Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ali Juma Mohamed

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninapenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia tena leo kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki.

Mheshimiwa Spika, ninataka nianze mchango wangu kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia, ni mwanadiplomasia namba moja nchini kwa kufanya kazi kubwa ya kuipaisha nchi yetu katika Diplomasia ya Kimataifa. Bado nchi yetu ya Tanzania, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiweka kuwa, tunaonekana ni kisiwa cha amani nchini.

Mheshimiwa Spika, katika historia ya nchi yetu tuna Marais wengi ambao wamewahi kuwa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa upande wa Rais wetu, ambaye tupo naye sasa, ana miaka minne tu tangu akae katika kiti hiki cha Urais, historia inasema kuwa, yeye ni Rais wa kwanza kuweza kupata tuzo nyingi za kimataifa ambazo zimetoka ndani na nje ya nchi. Kwa hivyo, muda huu mfupi ambao amekaa umahiri na haiba yake imesababisha nchi yetu kuweza kutajika vizuri katika hali ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, ninapenda pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Manaibu Waziri wake, ndugu yangu Mheshimiwa Cosato David Chumi na Mheshimiwa Lazaro Londo, kwa kufanya kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika Nyanja hii ya mahusiano ya kimataifa. Hivi sasa kumekuwa na ushawishi mkubwa kwa nchi yetu katika anga ya kimataifa na tumeshuhudia hivi karibuni kuongezeka kwa idadi ya Watanzania ambao wanaongoza taasisi mbalimbali za kikanda na zile za kimataifa huku duniani.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia pia kazi kubwa ya utendaji kazi katika Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tumeona kuwa hivi sasa speed ya utendaji kazi katika Wizara hii imekuwa kubwa; na tumeshuhudia kuwa Mheshimiwa Waziri ametengeneza vizuri timu yake ya Wizara; kwa maana ya kuimarisha umoja, mshikamano na upendo katika Wizara hii ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tumeshuhudia pia ongezeko la bajeti katika Wizara hii, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ongezeko hili la bajeti litaiwezesha Wizara hii kufanya mipango yao vizuri ili kuweza kufikia yale malengo ya kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, kama ambavyo wametangulia kuzungumza wenzangu, kulizinduliwa Sera hii ya Mambo ya Nje. Sera hii itatupa faida nchi yetu ya kupata mafanikio makubwa katika sekta ya uchumi na pia kupata mafanikio katika anga ya mahusiano ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili ninapenda nitoe ushauri wangu kwa Serikali, kuwa iendelee kutoa elimu kwa wakulima wetu ili waweze kutumia fursa nzuri ambazo zilikuwepo katika diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina fursa nyingi za diplomasia ya uchumi. Ukiangalia kuwa tuna ardhi nzuri ambayo tunaweza kupata mazao mazuri kwa kilimo, tuna mifugo mingi, vilevile Mungu ametujalia tuna bahari pamoja na maziwa ambapo vyote hivi tunaweza tukavitumia kwa ajili ya kuujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuipatia Wizara yetu hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki eneo au kiwanja cha kufanya ujenzi kwa ajili ya Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kule Zanzibar. Jambo hili litawezesha mashirikiano katika ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuimarika na kuweza kukuza Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuiomba Serikali kupitia Wizara hii kuendelea kuziomba nchi rafiki ambazo tayari zina ofisi zao hapa Tanzania ziweze kufungua ofisi zao kule Zanzibar pamoja na hapa Dodoma ili kuweza kukuza ushirikiano uliokuwepo kati ya Tanzania na mataifa ambayo tunayo. Pia, ninaomba niipongeze Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukuza mashirikiano ya kidugu kati ya nchi yetu ya Tanzania na nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ninaomba nitumie fursa hii kuiomba Wizara yetu ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ishirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweza kuangalia fursa ambazo zinaweza zikapatikana katika utalii wa mikutano ya kimataifa. Si mikutano tu, pia kuna utalii wa michezo. Sasa hivi Serikali yetu imejiandaa katika kuweka miundombinu mizuri ya michezo, kwa hiyo ninaomba Serikali iweze kutumia fursa hizi ili kuweza kukuza pato la nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, ninaunga mkono hoja. (Makofi)