Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii kuungana na Bunge lako Tukufu, kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka wa fedha 2025/2026. Mtu anayefanya vizuri anapaswa kupongezwa, anapaswa kutiwa moyo na kuungwa mkono hadharani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na Bunge zima, kwanza, kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais ni mwanamapinduzi wa uchumi wa kijani, tangu ameingia madarakani katika kipindi chake cha miaka minne, kila mmoja amekuwa shuhuda katika eneo lake namna ambavyo amefanya mabadiliko makubwa katika Kilimo. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu wa pili na muhimu sana kumpongeza ni Waziri, Mheshimiwa Hussein Bashe, ni Waziri mwenye maono, mbunifu na mwenye uthubutu. Amekuwa ni mtu ambaye anajaribu kufanya kila linalowezekana na yupo tayari kukosolewa ili mradi lile jambo liwe bora kwa faida ya wakulima hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nimejifunza sana kwake na moja ya jambo kubwa kwenye Wizara yetu alilolileta ni kufanya kazi kama teamwork na ndiyo maana leo unaona haya yote ni matokeo ya kufanya kazi as a teamwork. Unavyomwona Waziri wangu, ndivyo alivyo Katibu Mkuu, ndivyo walivyo Naibu Makatibu Wakuu, ndivyo walivyo Wakurugenzi na Maafisa wote wa Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo, hili niliona ni vizuri niliseme kwa sababu teamwork ndiyo ambayo imetufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, alituelekeza kuwekeza katika Kilimo cha umwagiliaji, wakati anaingia madarakani. Leo hii tunavyozungumza hapa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anaingia madarakani, mwaka wa fedha 2020/2021 kulikuwa na miradi 13 tu ya umwagiliaji, leo tunavyozungumza kuna utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji 780 ndani ya miaka minne.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, alisema wazi kabisa kwamba anataka twende kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa sababu kubwa mbili; Kilimo kinahitaji maji, hakihitaji kutegemea mvua peke yake. Tuondoke kwenye kilimo cha bahati nasibu ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais, ameyaweka kwenye Wizara yetu na ndiyo maana alipandisha bajeti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Wakati anaingia ilikuwa shilingi bilioni 46 peke yake. Leo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha huu tunaokwenda kuumaliza ilipokea shilingi bilioni 403 ambazo zinaendeleza uwekezaji kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, wakati Mheshimiwa Rais, anaingia madarakani eneo la hekta ya umwagiliaji nchini lilikuwa chini ya hekta 700,000 nchi nzima. Hiyo ni miaka 60 tangu tumepata uhuru. Mheshimiwa Dkt. Samia, sasa hivi anatekeleza miradi yenye ukubwa wa hekta 534,000 ndani ya miaka minne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaona kabisa kwamba lengo lake ni kuhakikisha kilimo kinakuwa cha uhakika, tulime throughout the year ili tulete tija kwa wakulima wetu. Mheshimiwa Rais, ametuelekeza vilevile kwamba tununue magari kwa ajili ya kuchimba visima ili tuweze kumsaidia mkulima mdogo mdogo kule chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaona juzi tulikuwa tunapokea magari saba ya umwagiliaji ya kwanza yameshafika, mengine 11 yapo baharini na bodi zetu tumeshazielekeza na zenyewe zitakuwa zinanunua magari ili tuweze kuwafikia wakulima kwenye kila mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya oparesheni tunayokwenda kuifanya hapo mbele, haya magari sisi hatutagawa kwenye Mkoa, yaani tunaondoka na gari zetu zote, tukifika kama ni Mkoa wa Songwe magari yanafanya kazi yanamaliza pale, yanahamia mkoa mwingine. Tunataka kuona tija katika kilimo kama Mheshimiwa Rais, alivyotuelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alituelekeza baada ya kuona changamoto kubwa katika bei za mazao hapa nchini, akasema sasa tubadilishe mifumo, twende katika mifumo ya kidijiti ili mkulima apate bei rafiki ambayo inaweza kumsaidia. Leo hii unaweza kuona watu wamekuwa wakizungumza hapa na nitatolea mfano baadhi ya mazao. Kwa mfano kahawa kabla ya mfumo wa kidijiti wa kutumia TMX Kahawa ilikuwa chini ya shilingi 1,000, au shilingi 1,200. Leo Kahawa imefika shilingi 6,000 kwa kilo, yote haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kokoa, bei ilikuwa chini ya shilingi 8,000 wakati Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaingia madarakani, leo kokoa tunauza kati ya shilingi 24,000 mpaka shilingi 34,000 kwa kilo moja. Sasa fikiri haya ni mabadiliko madogo tu kwamba sasa tunabadilisha mifumo, kilimo cha mazoea ambacho watu walikuwa wanakiishi miaka mingi. Leo hayo ndiyo matokeo ya uwekezaji na maelekezo ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mbaazi wamezungumza Wabunge. Mbaazi ilikuwa inauzwa kilo mpaka shilingi 100, leo kwenye mbaazi tumefika shilingi 3,000. Kwenye korosho tulikuwa chini ya shilingi 2,000, leo korosho tumefika mpaka shilingi 4,200. Sasa haya yote yanayofanyika ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tubadilishe mifumo ili tupate bei nzuri na masoko ya uhakika kwa wakulima wetu. Safari bado inaendelea, kazi bado inafanyika, na ndiyo maana mnaona haya yote yanatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, hata ukiangalia kwenye mauzo ya mazao nje ya nchi, wakati Rais Mheshimiwa Dkt. Samia anaingia madarakani, mauzo ya nchi mwaka 2021 yalikuwa dola za Kimarekani bilioni 1.2, uki-convert kwa wakati ule ilikuwa kama shilingi trilioni tatu. Leo katika mwaka wa fedha 2024/2025 mauzo ya nje yamefikia wastani wa Dola bilioni 3.54 za Kimarekani, sawasawa uki-convert kwa leo ni zaidi ya shilingi trilioni 9.6 fedha za kigeni zinazotokana na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ni mambo ambayo Mheshimiwa Rais, ameelekeza, utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na ninyi Wabunge mmeona matokeo ambayo yanaendelea kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alituelekeza vilevile tuanze kutoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo ili tuweze kumsaidia mkulima mdogo kuongeza tija na uzalishaji. Sasa matokeo yake leo kwenye hizo tija ambazo tumeziongeza kwa kutoa ruzuku kwenye pembejeo kwa maana ya mbolea, mbegu na viuatilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati anaingia madarakani mwaka 2020/2021 mahindi tulikuwa tunazalisha tani milioni 6.4 kwa mwaka. Leo katika mwaka huu uliokwisha tumezalisha tani milioni 12.2, mwaka wa fedha 2023/2024, hayo ni matokeo ya kuongeza ruzuku kwenye pembejeo. Ndani ya miaka minne tume-double na leo tumekuwa nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa mahindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaona kabisa kwamba kumbe kilimo kinahitaji uwekezaji. Kilimo kinahitaji uthubutu, kilimo kinahitaji watu wenye maono ndiyo maana unaweza kuona tu mambo yanatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo kwenye korosho kupeleka tu viuatilifu, ruzuku ya viuatilifu kwenye korosho; uzalishaji umetoka tani 210,000. Leo tunavyozungumza, tumefikia tani 528,000 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.598. Fedha hizo zimekwenda kwa mkulima wa korosho. Haya yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ambao leo Watanzania wanaona kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, Mheshimiwa Rais, vilevile alituelekeza kwamba, Benki ya Ushirika ambayo ndiyo ingeweza kuwasaidia wakulima moja kwa moja na wanaushirika, ambayo imekuwa ikielezwa muda mrefu kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, akasema nataka kabla hatujakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, Benki hii iwe imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi wote ni mashahidi, tarehe 08 mwezi wa Nne, mwaka huu Rais mwenyewe amezindua Benki ya Ushirika, ambayo inakwenda kuleta mabadiliko makubwa kwa wanaushirika na wakulima kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaona kabisa kwamba kuna dhamira ya dhati na ya kweli katika sekta ya kilimo ambayo inatokana na mwanamapinduzi wa ukweli ambaye ni Mheshimiwa Rais, ameweka uwekezaji mkubwa sana katika sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tutaendelea tu kuwaomba Bunge Tukufu, mtupitishie hii bajeti ili twende tukatekeleze yale ambayo tumeyaanza, yapo katikati, tuyamalize yale ambayo tunakwenda kuyaanza upya, lakini yote uwekezaji huu na niwaambie kabisa kabla ya mwaka 2030 matokeo yake yatakuwa ni makubwa sana na watu wataanza kuona sasa kweli kilimo ndiyo game changer wa uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tumepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais, sisi Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI tuhakikishe tunakuja, tuna model yetu inaitwa Morogoro model. Sasa tutapeleka kilimo kwa wanafunzi wa shule za msingi na wanafunzi wa sekondari katika yale mazao ya kibiashara kama karafuu ama kokoa. Yaani mwanafunzi atapewa mche, tutagawa bure kwa kupitia taasisi yetu COPRA ndiyo wamepewa hilo jukumu. Atapewa mche kama ni wa karafuu, atakuwa anamwagilia, unapanda pale nyumbani kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, mche mmoja wa karafuu ukikua, unampa mkulima wastani wa shilingi milioni moja mpaka milioni tatu kwa mche mmoja. Ukiwa na miche 10, maana yake una wastani wa kati ya shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 30 unapokuwa umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake ni nini? Utamsaidia mwanafunzi yule aweze kujimudu mpaka anapokuwa mtu mzima. Kwa hiyo, hayo ndiyo malengo yetu na ndiyo vision ambayo tuliyonayo sasa hivi kuhakikisha tunakwenda kubadilisha kila kitu katika Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana leo kila mmoja hapa anaweza akazungumza na akaona ukweli kabisa kwamba hiki kinachofanyika ni kwamba tulijaribu kuangalia wapi kwenye programu za kilimo zilizofeli, kuanzia “Kilimo ni Uti wa Mgongo”, “Kilimo ni Siasa”, “Kilimo ni Kujitegemea”, na “Kilimo Kwanza.” Yote yale sisi tuliangalia ndiyo maana tukaja tukasema hapana, sasa tuna-change direction totally, na hii direction tunayoibadilisha ndiyo pekee inayoweza kubadilisha maisha ya Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kabla ya mwaka 2030 kilimo kitatoa malighafi kwa 100% kwenye viwanda vyetu hapa nchini. Nchi zote ambazo zimeendelea za viwanda, nchi za viwanda hawakuanza tu kutengeneza viwanda bila ya kuwa na malighafi, waliwekeza kwenye kilimo, wakapata sana kilimo, wakagundua kwamba no, sasa tunataka tutoke kwenye kilimo kwa kuongeza thamani, ndiyo wakaleta viwanda. Ndio maana ukienda kusoma Industrial Revolution ilitokana na green revolution katika Europe wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mtu yeyote hawezi kutuambia kwamba tusiwekeze kwenye kilimo kwa maana ya mashamba makubwa, tusiwekeze katika Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika ngazi ya halmashauri, eti kwa sababu tunachukua maeneo makubwa. Tutafanya hivyo kwa sababu ndiyo njia sahihi na pekee ya kumkomboa Mtanzania wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba mtu yeyote ambaye anasema atamnyima kura Mheshimiwa Rais, kwa kutenda wema huu, basi ninaamini atakuwa hana anachokiona katika maisha yake. Maana yake mtu huyo hata ungemfanyia nini, hawezi kutoa kura, lakini hiki kilichofanyika kimekusudia kubadilisha maisha ya mwananchi mmoja mmoja wa kawaida hususan Mkulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kusema maneno hayo machache, nami nikushukuru sana kwa kuongoza Bunge vizuri na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)