Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Alfred James Kimea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye bajeti hii. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuniwezesha kusimama leo tena kuleta mchango wangu kwenye Wizara hii. Pili, ninakushukuru wewe, ninawashukuru Wabunge wenzangu pia ninaishukuru Wizara hii, kwa kipindi cha miaka mitano hii tunamaliza sasa, Bunge na nchi ilinipa heshima ya kuwa Mbunge anayeiwakilisha nchi yetu kwenye Mabunge ya SADC na kwa kuwa Wizara hii ndiyo inayotusimamia, kwa hiyo napenda kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza namna walivyoishi na sisi na kutupa miongozo kwa miaka mitano iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba niende moja kwa moja sasa kwenye mchango wangu, lakini ya kwanza nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika miaka mitano ya uongozi wake. Miaka mitano ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana hasa kurudisha na kudumisha mahusiano ya nchi yetu na Jumuiya ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo kubwa sana na tumeona matokeo yake kwa diplomasia hii Mama Samia aliyoiweka katika nchi yetu na nchi za kimataifa. Utakubaliana na mimi wewe ni mmojawapo wa manufaa hayo, umechaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Mataifa, tunaamini ni juhudi ambazo Dkt. Samia, amezifanya, juzi tulikuwa na Profesa Janabi, lakini na Kaka yangu Deo, ambaye amekuwa SG kwenye Bunge la Maziwa Makuu. Kwa hiyo hizo ni juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuweka mahusiano ya Tanzania na nchi za Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na matokeo hayo, matokeo ya kiuchumi ya moja kwa moja ya nchi yetu yameonekana. Tumeona watalii walivyoongezeka kwa kipindi hiki kifupi, siyo kuongezeka kwa watalii hata uchumi umeongezeka kupitia watalii wanavyokuja kwenye nchi yetu. Pia katika kipindi hiki tumeona tukipata mikopo ya bei nafuu kutokana na mahusiano Mama Samia aliyoyaweka na nchi za kimataifa ambazo zimeweza ku-finance shughuli za kimaendeleo. Nikitoa mfano wa Mradi wetu wa Miji 28, tumepata mkopo wa bei rahisi sana kutoka India, lakini haya ni mahusiano ambayo Mama Samia ameyaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi tu Jeshi letu la Zima Moto, linaenda kupatiwa vifaa vya firefighting kwa bei rahisi sana kutoka nchi za Falme za Kiarabu, lakini haya ni mahusiano ambayo Mama Samia, ameyaweka. Pia ameweza kuvutia Foreign Direct Investment ambayo watu wamekuja ku-invest kwenye nchi yetu, wameweka ajira na vitu vingi vimefanyika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo tumeona mikataba mingi ya ushirikiano kati ya nchi zetu na nchi za kimataifa, lakini pamoja na institution mbalimbali imeingiwa kati ya nchi yetu na jumuiya hizo. Kwa hiyo nimpongeze Mama Samia na Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nina ushauri mdogo katika Wizara hii, nina sehemu tano za kuishauri Wizara hii. Kwanza ni kweli tumeona nchi imefunguka, ni kweli tumeona diplomasia imejengwa, lakini wananchi wengi wa Kitanzania hawana elimu ya fursa hizi zinazopatikana.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwetu Korogwe kwa mfano au Muheza jirani zetu pale kwa mfano, wanalima sana machungwa, wanavuna machungwa, lakini hawafahamu kwamba kuna soko la kimataifa kama AGOA na mambo mengine kama hayo ambayo wanaweza kupeleka bidhaa zao kule. Hii inasababisha nchi jirani zichukue hizo opportunities, zinakuja kuchukua bidhaa zetu zinaenda ku-park na kuuza nje kwa sababu tu wananchi wetu wa Tanzania hawafahamu hizo opportunities ambazo zipo.
Mheshimiwa Spika, siyo hapo tu, katika ajira nje ya nchi wengi hawafahamu. Tunamshukuru Waziri wetu juzi ali-communicate na Watanzania, tuliona wamepata ajira kule Dubai, ninajua opportunities hizi zipo, Wizara waongeze jitihada wananchi wa Tanzania wafahamu opportunities ambazo zipo nje ya nchi. Maana tunasafiri tunaona mataifa ya jirani wanavyochukua hizo opportunities, lakini ukiwaangalia Watanzania ni wachache sana, kwa ajili tu hawana elimu ya kutosha juu ya opportunities hizo ambazo zipo nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili, kweli Rais amefungua nchi yetu, tumeingia mikataba mingi, lakini sijui kama tuna-keep progress na kuwa-update Watanzania status ya mikataba hiyo ambayo nchi inaingia. Inawezekana Rais, anatumia juhudi kubwa sana kuingia kwenye mikataba ya Kilimo, Umwagiliaji, sijui nini na nini, lakini tunafuatilia mikataba ile inafika mwisho? Kwa hiyo ninaomba Wizara hii ihakikishe mikataba ambayo nchi yetu inaingia na mataifa au taasisi za kimataifa, basi ifikie mwisho na Watanzania wawe wanapewa updates ya nini kinachoendelea. Tunafurahi kuona mikataba, lakini tunatamani kufurahi zaidi kuona inafikia mwisho ili tuweze kupata faida ya mikataba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa tatu, natamani Wizara yetu hii itengeneze incubation centre kwa ajili ya vijana wa Kitanzania. Ninamaanisha nini? Ninatamani Wizara hii itafute talented graduates kutoka vyuo vikuu mbalimbali, baada ya kuwapata vijana hawa ambao wanaufahamu mzuri, ni wazuri kichwani wawakusanye na kuwafundisha namna ya ku-grab opportunities ambazo zipo nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, vijana wafundishwe business nje ya nchi, waambiwe kuna ajira nje ya nchi, baada ya hapo tunaweza hata tukawa-finance ili waweze kwenda nje ya nchi kuweza kupata fursa hiyo, hii itasaidia kuwa na watu wengi nje ya nchi ambao watakuwa wanaleta remittance nchini kwetu. Nchi yetu ukilinganisha na nchi jirani remittance ni ndogo sana, foreign currency tunayoipata kutoka kwa vijana wetu wa Tanzania ambao wapo nje ya nchi ni ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natamani tutengeneze centre ambayo itakusanya vijana kutoka vyuo vikuu, wenye uelewa mzuri, wasomi hata kama ni 1,000 wawekwe chini wafundishwe nchi hii ina opportunities za kibiashara hii na hii, nchi hii ina ajira hii na hii, halafu tunawasaidia waweze kutoka. Tusing’ang’aniane na ajira ambazo zipo ndani ya nchi wakati tunaweza kutengeneza ajira nyingi nje ya nchi na watu wataenda kupata exposure kule, watu wataleta utaalam kutoka nje ya nchi. Wizara hii inaweza kuamua jambo hilo na likafanyika, likawa msaada kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne na la mwisho ambalo ninapenda kuchangia, siyo kila mtu kwenye hii International Community anakuja nchini kwetu, taswira ya Tanzania au taswira ya nchi yoyote ni Balozi zetu ambazo zipo kwenye nchi hizo. Nini ninataka kushauri? Ninatamani tuwe tuna Balozi nzuri ambazo zita-reflect taswira ya nchi yetu. Baadhi ya Balozi zetu, tunampongeza Rais, lakini tunaipongeza Wizara kwa kukarabati na kujenga Balozi kwenye nchi mbalimbali. Hata hivyo, bado tunazo Balozi ambazo zinawakilisha nchi yetu, ambazo haziendani na ukubwa wa Taifa letu la Tanzania. Mfano, Ubalozi wetu pale Nchi za Zimbabwe au Zambia pale au Msumbiji. Msumbiji kwanza hatuna kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninatamani tu-invest, tutafute wadau, tuhakikishe tunajenga Balozi nzuri ambayo kila mtu akiiona atasema yes nimeiona Tanzania hata kabla hajafika Tanzania. Hasa akifika akaona ofisi ya Balozi au tunakodi, hii haileti taswira nzuri, haileti ukubwa wa nchi hii ambayo inaongozwa na Jemedali Dkt. Samia Suluhu, haileti picha nzuri.

Mheshimiwa Spika, ninajua uchumi wetu siyo mkubwa kiasi hicho, ninajua watafanya juhudi kubwa kuhakikisha tunakuwa na Balozi nzuri ambazo zita-reflect kweli taswira ya nchi kubwa ya Tanzania, ambayo inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama ambaye amejipambanua, Mama jembe na Mama hodari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia, lakini kwa kuwa muda upo pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Korogwe Mjini, kwa kuendelea kuniamini, kunipa nafasi hii ya miaka mitano, bado tunawapambania na bado tunahakikisha tunafanya mazuri kwa ajili ya Korogwe na nchi nzima ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninakushukuru sana, Mungu akubariki. (Makofi)