Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Cosato David Chumi na Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo; pia watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye suala la Serikali ya Marekani kufanya mabadiliko ya sera zake za diplomasia ya mambo ya nje ambazo zimeitikisa dunia na nini kifanyike.

Mheshimiwa Spika, Marekani imefanya mageuzi ya sera za misaada, elimu na biashara huria duniani na Tanzania ni miongoni mwa nchi wahanga. Rais Donald Trump wa Marekani ameanzisha mabadiliko ya kidiplomasia duniani katika nyanja mbalimbali na sera zake za diplomasia ya mambo ya nje zimeitikisa dunia. Vita hivi vimevuruga utaratibu wa biashara na mahusiano mengine ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, vilevile mabadiliko haya yasipoangaliwa kikamilifu yanaweza kuzitumbukiza nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika msukosuko wa mapato na malipo ya nje. Ni kwa mantiki hiyo, ninaiona Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa mdau mkubwa wa kulikwamua Taifa letu katika msukosuko huo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Rais Trump amesaini agizo la kuiondoa nchi yake katika Shirika la Afya Duniani (WHO). Utawala wa kiongozi huyo umechukua hatua ya kusitisha usambazaji wa dawa za kuokoa maisha ya watu wenye HIV, malaria na kifua kikuu mbali na dawa za watoto wachanga katika mataifa yote yanayosaidiwa na Shirika la USAID duniani, ikiwemo Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Rais Trump ametoa agizo kwa Chuo Kikuu maarufu duniani cha Havard kutosajili wanafunzi kutoka mataifa ya kigeni. Pia Rais Trump alipoingia madarakani alitia saini amri kadhaa za kiutendaji. Miongoni mwa amri za kiutendaji ilijumuisha kujiondoa katika mkataba wa hali ya hewa wa Paris na alielekeza kusimamishwa kwa muda misaada ya kigeni ya Marekani, kusitisha haki ya uraia wa kuzaliwa kwa watoto waliozaliwa nchini Marekani. Trump vile vile aliamuru ufanyike uchunguzi kwa kiwango cha juu iwezekanavyo kwa watu wote wanaotaka kuingia Marekani na kwa Serikali kuzitaja nchi ambazo zina matatizo ya uchunguzi ili kuwazuia raia wake kuingia nchini Marekani.
Mheshimiwa Spika, kidiplomasia, mambo yote haya si mema, kwani yametuathiri Watanzania na watu wengine duniani. Kama nchi ni vyema kutambua kuwa mabadiliko haya yanahitaji tuwe na machaguo mengi zaidi ya kukabiliana na dharau na vitendo vyake vya uhasama na imetupa akili ya kuangalia mbali na kupambana na hali yetu.

Mheshimiwa Spika, ni vyema ikumbukwe kuwa kwa sasa dunia sio eneo la nchi moja tena, pamoja na kwamba Marekani ni Taifa lenye nguvu duniani, lakini kiuchumi kuna nchi mbalimbali duniani zenye uwezo wa kuziba ombwe linaloachwa na Marekani. Baadhi ya wachambuzi walitabiri kuwa baada ya Marekani kuondoa misaada yake Barani Afrika, janga lingetokea. Ni muda sasa baada ya Marekani kufanya hivyo na tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba hakuna kubwa baya lililotokea hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ninaamini kwa dhati kwamba hatma ya Bara letu kiuchumi inategemea biashara na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na zile zinazoibuka kimaendeleo duniani.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ielekeze nguvu kushirikiana na mataifa wanachama wa Umoja wa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, afya, elimu ili kusaidiana kutatua matatizo yaliyojitokeza kutokana na hatua za Wamarekani.

Mheshimiwa Spika, hatua za Rais Trump badala ya kuleta masikitiko zinatakiwa ziwe chachu ya kutuweka pamoja na kutuletea maendeleo yetu wenyewe Barani Afrika.

Mheshimiwa Spika, Afrika itakuwa na mwelekeo mkubwa wa mafanikio kama tutazingatia utekelezaji wa Makubaliano ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA). Hivi sasa makubaliano hayo yameshaidhinishwa na Nchi 48 Wanachama na kuashiria fursa ya kihistoria kwa biashara ya ndani ya Afrika na Tanzania imesharidhia.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ina jukumu kubwa la kidiplomasia kutupia macho mambo haya nyeti na kulikwamua Taifa letu dhidi ya mkwamo wowote ule kiuchumi. Wizara inatakiwa itumie wana diplomasia wake kote duniani kushawishi nchi marafiki wenye nia njema ili kulikwamua Taifa letu kutokana na madhara ya uamuzi wa Serikali ya Marekani.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, ninaunga mkono hoja.