Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii. Nitazungumza kwa ufupi sana kwa sababu hapa ni pongezi zaidi kuliko ushauri. Ninatumaini mambo yamefanyika vizuri sana nitatoa ushauri kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiona vinaelea ujue vimeundwa na vyote hivi ambavyo vimesomwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hotuba nzuri sana iliyosomwa na Mheshimiwa Waziri ni mafanikio ambayo yamepatikana kwa uongozi wa mpendwa Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanadiplomasia wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawiwa kusema kwamba sisi tunaoishi kwenye mikoa ya mipakani tunawiwa kumshukuru sana kwamba baada ya yeye kuchukua uongozi wa nchi hii, ndiyo tukaona mipaka ile imefunguka na mazao yetu sasa yanauzika kwa bei nzuri kwenye cross border trade na hivyo uchumi wetu kwenye mikoa ile umeimarika kutokana na falsafa hii ya economic diplomacy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, economic diplomacy kwa kifupi ninasema ni investment and export promotion. Niseme kwamba kweli investment imekuwa promoted na tukisoma taarifa za TIC tunaona kwamba miradi iliyosajiliwa inafikia takribani dola bilioni tisa; ni fedha nyingi sana. Mambo haya yote yameimarishwa kwa nguvu na jitihada za pekee za Mheshimiwa Rais mwenyewe akisaidiwa na Wizara hii ya Mambo ya Nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme, ninafikiri kwamba hata katika mkutano huu wa leo mara ya kwanza ninaona mabalozi ni wengi na wamekuja wenyewe. Hii inaonesha kwamba ushirikiano wa Kimataifa kweli umekuwa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hivyo niseme kwamba tumeona wakuu wa nchi mbalimbali wamekuja nchini kwetu kwa wingi. Tumeona mikutano ya kimataifa ikifanyika na sasa tunaona kwamba AFCON inakuja. AFCON inakuja na utalii mkubwa kama tutaweza kujipanga vizuri kwenye eneo hilo ili ku-exploit opportunity kwa watu wengi ambao watakuja kufanya michezo na kuangalia michezo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliku-miss sana lakini ulikuwa umepotea kidogo. Ninazungumza kidogo kuhusu diaspora. Nimefurahi sana kusoma kwenye kitabu hiki ambacho ametupa leo na kwenye ile hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ukurasa wa 74 mpaka 77 wameweka mikakati ya diaspora ambayo ndiyo nilikuwa ninafikiri nitashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo niseme kwamba bado kusema kweli tuna opportunity na tuna fursa kubwa sana kwenye eneo la kuhamasisha diaspora kutuma fedha kwa ndugu zao wanaowategemea lakini pia kuwekeza kwenye nyanja mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, diaspora remittance mwaka huu wa 2024 ilikuwa ni dola za kimarekani 757 kwa wastani (ninafikiri ni wastani huu). Dola 757 ambapo ni kama asilimia 0.9 ya Pato la Taifa; hicho ni kiduchu sana. Hebu tuangalie wenzetu kwa mfano, uzuri kwa sababu nimenukuu kutoka kwenye chanzo ambacho kinaaminika wenzetu kwa mfano, ninataja Kenya, Mheshimiwa Balozi anisamehe. Kenya, remittance ni dola bilioni 4.8 uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 4.1 ya pato la Taifa. Uganda ni dola bilioni 1.5 ni asilimia 2.6 ya pato la Taifa. Rwanda ni dola milioni 537; ni asilimia 3.9 ya pato la Taifa. Burundi ni ndogo lakini uwiano wa pato la Taifa kwao ni asilimia 1.6 ya pato la Taifa ambalo ni dola kama milioni 49. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi bado tupo nyuma sana. Mikakati hii ambayo tumeiona sasa ambayo wameiweka ni mikakati ambayo tulikuwa tunaiwaza sana sisi pale CRDB tulipokuwa tunaanzisha Tanzanite Account tukapigana nayo, lakini haikutokea, sasa ninaona inatokea. Moja ya mkakati ni ule wa kuwatambua diaspora na kuwawezesha kumiliki ardhi na kumiliki mali katika nchi hii bila kupoteza uraia wao ule ambao ni wa kigeni. Sasa hilo la kuwatambua rasmi imechukua muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, sasa hivi kutokana na andiko hili nililoliona hapa ni kwamba tayari Serikali imeshawasilisha marekebisho kwenye sheria mbalimbali hususan Sheria ya Ardhi na kadhalika itakayoweza kuruhusu wana-diaspora wa Tanzania wanaoishi nje kupewa vitambulisho maalum au hadhi maalum ya kuweza kumiliki ardhi hapa pamoja na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa ahsante hiyo ninaamini kilichobaki sasa ni lazima sisi wenyewe na benki (ninaamini benki nyingi tulisikia zimetajwa hapo benki takribani zote) sasa zimeanza kuchangamkia fursa za uwekezaji ku-harness akiba (savings) za Watanzania wanaoishi nje. Kwa hiyo, wameboresha amana zao kwa namna hiyo. Pia, hata uwekezaji kwenye nyumba zaidi kwamba wanatuma fedha kwa wingi kwa kusaidia ndugu zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nimefurahishwa nacho sana ni kile wanachosema wanaanzisha Diaspora Digital Hub (kanzidata) mfumo ambao utawezesha diaspora akiwa nje kule ana-access, pengine atakuwa ana-access kupitia internet, anaweza aka-access akajua kuna fursa gani za uwekezaji nchini hapa. Je na taratibu zikoje kwenye eneo lile ambalo anataka kwenda kuweza na atatumaje fedha?

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo kanzidata au mfumo huo utawezesha taasisi za kifedha kuunganisha na kuhamasisha wale vijana wetu na wale walio nje kuwekeza na kutuma fedha kwenye account ambazo pengine wanafunguliwa. Ninatumaini wameanzisha account specific.

Mheshimiwa Spika, hili la kuhamasisha na Serikali kujihusisha hususan Mheshimiwa Rais na uongozi mzima wa Serikali kujihusisha kuwatafutia Watanzania kazi nje hasa wale wenye ujuzi mzuri. Unaweza kukuta Watanzania wanaenda kufagia tu, lakini tumeona sasa watu wenye utaalam mzuri kama Profesa Janabi, Serikali imepambana na Mheshimiwa Rais mwenyewe amepambana na Mheshimiwa Spika umepambana na kila mtu amepambana na tumeona amechukua kazi. Ninaamini kwamba hiyo kazi aliyochukua ni kazi kubwa na ni kazi ambayo pia inainua hadhi ya Taifa letu na umaarufu wa Taifa la Tanzania kama eneo lenye uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na uwekezaji tulioufanya kwa mfano kwenye hospitali zetu sasa hivi tunapata tourism ya medical (medical tourism). Watu wanakuja Muhimbili wanatibiwa ni kitu ambacho kinainua hadhi na kweli kuthibitisha kwamba Tanzania bado tupo na tutaendelea kuwa imara kutokana na uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninataka nichukue fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wawili pamoja na uongozi wa Wizara hii ambao una Wanadiplomasia makini wanaotekeleza na wanaoelewa mambo ya kila aina hasa yale ya kifedha. Ninashukuruni sana.

Mheshimiwa Spika, ninasema hivyo kwa sababu wameweza kutumia mfumo mbadala wa kujenga Ofisi za Mabalozi kwa mfano hizo walizotaja ambapo wametumia ubia na mashirika yetu ya pensheni. Ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)