Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE (MHE. COSATO D. CHUMI): Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuturuzuku afya njema na uhai na kwa kuniwezesha kuendelea na utekelezaji wa majukumu yangu kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, nichukue fursa hii kipekee kumpongeza mwanadiplomasia namba moja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada anazozifanya katika kuitangaza Tanzania Kimataifa. Ninawaomba Watanzania wote na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ili aweze kutimiza malengo ya kuiletea nchi yetu maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ninaomba kuishukuru Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo nimehudumu kwa muda wa miaka tisa na nusu. Katika kipindi changu cha kuwa Mbunge toka 2015 nilipoingia ndani ya Bunge lako Tukufu nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kwa hiyo ninatumia pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba nimekuwa back bencher miaka tisa na nusu, lakini baadaye akaniona na kunisogeza huku mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki ni kitu ambacho ni shule kwetu; kuwa na ustahimilivu. Wakati wa Bwana ukifika mamlaka itakuona; na wakati ulipofika nilionekana na kwa kweli ninamshukuru Mheshimiwa Rais. Katika maisha yangu kwa mara ya kwanza Dkt. Samia Suluhu Hassan ananifanya nisimame hapa kuwa sehemu ya kutoa hoja upande wa Serikali. Mwenyezi Mungu wa Mbinguni ampe maisha marefu sana. Ninamshukuru sana kwa wengine wote pia ni namna ya kuishi katika ustahimilivu. Kama lipo jambo kwa neema ya Mwenyezi Mungu litakufikia. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa michango mbalimbali, lakini pia uniruhusu nitumie fursa hii pia kuwashukuru viongozi wetu wakubwa ndani ya nchi yetu; nikianza na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango; Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ambaye hapa tunapozungumza yuko Japan katika majukumu yale yale ambayo ametumwa na Mheshimiwa Rais kuiwakilisha nchi yetu kuendelea kutafuta fursa mbalimbali za masoko na uwekezaji; Mheshimiwa Kassim Majaliwa; Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko; na kama nilivyosema pale awali Kamati ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda nikufahamishe kwamba, viongozi wetu hawa wanafanya kazi kubwa sana. Mimi kama mmoja wa wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri ninapata fursa ya kusafiri kikazi na viongozi hawa. Hawalali, wanakutana na wawekezaji, wanakutana na washirika wa maendeleo. Ninaweza kuwatolea ushuhuda; moja ya safari tulikuwa London na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi. Kwa siku sita tulizokuwepo pale hakukupatikana hata siku moja ya kusema unaweza kwenda hata dukani ukanunue kitabu. Muda wote ilikuwa ni kazi kazi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya Wabunge wanayoyaona ni kwa sababu viongozi wetu wanafanya kazi kubwa, hawalali; na hiyo ukizingatia tofauti ya masaa hasa wanapokuwa katika ziara maeneo mbalimbali ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba uniruhusu na ninajiona nitakuwa ni mchoyo wa fadhila nisipomshukuru Mheshimiwa Waziri wangu Balozi Mahmoud Thabit Kombo. Ninawiwa kusema kwamba ninamshukuru Mungu na ninamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunipa nafasi ya kufanya kazi chini ya kiongozi mwenye upendo, problem solver na ambaye ni result oriented. Mimi na wenzangu katika Wizara tunajisikia ni watu wenye kubarikiwa kufanya kazi chini ya Mheshimiwa Waziri Mahmoud Thabit Kombo. Ni kiongozi anayefikika na ni kiongozi ambaye anashaurika.
Mheshimiwa Spika, ninakumbuka wakati wa Energy Summit kulitokea jambo, nikamwambia Mheshimiwa Waziri kwenye hili ninaomba wewe ndiye usimame. Akasema, Hapana, hiyo nimekupa wewe, nime-delegate, una baraka zangu zote, endelea. Nikamwambia, lakini kwa uzito wake Mheshimiwa ninaomba hili ulibebe wewe, akanielewa. Ni kiongozi anayeshaurika, ni kiongozi ambaye ameleta amani ya nafsi kwa watendaji katika Wizara; na sisi kama wasaidizi wake tunamwombea heri na utendaji mwema na uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, ninawiwa pia kumshukuru pacha wangu Mheshimiwa Denis Londo ambaye hayuko hapa, yuko katika majukumu ya kimataifa kwenye Mkutano wa Benki ya Maendeleo Afrika, ambayo mnafahamu kwamba imekuwa iki-support sana katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu. Kule kuna uchaguzi mkubwa wa kumpata Rais Mpya wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Makamu wa Rais yupo kule kuwakilisha nchi yetu na masuala mengine na Mheshimiwa Londo pacha wangu ndiyo maana hayupo katika Bunge letu siku ya leo ambaye ni Mbunge wa Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo na wananchi wa Mikumi wakiona hawamwoni basi wajue yuko kwenye majukumu ya kimataifa. Pia, watendaji wa Wizara wakiongozwa na Balozi Samwel Shelukindo, Balozi Steven Bundi na Naibu Katibu Mkuu Balozi Said Shaibu Mussa pamoja na wakurugenzi, watumishi na watendaji wote kuanzia wahudumu, masekretari, madereva, wote wanatupa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini ambao heshima hii niliyopewa na Mheshimiwa Rais si yangu, ni heshima yao Wanamafinga kupitia mimi mtoto wao. Ninawaomba waendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, waendelee kuniunga mkono na mimi mtoto wao. Wenyewe wanajionea; kama tunavyosema kule Mafinga, slogan yetu ni ile ile Mafinga ya Chumi, kazi zinaongea na kazi zitaendelea kuongea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana wananchi wa Mafinga Mjini. Tuendelee kuiombea nchi yetu kama mara zote nikisema katika mikutano. Kuombea viongozi wetu, kuombea familia zetu na kuombeana sisi kwa sisi, kwa maana ya ustawi wa Taifa letu. Ninataka niwafahamishe kwamba mimi Chumi bado nipo na tutaendelea kuwa pamoja kwa kadri ya uzima wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, niishukuru familia yangu, mke wangu, wanangu na wote ambao wanani-support katika shughuli mbalimbali za kuniwezesha kuwepo hapa. Vijana wanaoni-support nyumbani katika kazi zangu na kila mmoja ambaye kwa namna moja au nyingine ana mchango katika maisha yangu kufika hapa ambapo nimefika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nijielekeze sasa katika baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge; nianze na hoja za Kamati. Moja ya hoja ya Kamati imetueleza; na huu ndiyo ukweli; kwamba 70% ya Bajeti ya Wizara inakwenda kufanya kazi katika balozi zetu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zahor amesema hapa, kwamba mabalozi wachape kazi, na sisi tunakuja na performance indicator. Nia yetu ni nini? Ikiwa Mheshimiwa Rais na viongozi wetu kitaifa wanafanya kazi kubwa ya kuifanya nchi itambulike kimataifa, basi ni matarajio yetu kama Wizara kwamba ile 70% ya bajeti inayokwenda katika balozi wetu basi iwe na tija; iwe na return ya kutuletea wawekezaji, kufungua masoko, kuendelea kutangaza nchi, kupata watalii na fursa za ajira na fursa za elimu kwa watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakuja na mkakati wa kuwa na performance indicator ili asilimia 70 iendane; kwamba kile kinachokwenda katika balozi zetu basi kiwe na tija kwa Taifa letu la Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ya Kamati imezungumzwa kuhusu kuwafanya Watanzania waweze kuwa na uelewa wa lugha ya diplomasia ya uchumi. Mimi kama mjumbe wa Kamati wa muda mrefu tumelisema sana hili katika Kamati zetu; na hapa ninapenda kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kupitia sera yetu hii, toleo la 2024, humu pamoja na mambo mengine tumeeleza na Mheshimiwa Rais ametuelekeza; na hapa nitoe wito kwa sekta zote za binafsi na za umma; tutakapowajia kupitia mabalozi wastaafu basi watupokee. Hii ni katika kupanua wigo wa kufahamu fursa mbalimbali za ajira, za elimu, za masoko, za biashara na za utalii ambazo zinapatikana kupitia diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Kamati imezungumza ni faida ya ziara za viongozi. Mheshimiwa Waziri wangu atasema kwa upana, lakini moja wapo kama ambavyo tumesema ni pamoja na kutafuta masoko, kuvutia wawekezaji, na kuleta watalii. Lingine lililo muhimu ni pamoja na kuvutia mikutano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninyi wenyewe mmeona katika muda mchache tumeona mkutano kama wa Energy Summit, ambao mimi nilihusika kwa takriban 60% kupokea na kuwasindikiza viongozi wakubwa waliokuja katika mkutano ule. Wote kwa mujibu wa kidiplomasia, nilipokuwa nikiwapokea ninakwenda nao kwenye gari mpaka hotelini wananiambia, tumekuja kwa ajili ya heshima ya Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wahehe wana msemo, “Kawo kobita, kawo kopiluka.” Mkono utoao ndiyo mkono upokeao. Mnapoona viongozi wetu wanakwenda na wao ndiyo wanaweza kujenga imani ya wengine nao kuja; na wale wanapokuja maana yake ni kwamba, kama nilivyosema, tutafungua masoko, tutatafuta wawekezaji, tunaleta watalii, tunafungua fursa mbalimbali katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge pia wameona, tulikuwa na Mkutano wa e-Learning hivi karibuni na wenzetu wa Wizara ya Elimu; vilevile tukikuwa na Mkutano wa Coffee Summit na wenzetu wa Wizara ya Kilimo, lakini the most important, hili ni lazima tulielewe, viongozi wanapofanya ziara, wanavyokutana na wawekezaji na washirika wa maendeleo maana yake ni nini? Kuna kitu kinaitwa political will, maana yake unawapa imani, unawajengea, kuaminika na kuaminiwa zaidi na wale ambao unaenda kukutana nao. Kwa hiyo, ziara hizi zina mchango mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema masoko, biashara lakini political will. Waheshimiwa Wabunge wameelezea kuhusu AFCON na CHAN na mimi kama mwanamichezo ninapenda kusema kwamba, sisi kama Wizara tuko tayari kushirikiana na wenzetu katika kuhakikisha kwamba tunaimarisha, si tu diplomasia ya uchumi na public diplomacy bali pia na kitu kinaitwa sports diplomacy. Tumeona vilabu vyetu vya Simba na Yanga miaka miwili mfululizo vimefika Fainali ya Confideration, ni sports diplomacy.

Mheshimiwa Spika, tumeona vile vile tuna watoto wetu katika michezo, watoto wa kike wanacheza katika ligi huko duniani. Wako watoto wanacheza; akina Clara Luvanga wako Saudia Ligi, wako Mexico; hii yote ni sports diplomacy. Kwa hiyo tunaahidi kushirikiana na Wizara zinazohusika kuhakikisha kwamba, kama tulivyofanya katika Energy Summit na katika CHAN na katika AFCON tutakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba sports diplomacy inaendelea kuthibitika chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia ninaona umewasha, imezungumzwa kuhusu diaspora. Mheshimiwa Dkt. Kimei amesema vizuri sana tuna hiyo Diaspora Digital Hub, tunatoa wito na Sera yetu kwa mara ya kwanza pamoja na mambo mengine imeelezea ushiriki na ushirikishwaji wa Diaspora. Kwa hiyo ni uthibitisho kwamba, tunapanua wigo wa ushiriki wa Diaspora ili na wenyewe wawe na mchango katika Taifa letu wa kiuchumi na kiuwekezaji; lakini na wenyewe kama mabalozi wetu wa kutafuta fursa kule nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninarudia tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia na Bunge lako Tukufu na nimalizie kwa kusema kama utaridhia kwa lugha ya kueleweka kidogo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa, muda umekwisha, malizia sekunde tatu.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE (MHE. COSATO D. CHUMI): Mheshimiwa Spika, niwaombe Watanzania tusijichukulie poa tupo vizuri duniani, tujiamini tumuunge mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)