Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuwezesha na kuboresha kilimo. Kilimo ni mkombozi wa Watanzania walio wengi ambao ni wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo, kweli yeye ni jembe. Mawazo yake na mipango yake imeleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo. Mkoani Kagera bei ya kahawa imepaa kutoka shilingi 1,200/= hadi shilingi 5,000 kwa kilo. Haya ni mafanikio makubwa na manufaa makubwa kwa wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ushirika nawapongeza kwa kuendelea kukuza ushirika nchini. Mkoa wa Kagera kuna tatizo kubwa la benki ya wakulima iliyofungwa na Benki Kuu mwaka 2018, eti haina mtaji wa kutosha. Baada ya Benki Kuu kuongeza kiwango cha mtaji wanaotakiwa kuwa nao kama benki, wafanyakazi walifanya kazi kubwa ya kushawishi watu wajiunge na benki hii na wengine walishawishiwa waweke fixed deposit. Mwezi mmoja hadi miwili benki ikafungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki ya Kagera Farmers Cooperative Bank (KFCB) ilifungwa ghafla. Waliokuwa wameweka amana zao, wanalia. Benki ilifungwa mwaka 2018. Walipewa shilingi milioni 1.5 mwaka huo na mwaka 2022 walilipwa 43% ya fedha zao. Wapo wastaafu ambao waliweka kiinua mgongo chao humo, hawakuwahi kukopa toka benki hii ianze. Wako wanalia, hawana mshahara na fedha za kiinua mgongo kimefungiwa benki. Kuna fedha za wakulima, vikundi vya akina mama, kuna fedha za Chama Kikuu cha Ushirika (KCU) na za wafanyakazi, wote wanalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, waliokuwa watumishi wa benki hii hawajalipwa haki zao za kiutumishi. Walilipwa nauli isiyozidi shilingi 150,000, leo ni miaka minane wanateseka. Wanazunguka ofisi nyingi, lakini hawajapata suluhu. Waliniletea tatizo lao ili nilifikishe kwa Mheshimiwa Waziri, nikaenda Tume ya Ushirika, nimefika Wizara ya Kilimo, Waziri hakuwepo, nikaongea na Katibu Mkuu, nimeenda Benki Kuu Kitengo cha Ufilisi, kote sijaona dalili ya suluhu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa nini badala ya kuifilisi benki hii, hawakuiunganisha KFCB na mabenki mengine ili kulinda mitaji ya wakulima, wastaafu na wote waliokuwa wameweka fedha zao humo?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri Bashe atutatulie hili tatizo. Ni mwiba mkubwa Mkoani Kagera. Watu walioathirika wanaumia na wanapiga simu kila wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, hawa wahanga ni lini watalipwa fedha zao? Ni lini waliokuwa watumishi wa KFCB watalipwa haki zao za kiutumishi wakati taratibu nyingine zinaendelea? Je, Serikali haiwezi kutafuta fedha mahali fulani, wakawalipa wahanga hawa ambao hawakuwa na hatia, tukaondoa huu mwiba?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up alizungumzie, awatie moyo, maana maumivu ni makali na wana hasira kali, please.