Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mchangiaji kwenye Wizara hii. Sasa ninaomba nianze kwa sababu ya umuhimu wa muda, kwanza ninaomba kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninampongeza kwa sababu ya kazi yake kubwa ya kuhakikisha kwamba analinda na anadumisha mahusiano yetu na Jumuiya za Kanda na Jumuiya za Kimataifa, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema kwenye taarifa tunamshukuru kwa kuzindua sera hii ya mambo yetu ya nje kwa sababu ndio kioo, kule nyuma kama Kamati tuliwahi kusema kwamba Wizara hii ndiyo kioo na ili kiwe kioo lazima sera zake ziwe vizuri na ziwe zinatambulika ndani na nje, kwa sababu hapa ndipo tunapohukumiwa, tunahukumiwa kwa mazuri na mabaya kwa kutumia Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba niishukuru Wizara ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Waziri Mahmoud, kwa sababu imeongeza thamani na imetuongezea thamani kama Taifa kwa sababu sasa inafanya kazi zake ipasavyo, tunakushukuru sana. Vilevile ninaiomba Wizara hii iendelee na kazi zake hasa kwenye kudumisha suala la diplomasia ya uchumi, kwa sababu diplomasia ya sasa ni uchumi bila ya uchumi maana yake tuko mbali. 
Mheshimiwa Spika, vilevile kuendeleza sera ya kutunza marafiki zetu, kwa sababu kudumisha marafiki ni kazi kubwa ni gharama, marafiki hawa hata kama wanachangamoto ni vema tuendele kufanya nao kazi kwa sababu bila ya marafiki maana yake tatizo linakuwa kwetu ni lazima tudumishe marafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyohiyo ningeomba sasa kuwapa changamoto hasa Mabalozi wetu, kwa sababu Mabalozi wetu ndiyo vioo vyetu huko duniani, ningewaomba kwanza wao wenyewe wawe vinara kwenye kuchangamkia diplomasia ya uchumi na wao ndiyo waweze kusimamia. Kwa sababu bila ya wao maana yake ufahamu wa nje na ndani juu ya sera hii itakuwa ni ngumu sana. Kwa hiyo, wachangamkie kwa sababu Mheshimiwa Waziri, inawezekana unajua au hujui, lakini tunahisi wapo Mabalozi wenzetu wengine kama vile wamekata tamaa kama vile hatuwaoni, kama hawahusiki na mambo ya Kitanzania, kama wanafanya mambo yao tu wenyewe. 
Mheshimiwa Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, awahimize Mabalozi wetu hawa kwamba wafanye kazi yao ya Kibalozi na wafanye kazi tulizowatuma kama Mabalozi, naomba sana. (Makofi)   
Mheshimiwa Spika, suala lingine kwenye hilo hilo ningewaomba wafanyabiashara wetu wa nje na ndani watumie opportunity hizi, kwa sababu pamoja na kwamba Wizara inafundisha, pamoja na kwamba na Mabalozi wengine wanafundisha lakini bado nafasi hizi hatujazichangamkia. Kwa hiyo, ningewaomba sana wafanye kazi wafanyabiashara ya kuchangamkia nafasi hii kwa sababu zipo kwa sababu jumuiya zetu zimetoa nafasi nyingi, lakini bado hatujazichangamkia, ninawaomba sana. (Makofi) 
Mheshimiwa Spika, kuliko hayo Mheshimiwa Waziri ningeomba sana, sasa tunapoelekea diplomasia yetu inakwenda kuimarishwa kwenye mambo ya uchumi, tufanye kazi ya kuhakikisha kwamba ndani tunafundisha zaidi wananchi wanaelewa zaidi na hata wenzetu wa nje wanaelewa zaidi kwenye hili, ningeomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kuliko yote, ninaomba nichukue nafasi hii kupongeza, nimesoma kwa haraka haraka, nimesoma rafiki yetu, Kaka yetu Mheshimiwa Ruto, akituomba radhi wananchi, lakini ninaomba sana na sisi tunapokea. Tunapokea kwa sababu hakuna binadamu aliyemkamilifu, sasa inawezekana na sisi tunalo tatizo lakini ndiyo binadamu, tusameheane ili maisha yasonge, kwa sababu binadamu lazima tukoseane. Kwa hiyo, ningeomba sana kwamba pale ambapo na sisi kama Taifa kama Bunge tumejikwaa ndiyo maisha, lakini ukweli ni kwamba tunahitajiana kama Mataifa rafiki, tunahitajiana kama Tanzania na Kenya, lakini tunahitajiana kama Mataifa yaliyo pamoja na hatuwezi tukafanya kazi bila ya kuwa na changamoto, hizi ni sehemu ya changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa kuliko yote, tulipofika tuchore mstari ili Taifa lisonge kwa sababu hatuna nafasi ya kurudi tunahitaji kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima, ninaipongeza sana Kamati yetu, ninaipongeza Wizara kwa sababu kazi ni kubwa na Wizara imefanya kazi nyingi, lakini ninaipongeza sana Serikali kwa sababu kwenye bajeti za maendeleo tumefika zaidi ya 80% na maeneo mengine tumefika zaidi ya 100% na bahati nzuri kuna wakandarasi wengine tunawadai kazi, hela Serikali imetoa. (Makofi)
 Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Serikali kwa kuelewa, ninaishukuru Serikali kwa kusikia na imesikia kilio cha Kamati na kwa kweli imetekeleza kuliko matumaini yetu tuliyotegemea. Kwa hiyo, ninaomba sana hili liendelee kwa sababu bila ya hivyo maana yake ni kwamba maendeleo tutakuwa tunayarudisha nyuma. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri asimamie hili na kwa sababu sisi kama sehemu ya Kamati na yeye kama Mjumbe wa Kamati ninamwomba sana asimamie ili Tanzania iendelee kusimamia na kuongoza kwenye Jumuiya hizi, lakini na Jumuiya ya Kimataifa. (Makofi) 
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)