Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi. Pili, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema iliyotuwezesha kufika hapa leo, kutekeleza kazi hii na kumalizia jukumu lililo mbele yetu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa support anayotupa katika kutimiza majukumu ambayo ametugawia sisi kama wasaidizi wake. Vilevile, niwashukuru sana Naibu Waziri wangu ndugu yangu Mheshimiwa Silinde, kwa kuchangia na kujibu baadhi ya hoja na kutoa clarification. (Makofi) 
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru kwa dhati kabisa kwa support anayonipa mimi Waziri wake na ushirikiano na mahusiano ambayo tumekuwa tukijenga. Namshukuru Katibu Mkuu, nawashukuru wataalamu wote wa Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii kusema kwamba kwanza pongezi zinazotolewa kwa Wizara ya Kilimo anayestahili wa kwanza ni Mheshimiwa Rais, kwa sababu mimi kama Waziri, na bahati nzuri Waziri wa Fedha yupo hapa, anafahamu kwamba kukiwa na changamoto yoyote ni kwa namna gani huwa anakuwa summoned Waziri wa Fedha kwa ajili ya kuhakikisha shughuli za kilimo zinakwenda hasa zinazohusiana na matatizo ya wakulima wadogo. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hizi pongezi nataka niseme tu kwamba Watumishi wa Wizara ya Kilimo wanastahili hizi pongezi, ni za kwao. Wanafanya sana kazi nami mbele ya Bunge lako Tukufu. Nawashukuru sana kwa support ya ushauri wanayonipatia kama Waziri. 
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa uchache, mara nyingine huwa wanakuwa wakali sana kwangu kama Waziri pale ambapo kuna mambo ya kitalaam, mimi na wao tunatofautiana, mahali ambapo nataka matokeo yatokee kesho, wenyewe huwa wanakuwa wakali sana. Nami nataka niwatie moyo, wawe na haki ya kunikosoa mimi kama Waziri ndani ya boardroom, kwa sababu ni wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge. Katika Bunge hili nimekuwa Naibu Waziri chini ya kaka yangu Mheshimiwa Hasunga, yule pale. Nataka niseme tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 270 hivi, au shilingi bilioni 280, tulikuwa tunapata disbursement asilimia 30 na yeye yule pale shahidi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunakuja hapa pressure juu, tunalalamika tuna maumivu, hakuna fedha, lakini nimefanya kazi chini ya Mheshimiwa Prof. Mkenda, tukawa na shilingi bilioni 297, tukasema mimi na Mheshimiwa Prof. Mkenda hatuna hela. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hela allocation iliyoko ni shilingi bilioni 290 something, tupeleke wapi fedha? Tukasema tuwekeze kwenye utafiti tu angalau tutafsiriwe kwenye suala la utafiti na ugani. Ndiyo dhana ya kuanza kufanya reform ya research ilikoanzia pale. Hatukuwa na fedha, disbursement ilikuwa isiyozidi 60%, au 70% ya shilingi bilioni 290. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaelewa sana Waheshimiwa Wabunge kwa hoja ya kwamba kweli hakujawa na disbursement inayotakiwa ya hundred percent. Ni matamanio ya kila mtu, lakini nataka niwatie moyo six hundred billion shilling tuliyoipokea mpaka Aprili na tumeendelea kuwa na engagement na mwenzangu Waziri wa Fedha tunatarajia kuendelea kupata fedha ndani ya mwezi huu wa Tano, tutapata fedha mwezi wa Sita. Ninaamini kwamba tutakapoumaliza mwaka huu wa fedha, sehemu kubwa ya matarajio yetu yatakuwa yamepatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu mkubwa ni kutafuta fedha nje ya mfumo rasmi wa kawaida. Namshukuru Waziri wa Fedha, namshukuru ndugu yangu Waziri wa Mipango, wametukubalia kutengeneza taratibu za kutafuta fedha katika njia ambazo siyo za kawaida kutegemea kapu moja tu la Hazina. 
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeanza kupata fedha kutoka World Bank, na juzi ametusaidia kutupitishia fedha kwa ajili ya kupewa kutoka World Bank, zaidi ya dola milioni 54 ambazo zitaenda kwenye mabwawa hundred percent, hizi fedha zote zitaenda kwenye mabwawa. Ametuidhinishia, tumepata fedha kutoka World Bank dola milioni 300 za P4R, tutakazoanza kuzitumia katika sekta ya kilimo. Hii ni njia mpya ya kutafuta fedha katika mfumo ambao siyo wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wakati Mheshimiwa Rais anazindua Benki ya Ushirika, tumepata fedha kutoka African Development dola milioni 120 na kidogo ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo. Hizi ni fedha ambazo tunaenda kuzitumia kwenye Programu ya BBT na agricultural financing. Tumepata fedha vilevile kutoka IFAD zaidi ya dola milioni 40. Hizi fedha zitaanza kuonekena matumizi yake kuanzia mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haikuwa kawaida, Mheshimiwa Hasunga, yupo hapa na ninyi Wabunge mmekuwa mfano mliokuwepo hapa kwa muda mrefu. Haikuwa kawaida Wizara ya Kilimo kuidhinishiwa kupata fedha kwa mfumo wa P4R ambao unatumika katika sekta ya elimu. Haikuwa kawaida. Nasi ndio tutakuwa moja ya nchi ya Afrika ambayo inatumia P4R modal kwenye agriculture. Kwa hiyo, namshukuru sana Waziri wa Fedha, ni matamanio yetu sote tupate hundred percent. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri pale Wizara ya Fedha nina kabechi kwa PST, kwa Kamishna wa Bajeti, kwa Kamishna wa Madeni na kwa Waziri mwenyewe naenda bila appointment, nitakaa kwenye foleni kuhakikisha kwamba tunapa fedha. 
Mheshimiwa Naibu Spika, niwatieni moyo, tutapata fedha za sekta ya kilimo kwa sababu nao wameona remittance za agricultural export, wameona namna gani uchumi wetu umekuwa imara, umekuwa stable wakati tuna Covid hii nchi, wakati kuna matatizo ya dunia. Wengine wakiingia kwenye matatizo, sisi bado uchumi wetu ulikuwa imara, ni kwa sababu ya uimara wa sekta ya kilimo. Kwa hiyo, naomba niwatie moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zimesemwa hoja nyingi na Waheshimiwa Wabunge, nami nitajaribu kuzijibu baadhi. Katika hizi hoja, moja ya hoja ambayo imeongelewa na ninaomba tu niseme kwa ufupi, Mheshimiwa Asenga, kuhusu issue ya Wakulima wa Kilombero, nataka tu niwahakikishie, tulikaa mimi na yeye, niliambie Bunge hili Tukufu akiwepo Mheshimiwa Londo, AMCOS zote za Bonde, Kiwanda cha Kilombero. Tulikubaliana tunaita gentlemen agreement, tu-form timu ya wataalam ambayo itaongozwa na Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo, TBS, Wakulima na Kiwanda. Timu tumeshaunda na inaendelea na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusubiri matokeo ya timu, tusikihukumu kiwanda kabla ya matokeo ya timu. Nikuhakikishie wewe na wakulima wote, maslahi ya wakulima yatalindwa bila uwoga wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wakulima waliokatiwa mazao yao ya kakao niombe tu, tupewe fursa, nitakaa na wenzangu wa Wizara ya Maliasili, tutakaa na Serikali ya Mkoa tutapata solution kwa tatizo hili tuweze kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee, zao la pamba. Amesema Mheshimiwa Boni, amesema kaka yangu Mbunge wa Sengerema na wameongea wengine. Mimi ninatoka kwenye pamba na tumbaku. Cha kwanza, niongelee hapa hapa, niseme ukweli, kama sisi wanasiasa tunaotoka kwenye ukanda wa pamba, na viongozi tunaotoka kwenye ukanda wa pamba hatutakubali kubadilika na kuheshimu sayansi kwenye pamba na kuigeuza pamba kuwa zao la siasa, hatutaondoka kwenye umasikini wa wakulima wa pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya msingi ya pamba; moja, ni kukataa sayansi. Tunaambiwa tusichanganye mazao ndani ya pamba. Wote tunafahamu kule Usukumani tunakubaliana kwenye vikao vya ndani, tukienda kwenye mikutano ya hadhara, kuna yale maneno, “kwani wewe shamba la kwako? Mwache tu achanganye pamba na mahindi.” Hawezi kupata tija. Hoja ya pamba siyo bei tu, hoja ya pamba ni tija. Nami nataka niwape takwimu ili tukubaliane sote kubadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie, waulize ndugu zangu wa tumbaku wa Tabora, tulikamatana na nikawaambia wanasiasa wenzangu wakae pembeni. Leo tumbaku imenyooka, kila mmoja anashangilia. Sasa zao lililobaki kwenye nchi hii ni haya mawili. Mamlaka yangu kama Waziri wa Kilimo yanaisha baada ya kuapishwa mwingine. Nina pamba na chai, na nikimaliza hapa nakuja kwenye pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi, naomba tusikilizane. Wakati sisi leo bei yetu ni shilingi 1,150, pamba hailimwi Tanzania peke yake, Zambia wanalima. Mkulima wa Zambia anapata shilingi 800, mkulima wa Malawi anapata shilingi 864, mkulima wa Msumbiji anapata shilingi 918, tumezi-convert kwenye shilingi, Mkulima wa Zimbabwe anapata shilingi 800, na hawa wote hawapati ruzuku ya aina yoyote kutoka Serikali zao. Kwa nini? Hakuna kelele, wanapata kwenye ekari moja zaidi ya kilo 1,500 mpaka kilo 2,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaenda kule tunatuma watalaam, na wanasayansi tunasema kwamba plant population kwenye ekari ifike angalau miche 44,000 mpaka 50,000. Tunaenda kufanya mikutano ya hadhara tusizuiliwe, wewe weka na mahindi ukitaka. Wallah, nitawaweka ndani watu. Nataka niwe mkweli. Kwenye hili, nataka niwe mkweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Brazil mkulima mmoja kwenye hekta anapata kilo 6,500. Mwaka 2024 nilivyotangaza tunaanza Programu ya BBT kwenye kilimo cha pamba na tunapeleka matrekta tumewalimia wakulima wa pamba kwa shilingi 35,000/= kwa ekari, tumewapelekea mbegu na dawa. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu sasa hivi wapo Mahakamani. Mbegu tunazo, wapelekewa, wanazichukua kwenda kuzipeleka kwenye ginnery kuzikamua mafuta. Wanaenda kuzikamua mafuta, ukimkamata unapigiwa simu na kila mtu unayemjua. Lazima tubadilike watu wa pamba kama tunataka kubadilika. Nimewaambia wataalam waweke hapo kwenye screen mwone. Mwaka 2019/2020, 2018/2019 tulifika tani 340,000 ya pamba. Ilifia humu ndani, Waziri wangu Mheshimiwa Hasunga yule pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa Manaibu Waziri wawili, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, wakati huo Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru, ameita vikao BoT, ameita wapi, Ofisi Ndogo ya Lumumba, nani waliiua. Sisi wanasiasa! Tukamdanganya Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, tukamdanganya Waziri Mkuu, Waziri Mkuu akaenda akaita vikao pale Mwanza mpaka saa saba usiku. Tubadilikeni wanasiasa tulioko kwenye ukanda wa pamba. Huu ndiyo ukweli mchungu, lazima tubadilike, tukubali kilimo ni sayansi siyo magadala. Hili ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka BBT, kelele! Tumbaku leo inashangiliwa, ni contract farming. Tunachokitafuta leo, tuna mkulima amepewa trekta na Mheshimiwa Rais amefika kilo 2,200 hapa hapa Tanzania na yupo Mkoa wa Shinyanga. Kwa nini, ametumia mbolea? Amefuata utaratibu wa kisayansi kapanda miche 44,000 kwenye shamba lake, kapata kilo 2,200.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila tukiongelea kichaka chetu, wakulima wa pamba wanaibiwa, anayetaka kuniletea mnunuzi akatayenunua pamba shilingi 3,000/= nitampa mkataba yeye pekee yake aje anunue, haipo. Nataka niwaambieni kwa nini haipo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya dunia leo ni senti 64 dola, CIF price. Mwaka 2024 wakati sisi duniani iko senti 75 bei yetu elekezi ilikuwa shilingi 1,200 ikafika mpaka shilingi 1,400 na tulitumia ushirika kuipandisha hii bei kufika shilingi 1,400. Mwaka 2023 ilifika shilingi 2,000; pamba bei ya dunia ilikuwa dola 1.16. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, cha kwanza tufahamu kwamba bei ni function ya supply and demand, huo ndio ukweli. Tunachotakiwa sisi kupambana nacho ni tija na kuongeza thamani. Serikali inachukua hatua gani? (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, tumeleta ruzuku ya dawa, mbegu, matrekta kwenye pamba tumepeleka ugani. Mwaka huu 2025 tutatoa tani 149,000, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutafika tani 400,000, au 450,000 za pamba. Nawaomba tusiende kuivuruga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya nini kama Serikali? Tunaenda hatua ya pili, tunafanya value addition. Tumeongea na Wizara ya Afya, tumekubaliana tunajenga industrial park ya kwanza Simiyu. Tumeshakubalina kutakuwa na ekari 1,000, tutaanza kujenga pale kama tulivyoanza kujenga Malanje, tutatoa ruzuku ya umeme, tutapeleka maji, na Serikali itaanza kujenga infrastructure ya maghala. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo linaongelewa sana kuhusu wawekezaji. Hawa wawekezaji ni akina nani? Lazima uchumi huu ushikiliwe na wenye nchi, ndiyo Taifa hili litakuwa salama. Tukifanya makosa ya kuhakikisha uchumi wote unashikiliwa na foreigners, hautamsaidia Mtanzania wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajenga industrial park pale Simiyu ya kwanza ya pamba. Tutazuia importation ya vifaatiba vinavyotokana na pamba na Serikali itaweka fedha kwenye hili eneo. Tutazuia importation ya kamba za kufungia tumbaku. Tunatumia zaidi ya dola milioni 19 kuingiza hivi vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishaanza kuongeza thamani, Mwalimu Nyerere alijenga ginnery Igunga, akajenga kiwanda cha nyuzi Tabora, tumerudi wenyewe nyuma kwa sababu tuliamua as a policy kufanya wrong privatization, that is the truth. Huo ndio ukweli, dunia imetufundisha, tunarudi kwenye misingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunasema magodauni ya SHIRECU yaliyopo pale bandari na magodauni ya Bodi ya Pamba yafanyiwe uthamani? Ipatikane pesa, hiyo pesa ndiyo tutaenda kufanya uwekezaji, na pale tunaenda kujenga kiwanda cha kuchanganya mbolea. Nyerere alijenga Kiwanda cha Kuchanganya Mbolea Tanga akaweka bomba kutoka bandarini kuingia kiwandani, tulikiuza. 
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaenda kuwekeza kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa kutumia maghala yaliyokuwa yanamilikiwa na Bodi ya Pamba na maghala yaliyokuwa yanamilikiwa na SHIRECU na niwahakikishie, wana Ushirika wa SHIRECU, na SHIRECU inapata bilioni moja kwa mwezi au milioni 900.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, kwa mujibu wa Kanuni, ninaongeza muda kidogo. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, SHIRECU inapata karibu bilioni moja. Hizi fedha wanazitumia kwa matumizi ya kawaida tu, hawawekezi popote, zinaishia vikao, mikutano, posho. Tunafanya nini? Kweli mnataka niiache SHIRECU namna hiyo? It will be very wrong for this country. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme tu kwamba wakulima wa pamba tutahakikisha tunawasaidia waongeze tija na vipato vyao viweze kuongezeka. Huo ndiyo mwelekeo wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limeongelewa sana na Wabunge ni eneo la mitaji kwenye sekta ya kilimo (agricultural financing). Mheshimiwa Mpakate, amesema kuhusu akaunti za wakulima zinakuwa dormant baada ya muda mfupi. Niseme tu kitu kimoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, namshukuru Waziri wa Mipango na timu nzima ya Planning Commission, tumekubaliana na ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais tuunde timu ya pamoja kwa ajili ya kutengeneza technical team kwa ajili ya kuandaa Agricultural Financing Policy. Lazima tuwe tuna sera ya ukopeshaji kwenye kilimo. Kilimo hakikopeshwi kama kuuza vitu vingine, ni tofauti kabisa. Kwa hiyo, sera itakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Benki yetu ya Ushirika tunachukua hatua gani? Tunashirikiana na Commercial Bank, nami niwashukuru sana. Namshukuru Majid, Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika. Namshukuru sana, nawashukuru NMB, nashukuru benki zote za Commercial Bank. Leo hii wanatoa mikopo na mikopo hii wanayotoa kwenye input haina guarantee yoyote, ni kuaminiana na ni makaratasi tu, na ninawashukuru sana kwa hatua hii, tumefika shilingi trilioni nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachukua hatua gani? Tutashirikiana Tanzania Agricultural Development Bank, Agricultural Trust Input (AGITF), tutashirikiana na Benki yetu ya Ushirika. Tutaanzisha window ndani ya Benki ya Ushirika itakayokuwa na mambo matatu. Moja, itakuwa ina guarantee scheme kwa ajili ya wakulima wadogo ambayo watakopeshwa kwa kiwango kisichozidi asilimia saba, lakini vilevile itakuwa na equity fund na itakuwa na direct land. (Makofi) 
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali kupitia AGITF tunatafuta fedha. Mfano kama sasa hivi tunawapelekea shilingi bilioni 17 Agricorp Bank ambayo inaenda kama guarantee ili wao watoe mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 51 kwa riba isiyozidi asilimia saba. 
Mheshimiwa Naibu Spika, ile inaenda kama dhamana, hatutaki kui-distort bank kufanya commercial function yake, lakini tunaanzisha dirisha maalum ndani ya Benki ya Ushirika ili iweze kuwahudumia wakulima kwa riba ndogo na nafuu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na African Development Bank kwenye fedha alizotuidhinishia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, nami niseme hapa, na Waziri wa Fedha anasikia, kama AFDB hawatakubali kufuata utaratibu wetu, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu huo mkopo tusiuchukue kwa sababu hawatupatii msaada, wanatupatia mkopo kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, agricultural financing fedha yake yote itaenda AGITF na Coop Bank, itaenda kuwekwa kama guarantee na equity fund dola milioni 35. Hizi fedha zote zitaenda kuwakopesha wakulima kwa kiwango kisichozidi asilimia saba. Tumefungua window, tutaziruhusu commercial bank zinazotaka ku-access hizo fedha, tutawapa ili waweze kuwakopesha kwa masharti tunayotaka sisi, siyo masharti wanayoyataka wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili, najua litaleta mjadala sana kwenye sekta ya fedha kama Waziri, I will be ready to face that discussion, lazima mfumo wa ukopeshaji ubadilike katika sekta ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa ninataka niseme kuhusu BBT, ninawashukuruni sana, BBT is a program, ita-evolve, itabadilika. Nilikuja na wazo la block farm, mmeshauri sana, sasa tumeenda kwenye Halmashauri, tumeenda kwa wakulima wadogo, tutaendelea kubadilika. BBT maana yake nini? Nia na madhumuni ni kuhakikisha kizazi kijacho cha nchi hii kinamiliki mali yake, kinamiliki ardhi yake, kinamiliki uchumi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilitaka niseme kuhusu umwagiliaji. Kama nchi hatutaamua kuwekeza kwenye eneo la umwagiliaji kwa nguvu, kwa muda mrefu hatutawaondoa maskini walioko kwenye sekta ya kilimo kwenye umaskini wao. Hili ni muhimu sana na hapa nimeorodhesha miradi pamoja na ile 780 ambayo tunaendelea kutekeleza. 
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wanasema, kwa nini usifanye kidogo ili matokeo yaonekane? Hebu naomba kuuliza, hiyo kidogo nianzie wapi? Yaani ni wapi wakubali kusubiri wakati kidogo inakuja? Nadhani tusiogope kuvamia hii bahari kubwa. Tuogelee kama tuna-plan, tutafika mwisho na tutatoka mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tumetangaza feasibility study na detail design ya mradi wa Lake Tanganyika na Lake Victoria. Huu mradi utakuwa ni wa jumla ya hekta milioni tatu, na ninataka niwaambie nendeni mkasome kuna mradi unaitwa The Largest African Irrigation Scheme, inaitwa Gezira Scheme. Ipo wapi? Ipo Sudan, imeanza kujengwa 1904, ina hekari milioni tatu. Wameijenga kwa zaidi ya miaka 100. The largest Irrigation Scheme, inaitwa Gezira. Tusiogope kuwekeza kwenye umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimeorodhesha mabonde yote na maeneo yana jumla ya hekta 5,383,850 na yote haya yanaenda kufanyiwa feasibility study na detail design na yataanza kujengwa ili yasiishie njiani. Niwaambie tu wote mjue, kila bonde tumeanza heka 500, heka 1,000, heka 2,000, yatamalizwa tu, hata sisi wote tusipokuwepo humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere alifikiria kizazi kinachokuja, hakufikiria kizazi chake. Tuombe kwa Mwenyezi Mungu, tuache kufikiria leo, tufikirie wanaokuja kwa sababu we are surviving, kuna wengine walifikiria on our behalf, hii ndiyo njia pekee ambayo inaweza kutuondoa kwenye matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya mabonde yote Mheshimiwa Rais kaidhinisha, tuendelee. Irrigation ya Victoria kaidhinisha tumeshaanza, tumeshatangaza feasibility study na detail design, tumeanza kujenga kule kwa Prof. Muhongo, tumeanza kujenga Ngono. Ngono waliofanya visibility study ya kwanza, wamekufa, hawapo. Tusiogope, this is the right direction, tuna Mheshimiwa Rais, tunaenda kwenye uchaguzi mwezi wa Oktoba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu atashinda, atarudi ana commitment na wakulima. We have this advantage, tuitumie kwa ajili ya wakulima. 
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua kununua mbolea kwenye viwanda vya ndani, tani 200,000 za mbolea. Tunaanza mwaka kesho, zitakuwa ni targeted subsidy program, haitaathiri ile ruzuku. Wote wanaofikiri kwamba tunatoa ruzuku kwa bahati mbaya, it is well calculated. 
Mheshimiwa Naibu Spika, ruzuku ya mbolea ni well calculated, ruzuku ya mbegu tuliyoianza ambayo tumeianza mwaka huu imepata changamoto, na ninyi mnakumbuka tulivyoanza ruzuku ya mbolea ilikuwa ina changamoto. Leo we are all happy. ruzuku ya mbegu, na nimewaambia juzi makampuni sitasita kumfutia leseni hata awe kampuni ya Kimataifa, atafuata utaratibu tunaotaka sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ruzuku ya matrekta tunaanza, mwaka huu Mheshimiwa Rais katuidhinishia kuanzia mechanization center 1,000, trekta 10,000. Kwa Wilaya za uzalishaji tuna uwezo wa kupeleka kila Wilaya zaidi ya trekta 50, kila Wilaya zitaenda kulima kwa ruzuku, siyo kwa bei ya soko, ni kwa bei ya ruzuku na hii inaanza mwaka huu. Siyo bahati mbaya, it is well calculated.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaanza kuchimba visima kwa ruzuku kwa sababu sisi tutapata fedha kwenye mazao yatakayotoka. Hatuhitaji kupata fedha kuliko kwenye uchimbaji wa kisima. Wakulima wadogo, maskini watachimbiwa bure kwa sababu ndiyo wameibeba hii nchi kuifikisha hapa ilipo. Tutaujenga ushirika kwa nguvu, wezi tutawafunga, ushirika hatuufuti, tutaendelea kuujenga pole pole ili uweze kuushikilia uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, nami niseme tu, Bunge hili litaenda kwenye uchaguzi likiwa limeacha msingi imara kwenye sekta ya kilimo. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zao la chai, nataka tu niseme, wataalam wa Wizara ya Sheria wa Kilimo wanamwandikia AG, tunampelekea AG, tutatumia sheria za nchi hii kuyachukua yale mashamba kwa maslahi ya umma. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi, nami nawaambia hatuwezi DN na wenzake kwa sababu tu wanaitwa wawekezaji kushikilia nchi hii kuwa mateka for a very long time. Tumewapa option ya kuyachukua yale mashamba, Mheshimiwa Rais kaagiza, ongea nao uyanunue yale mashamba, imekuwa shida. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni zote zilizomilikishwa, ninawashukuru WATCO nataka tu niwaambie watu wa Rungwe, Mwenyekiti wa Bodi ya Chai yule pale juu, Majid, nimeshampa maelekezo. WATCO wamekubali, tunakinunua kile kiwanda, tunakikabidhi kwa wakulima wadogo, watamilikishwa viwanda vile. Tumeshanunua viwanda viwili, vinakuja kwa ajili ya kufungwa kwa wakulima wa Rungwe na Kilolo kwa ajili ya kuchakata chai. Chai tuna changamoto, lakini tutazimaliza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa dhati na kuwapa commitment ya Wizara ya Kilimo, tutaendelea kufanya kila ambacho kimo ndani ya uwezo wetu kuondoa matatizo yanayoikabili sekta ya kilimo. Hayataisha leo, yataendelea kuwepo, tutaendelea kukabiliana nayo kwa sababu tuna Jemedari Mheshimiwa Rais mwenye nia thabiti ya kuwalinda wakulima nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja, nashukuru sana. (Makofi)