Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Nje na Africa Mashariki. Kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye ametuwezesha leo hii tupo mahali hapa. 
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanadiplomasia namba moja, ambaye amefanya mambo makubwa. Hatumpongezi hivihivi, kuna mambo makubwa sana ambayo ameyafanya, ameweza kupata tuzo mbalimbali za nje na ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu anafanya kazi kubwa sana, anatuheshimisha Watanzania. Licha ya hivyo, Mheshimiwa Rais alileta 4R ambazo ni urithi wa kidiplomasia wa nchi yetu. Hii 4R inaweza ikatumika ndani na inaweza ikatumika nje ya nchi, kwa ajili ya kuleta diplomasia kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ninapenda pia, kukupongeza wewe mwenyewe, hongera sana, umetuheshimisha kwa kuwa Rais wa IPU na kwa kweli unatuwakilisha vyema. Wewe ni mfano wa Waheshimiwa wengi hapa ndani na nje ya nchi, hongera sana kwa kazi kubwa unayoifanya, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila kwa kutowapongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Manaibu Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara imepata Mawaziri. Waziri huyu ameweza kuleta mabadiliko makubwa sana katika Wizara hii, ameweza kufanya makubwa, ambayo yanaleta matunda makubwa katika nchi yetu. Tunaona leo tupo na mabalozi pale, lakini tupo na watu mbalimbali, ni kazi ambayo amefanya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii. Hongera sana, wanafanya kazi kubwa, hongera kwa majukumu hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni yenye upendo, ni nchi ambayo kwa kweli, imefanya nchi nyingi za Africa kupata uhuru; yenyewe ilikuwa inataka, hata isipate uhuru mapema, ili nchi nyingine ziweze kupata uhuru. Hii tuliiona toka mwanzo, sisi ambao ni wa siku nyingi. Nchi yetu imefanya kazi kubwa sana ya kuweza kusaidia nchi za Afrika ziweze kupata uhuru; ni kwa ajili ya upendo wa nchi yetu hii. Kwa hiyo, nchi yetu ni ambayo ina upendo mkubwa. Hata ukiona mambo mengine yanaendelea, lakini nchi yetu ni tulivu na yenye amani. Tunazidi kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuzingatia hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Wizara kwa kuleta Sera ya Mambo ya Nje, ambayo imezinduliwa tayari. Kwa hiyo, ninawaomba Wizara sasa waende wakaitekeleze inavyotakiwa, wakaifanyie kazi kama makusudio ya sera yanavyotaka. Mikakati yake iende ikafanyiwe kazi, ninaomba wazidi kuifanyia kazi, sera hii, kwa sababu mambo yaliyomo mle yana umuhimu kwa jamii yetu.
Mheshimiwa Spika, sasa ninajielekeza katika hoja zetu. Kuna balozi zaidi ya 105 ambazo bado hali si nzuri na Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa, ninampongeza kwa sababu, ameweza kutafuta hata baadhi ya taasisi ambazo zitaenda kusaidia kujenga, hongera sana, hicho ndiyo kitu tulichokuwa tunapenda kukiona, ni jambo jema. Ninaiomba Serikali, Wizara ya Fedha, iweze kutoa fedha hizo kwa balozi nyingine ambazo bado hazijafikiwa, ili ziweze kujengwa vizuri na kuleta sura nzuri, ambayo mama yetu Samia anaileta kwa nchi yetu. Kwa hiyo, wakienda wafadhili, wanavyokuja katika nchi yetu au wakiwa kule kwenye nchi zao wakaona zile balozi zilivyo wanaona kama nchi yetu ipo tofauti, kwa hiyo tunaweza tukakosa manufaa mbalimbali. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara iweze kufuatilia hilo na Wizara ya Fedha iweze kutoa fedha, kwa ajili ya ujenzi. 
Mheshimiwa Spika, tupongeze, wameweza kujenga Kituo cha Haki za Binadamu na Watu ambacho Mjini Arusha. Ni kituo kikubwa ambacho kitakwenda kufanya kazi kubwa ya Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu. Mahakama hii itaweza kusaidia sana katika utoaji wa haki katika nchi yetu kwa region nzima ya Afrika. Kwa hiyo, ninaomba, Mheshimiwa Waziri, wapambane kituo hiki kiweze kukamilika kwa wakati, kipo vizuri na kinaenda vizuri. 
Mheshimiwa Spika, ninakwenda sasa katika kipengele cha diplomasia ya uchumi. Mheshimiwa Rais alizindua program ya matumizi ya nishati safi ya kupikia Afrika. Hii program ya nishati safi ya kupikia Africa aliizindua alipokuwa kwenye mkutano wa nchi wanachama uliofanyika huko Dubai.
Mheshimiwa Spika, ninawapongeza kwa sababu, sasa hivi wanaona jinsi nishati safi ya kupikia imekwenda katika taasisi mbalimbali Tanzania, kwenye shule ukienda, kwa wananchi na jamii, nia yao kubwa ni kwamba, ifikapo Mwaka 2034 watakwenda kufikia wananchi 80% kwenda kupata hiyo nishati safi ya kupikia. Kwa hiyo, ninawaomba, Serikali, waweze kuongeza juhudi, ili kufikisha nia hiyo kwa hakika.
Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni diplomasia ya kiuchumi. Diplomasia hii, ninaishauri, Wizara iende sambamba na kutoa elimu kwa jamii. Ninashukuru umesema kwamba, watafika mpaka ngazi za chini, lakini hapa tulipo wananchi waliopo Kalenga na waliopo maeneo mbalimbali kule chini, wanaolima, ambao wanaotumia kilimo kama njia ya kupata uchumi wao, hawajui wanafikishaje ama wanaendaje kufanya biashara sehemu mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninawaomba waliweke wazi, kwamba, kama ni mkulima, anatoaje mazao yake kutoka hapa yakafika nchi nyingine? Anapataje vibali? Iwekwe wazi kabisa watu wawe wanatambua kwa sababu, bila kutoa hii elimu wananchi wanashindwa kujua wafanyaje? Wanakuja wanatuuliza hata sisi Wabunge kwamba, hivi nitafanyaje kwenda kuuza mazao yangu? Wamelima mazao ya kutosha, lakini hawajui utaratibu ukoje? 
Mheshimiwa Spika, kuna masuala ya kodi nyingi ambazo zinawa-discourage, ambazo zinawafanya washindwe kwenda kuuza huko. Ninawaomba Wizara hii washirikiane na Wizara nyingine wahakikishe kwamba, wanaweka mazingira mazuri ya wananchi wetu wanaolima waweze kufanya biashara, hata katika nchi nyinginezo, waweze kufanya kazi vizuri. Wizara ya Kilimo angalau walipeleka wakulima wa parachichi…
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Grace Tendega, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.
TAARIFA
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nitumie nafasi yangu, mchango huu anaouzungumza Mheshimiwa Mbunge, kwa Taifa, kama la Burundi na Congo, tunaona kwamba, Serikali kwa ushirika na CRDB Bank ni mabalozi kule. Wamekuwa wakitumia fursa hii pia, kuwaelimisha Wakongo na Warundi shughuli za kiuchumi, ambazo zinapatikana ndani ya Taifa letu, ikiwemo biashara kati ya nchi hizi mbili tofauti. 
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaunga mkono hoja kwamba, ni muhimu sana wakaweka msisitizo kwenye balozi nyingine kuhakikisha kwamba, tutawasaidia kwenye taswira ya kiuchumi kidiplomasia.
SPIKA:  Mheshimiwa Grace Tendega, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru, ninaipokea Taarifa hiyo. Kwa hiyo basi, Tanzania nayo iweze kuiga mfano huo kusaidia wananchi waweze kupata hiyo elimu na kufanya biashara zao, wakauze nje bila vikwazo vyovyote.
Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Wizara ya Kilimo, ambayo walichukua wakulima wetu wa parachichi wakawapeleka Nchini Ujerumani ambako walikwenda kule wakajifunza. Wanapata exposure ya kujua kwamba, ni kitu gani na mambo gani yafanyike; basi Wizara hii ikishirikiana na Wizara nyingine waone namna ambavyo wataweza kuwachukua wawekezaji wetu, baadhi, waende nje ya nchi wakajifunze, wakirudi wanaweza wakawekeza nje ya nchi au hata ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaona kwamba, kuna wawekezaji wachache sana walioko nje ya nchi, ndani ya nchi wapo. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri aangalie namna ambavyo wataona inafaa wawekezaji waweze kuziona fursa nje na waweze kuwekeza. Watanzania wanaweza kwenda kupata fursa kule, lakini waweze pia kuwekeza zaidi na kuleta wawekezaji wengi ndani ya nchi kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la diaspora. Ninawapongeza, wameweza kusimamia kupata ile data na kujua, lakini ninawaomba hizi data ziwe zinakuwa updated daily, ili kujua kila mara tuna diaspora wangapi waliopo masomoni? Wangapi kazini? Wangapi ni wafanyabiashara? Pia, kuangalia masuala mbalimbali, ambayo wanaweza waka-capture their economic indexes kuona kwamba, uchumi wao upoje na utanufaisha vipi katika nchi yetu? Tuweze kufaidika na kunufaika nao. Hilo ni jambo ambalo ninaomba kuliweka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la sekta binafsi kushindwa ipasavyo kuona fursa. Wizara hii ndiyo kioo cha sekta binafsi kuona fursa mbalimbali. Kwa hiyo, ninawaomba waende wakawafikie, sekta binafsi, waweze kuziona fursa hizi na kuzichukua; fursa za kiuchumi, kibiashara, kielimu na kadhalika ziweze kutimizwa.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)