Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango kwenye hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanadiplomasia namba moja kwa jitihada zake kubwa sana za kuifungua nchi yetu na kuifanya sasa tuweke nguvu kubwa katika kuiunganisha na mataifa mengine. Tunao ushuhuda kwamba mahusiano yetu na mataifa mengine yameongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wawili; wanafanya kazi kubwa sana bila kuwasahau Katibu Mkuu na Manaibu wake. Sisi kama Kamati tunafarijika sana na utendaji wa Wizara hii. Kwa muda mfupi kumekuwa na mabadiliko makubwa sana chanya kwenye Wizara hii. Mheshimiwa Waziri na timu yako yote, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tarehe 19 mwezi huu Mheshimiwa Rais alizindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2021 na mkakati wake wa utekelezaji. Vipaumbele kwenye bajeti yetu ni kuhusu kuratibu utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. 
Mheshimiwa Spika, Sera hii aliyoizindua Mheshimiwa Rais katika mambo makubwa inayoongelea ni kuimarisha diplomasia ya uchumi ili tuweze kuitumia kutangaza fursa tulizo nazo, kuvutia wawekezaji, kujumuisha diaspora kwenye maendeleo ya uchumi wetu na kukuza Kiswahili kama lugha muhimu ili tuibidhaishe Kimataifa. 
Mheshimiwa Spika, ninataka kushauri; kwenye eneo la diplomasia ya uchumi tunaenda vizuri kwa sababu, kitakwimu kuanzia Mwaka 2020 mpaka leo 2025 kumekuwa na mabadiliko makubwa sana. Kupitia mabadiliko hayo kwenye diplomasia ya uchumi hata uwekezaji kwenye Taifa letu, tumekuwa na maendeleo na matokeo yake kumekuwa na nyongeza ya uwekezaji kiuchumi kwa karibu 21% ni jambo zuri, lakini kupitia sera hii tunaweza tukafanya vizuri zaidi na kama ambavyo kwenye mpango kazi wa Wizara walivyouweka, kwa ajili ya mwaka kesho 2026, ninapenda kushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bado kuna uelewa mdogo sana wa diplomasia ya uchumi na kwa sababu hiyo, jamii, taasisi na Wizara nyingine wanaona kama vile diplomasia ya uchumi ni suala la Wizara ya Mambo ya Nje pekee, kitu ambacho siyo sahihi. Kwa sababu hiyo ningependa kuishauri Wizara ya Mambo ya Nje, kupitia wataalam wake wa diplomasia ya uchumi, kuwekeza sana kwenye mafunzo na elimu, ili taasisi, idara na Wizara zote zione kwamba, diplomasia ya uchumi ni yetu sote, kama Watanzania. Katika mipango yao, diplomasia ya uchumi iwe ni item mojawapo katika utekelezaji wa shughuli zao, ili kuhakikisha kwamba, hii dhamira ya Taifa letu, dhamira ya Mheshimiwa Rais, kuitumia diplomasia ya uchumi kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwenye Taifa letu inaweza kufikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu, Mheshimiwa Rais wetu amefanya kazi kubwa sana kuiunganisha Tanzania na mataifa mengine na kwa kutumia diplomasia ya uchumi kumekuwa na mabadiliko makubwa sana. Kama sote tukiwa na uelewa wa pamoja wa namna ya kuingia na kuitumia diplomasia ya uchumi, Taifa letu litanufaika kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu ya advantages nyingi tulizonazo, kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kushauri vilevile kwa sababu, tunazo fursa nyingi na kwa kutumia diplomasia hii ya uchumi, ninaomba mabalozi wetu wote wapewe performance indicators, ili tuweze kuwapima nini kimepatikana kutoka Ubalozi A tukilinganisha na Ubalozi B kwa sababu, kila Taifa lina fursa tofauti. Tukiweza kutoa performance indicators kwa mabalozi wetu itatupa fursa ya kupima ubalozi fulani umetendaje kulingana na fursa zilizopo, Watanzania kiasi gani wamenufaika na ubalozi kwenye Taifa hilo, jambo ambalo litatusaidia kufanya review, ili kuangalia sasa ni wapi hatujaenda vizuri na kwa sababu gani tufanye marekebisho, ili mwisho wa siku tuweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo linguine, mchangiaji mmoja hapa ameelezea namna ambavyo balozi zetu nyingi haziakisi taswira ya Taifa letu, zimechoka, hazina mazingira mazuri. Ninatambua Wizara inao mpango mkakati wa ubia kati ya Serikali na taasisi binafsi, ili kujenga ukarabati na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye mataifa mengine, hasa kwenye balozi zetu. 
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Wizara, waharakishe basi changamoto zilizopo kwenye kukamilisha mpango mkakati wetu huu wa ubia kati ya Serikali na taasisi binafsi, ili moja, tuweze ku-save pesa za Serikali na tuweze kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambayo inasuasua kwa sababu ya upungufu wa rasilimali pesa, ambayo Serikali tupo nayo. Tukiweza kukamilisha haraka huu mpango mkakati wa ubia kati ya Serikali na taasisi binafsi kusaidia Wizara ya Mambo ya Nje kukamilisha miradi yake iliyopo nje ya nchi, tunaweza tukaharakisha zaidi kufanya maboresho, kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali, ikiwemo balozi, ofisi na vitega uchumi tulivyonavyo kwenye mataifa ya nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine nililotaka kuchangia ni namna ambavyo tunaweza tukatumia michuano ya AFCON, ambayo itafanyika nchini kwetu, kuweza kutusaidia kiuchumi. Ninashauri, tutumie balozi zetu ku-promote michezo hii na ku-promote vivutio mbalimbali tulivyonavyo kwenye Taifa letu, ili mtu atakapoenda kwenye ubalozi wetu akute matangazo pale kwamba, pamoja na michezo, ukija Tanzania kuna jambo fulani, kuna fursa hii, kuna eneo fulani la utalii, ili asiweze kutambua tu kwamba kuna habari ya michezo, lakini vilevile fursa nyingine zilizopo kwenye Taifa letu, kupitia balozi zetu, wananchi wa mataifa mengine waweze kuziona.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu, balozi ni sector for investment, kwa hiyo, mtu akienda pale akakuta maelekezo, akakuta matangazo, inakuwa rahisi kwake sasa kutafuta amali za ziada. Kwa maana hiyo, kama Taifa, tukanufaika kupitia promotion inayoweza kufanyika kwenye balozi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo machache ninaipongeza tena Wizara yetu, wanafanya kazi kubwa sana. Sisi, kama Kamati, tunafarijika sana na utendaji wenu. Ninaamini, sisi kama Wabunge, tutaendelea kuiomba Serikali pale kwenye mapungufu, hasa ya kirasilimali, iweze kuendelea kusaidia, ili dhamira ya Serikali yetu kuitumia Wizara hiyo, kuitangaza nchi na kuisaidia Tanzania, kama Taifa, kufaidika na majirani zetu, mataifa mengine, tuweze kuitumia.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana kwa nafasi. Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)