha maendeleo katika eneo la Vijiji vya Manushi na Umbwe lenye wakulima zaidi ya 500. Naiomba Serikali iharakishe ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Makeresho ambayo bado haijapata mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mandaka Mnono katika Kijiji cha Mandaka Mnono. Naiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa skimu hii ili wananchi waanze kunufaika na mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Wizara kwa kutuma wataalamu na kutembelea eneo la ukanda wa tambarare huko Kata ya Arusha Chini. Kwa kuwa tayari tumesajili Chama cha Wananchi Wanaomwagilia Mazao katika eneo hili, naiomba Serikali itekeleze ahadi ya kujenga skimu mpya katika Kata ya Arusha Chini katika Mto Ronga itakayohusisha Vijiji vya Mikocheni na Chemchem ambako kuna takribani 2000 ha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba kilimo cha umwagiliaji kitatoa nafasi kwa wakulima kupata faida kubwa kwa sababu watalima zaidi ya msimu mmoja na kupata mavuno ya juu na mazao yenye ubora. Kumwagilia mashamba kutasaidia wakulima kupata mazao ya uhakika hata wakati wa ukame au vipindi vya mvua kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, ninaunga mkono hoja.