Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ambayo ipo mbele yetu leo hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali cha uhai, pia nainmshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kila iitwapo leo. Kupitia Wizara hii nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje pamoja na timu yake yote, wasaidizi wake, lakini pia niwashukuru wanakamati wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nimemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mambo mengine anayoyafanya ndani ya nchi, wenzangu wametangulia kusema kwamba amefungua milango ya mahusiano katika nchi mbalimbali duniani na matokeo yake tunayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alifanya royal tour ambayo imeliletea Taifa hili fedha nyingi za kigeni na bado wageni na watalii wanakuja katika maeneo yetu mbalimbali hali ambayo hata sisi ambao tupo huku chini tunaona manufaa. Mwananchi mmoja mmoja ananufaika na ziara ile ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ufunguzi huo wa mipaka ndani na nje ya nchi tumeona mwezi Januari mwaka huu kuliendeshwa summit (Energy Summit) kubwa sana ya kimataifa pale Dar es Salaam. Kwa kweli ina mchango mkubwa sana kwa uchumi wa Taifa hili na wananchi wamejipatia kipato kikubwa. Kwa hiyo, ninaona ile dhamira yake ya dhati ya diplomasia ya uchumi namna ambvyo yeye mwenyewe anaisimamia. Siyo rahisi sana kama h

una utashi wa ndani kutekeleza yale mambo. Kwa hiyo, tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake ambazo anaendelea kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata ukienda kwa wakulima ukiachana na hii ya Energy Summit na mikutano mbalimbali ambayo inafanyika ndani na nje ya nchi tumeona matokeo yake. Wakulima wa mbaazi na ufuta ni wanufaika wa safari ambazo Taifa hili kupitia viongozi wake wanazifanya nje ya nchi. Niendelee kuomba Wizara iendelee kusimamia pale ambapo Mheshimiwa Rais anaachia, Wizara tuendelee kutafuta masoko kwa ajili ya wakulima wetu ili ile diplomasia ya uchumi ambayo imeanza kutekelezwa iendelee kushika kasi na wananchi waone manufaa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ameeleza namna ambavyo watashirikisha mpaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kule chini kuhusiana na suala hili la diplomasia ya uchumi. Ni wazo zuri na ninaomba tukalisimamie. Kwa nini, tukalisimamie? Kwa sababu kule chini ndiko ambako kuna wakulima wengi. AMCOS zipo kule, tuwashirikishe elimu ifike kwa watu wote ili wananchi wanufaike na fursa ambazo zipo kitaifa pamoja na kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ambaye amemaliza kuongea hapa amezungumzia suala la machungwa mengi ambayo yanalimwa Tanga, lakini yanakaa muda mrefu hayapati soko kwa sababu tu tunakosa fursa namna ya kuziendea ili watu waweze kuuza yale mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda mikoa ambayo inalima korosho sasa hivi wanawake wameamka sana. Wanabangua kweli korosho zao lakini wanakosa namna ambavyo wanaweza kufikisha kwenye masoko ya kimataifa ili na wenyewe waweze kunufaika na uwepo wa diplomasia hii ya uchumi katika nchi yao na mataifa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na yote Mheshimiwa Waziri ninaomba walichukue kwamba tumefikisha na tutafikisha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini tukasimamie tuone utekelezaji wake kule chini ukoje ili wananchi wa kawaida nao wawe wanufaika wakubwa wa suala hili la diplomasia ya uchumi ambalo tunaliendea sasa hivi na Mheshimiwa Rais wetu ni mlezi mzuri katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kituo chetu cha Mikutano cha AICC pale Arusha. Kinafanya kazi nzuri sana, mikutano inaendelea na maboresho ya kituo kile yanaendelea lakini pale zipo changamoto. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri amesema hapa kwenye hotuba yake amezungumza kwamba sasa hivi pamoja na kituo kile ambacho kipo, lakini pia wameingia mikataba mwezi Machi, mwaka huu na wenzetu wa NSSF kwa ajili ya kujenga kituo kipya cha kisasa kabisa ambacho kitavutia mikutano mikubwa mikubwa mingi zaidi ya kimataifa. Ninamshukuru na kumpongeza kwa huo ubunifu ambao Wizara wameuona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina ushauri pia, pamoja na kwamba tunaenda kuingia huo ubia na wenzetu wa NSSF, lakini kituo chetu cha mwanzo cha awali kiendelee kuboreshwa. Kufikia mwaka 2027, nchi yetu inaenda kuhodhi mashindano makubwa ya AFCON. Sasa kituo kile ninaomba kikatumike vizuri na wananchi wanufaike na uwepo wake na suala zima la AFCON katika kuliongezea kipato.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kituo hakitakidhi haja zaidi au hakitafanyiwa maboresho yale yanayokidhi haja zaidi tutapoteza hizo fursa ambazo wananchi wetu wanazihitaji sana. Kwa hiyo, niombe maboresho yafanyike pande zote mbili ili kituo cha zamani kiwe cha kisasa na hicho kipya ambacho kinatarajiwa kujengwa kikawe cha kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kituo kile pia kinakabiliwa na changamoto mbalimbali pamoja na masuala ya madeni. Karibu shilingi bilioni tano inayodai ni madeni kutoka katika Sekta Binafsi na taasisi za umma. Niombe ule mkakati ambao tumejiwekea namna ya kukusanya yale madeni tuusimamie ili madeni yote yaweze kurudi na kituo kiendelee vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taasisi zetu za umma pia zinaenda zinafanya hiyo mikutano na wenyewe wanadaiwa. Niombe Wizara kwamba kama kumbi za kawaida tunapoenda kukodi mambo yetu ya harusi na vitu vinginevyo tunatoa fedha kwanza lazima utoe advance ndipo uendelee na shughuli, kwa nini, kituo chetu hiki hatutoi advance ndipo tukafanye mikutano yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwa taasisi zetu za umma ambazo zinaenda kutumia kituo kile basi na zenyewe ziwe zinalipa advance kwanza halafu mikutano iendelee ili kituo chetu kiendelee kusimama kama vile ambavyo tulikuwa tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu tunaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Fedha zimetolewa za kutosha, kazi iliyobakia ni kwa wakandarasi kutekeleza yale ambayo tumekubaliana kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu anaendelea kutekeleza miradi mikubwa ambayo ina tija kwetu sisi kama Wananchi wa Tanzania, lakini pia na wenzetu wa nchi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ninataka niliongee kwa kifupi linahusiana na kituo chetu cha Uhusiano wa Kimataifa wa Dkt. Salim Ahmed Salim, pale Dar es Salaam. Ninashukuru kwamba Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa ule mradi na fedha zinatolewa, lakini kile kituo mpaka kufikia Disemba, 2024 kilikuwa kimetekelezwa chini ya 30%. Ule mradi unasuasua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe wale ambao wamepewa mamlaka ya kutekeleza ule mradi wausimamie ili ule mradi uakisi jina la kituo na matendo au majengo mazuri ambayo yatakuwa pale. Inatia huruma, ni mradi wa muda mrefu, lakini utekelezaji wake kama nilivyoongea unasuasua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa na hayo kwa kifupi na ninashukuru sana kwa nafasi. Niendelee kuipongeza Wizara kwa utendaji mzuri wa kazi, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri wa nchi yetu na namna ambavyo anaendelea kutupatia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo hii miradi ambayo inatekelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)