Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninapenda kukushukuru tena kwa nafasi nyingine kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa ufafanuzi wa kufanya majumuisho ya mjadala ambao umekuwa ukiendelea pamoja na michango ya Wajumbe mbalimbali. 
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukushukuru na kukupongeza tena kwa kuongoza na kusimamia mjadala wetu wewe pamoja na Naibu Spika ambaye tulianza naye asubuhi kwa umakini mkubwa na umahiri. Niwashukuru pia sana Waheshimiwa Wabunge kwa kushiriki kikamilifu katika mjadala huu na kimsingi maoni yao, michango yao na ushauri pamoja na yale yote ya nyongeza tumeyapokea, tutayazingatia, tutayafanyia kazi na pia kuyaboresha. 
Mheshimiwa Spika, niwaombe jambo moja tu Waheshimiwa Wabunge, hasa wale waliochangia nitawataja sasa hivi. Fursa nyingine ni za kwetu pamoja, mimi leo ningekuwa katika nafasi yenu Mabalozi wote hawa ambao wapo basi ningewatumia kwa ajili ya miradi mbalimbali majimboni. Tuna nchi zaidi ya 52 leo wako pale juu na hii ni fursa wametoka kwenye maofisi yao kuja hapa. Kwa sababu kule ukienda kwenye maofisi yao kuna mageti, kuna walinzi, wanaku-search na kadhalika, leo wako katika uwanja wa nyumbani. Kwa hiyo, ninaamini sana Waheshimiwa hasa wale wenye majimbo na miradi maalum watatumia fursa hii ya kuwa na mabalozi hapa; lakini sisi kwa upande wa Wizara yetu pia tutajitolea katika hilo kuwasaidia na kuwanganisha nao moja kwa moja. 
Mheshimiwa Spika, wapo mabalozi hapa ambao nchi zao zinahitaji juice ya machungwa, kwa hiyo machungwa ya Korogwe yanaweza yakakamuliwa yakafungwa vizuri katika vifungashio na kufika kwao. Hilo tulianze hapa hapa tusiache fursa hii kututoka. Hiyo ndiyo diplomasia ya uchumi kwa vitendo na inaweza kuanzia katika Ukumbi wako wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa ninaomba kuishukuru tena Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi mahiri kabisa wa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa pamoja na Wajumbe wake wote wa Kamati, kwa kuipatia Wizara yetu ushirikiano mkubwa na kwa michango yao mizuri na mahiri sana yenye kujenga. Kama walivyosema leo, wametoa yenye kujenga na tumepokea na ninawaahidi tutaifanyia kazi kwa kadri ya uwezo ambao Mwenyezi Mungu atatujaalia mimi pamoja na wenzangu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wako ulionipa ni mdogo na sitoweza kuwatambua wote, lakini ninaomba niwatambue kwa uchache kabisa na michango yao na kujaribu kwenda moja kwa moja kwenye michango. Moja, nimelieleza hilo la diplomasia ya uchumi kwa vitendo. Ninamshukuru sana aliyechangia kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula. Kwanza, nichukue fursa hii ya kumpongeza kwa nafasi kubwa aliyoipata hivi karibuni ya kuwa Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika kwenye masuala ya wanawake, amani na usalama. Hongera sana Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula anaungana katika orodha ambayo wewe umo kama ile ya IPU ya Watanzania wanaoleta sifa kubwa la Taifa letu Kimataifa. Haya yote yamefanyika wakati wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwanadiplomasia nambari moja. Ninaomba niwataje wachache, kwa sababu tunataka kutumia ukumbi huu pia kuwafikishia Wabunge ambao wana majukumu na wajibu wa kufikisha kwa wananchi. Kwa sababu leo yamezungumzwa mengi sana, lakini ninataka baadaye kueleza kwamba tunashirikiana pamoja. 
Mheshimiwa Spika, mwananchi wa kawaida akiwa hajui Diplomasia ya Uchumi na Mbunge naye anahusika kama ninavyohusika mimi na Wizara yetu ya Mambo ya Nje. Kwa sababu Wabunge wanapokea kwa wananchi na kuyaleta hapa Waheshimiwa Wabunge, lakini wanawajibu kwa kutoa hapa na kurejesha kwa wananchi. Kwa hiyo, leo kupitia kwako, ninaomba niwatambue Watanzania, hawa Watanzania kwenye nafasi za kimataifa hawawi hivi hivi bila ya kupewa ridhaa na nchi yao. Hawa Watanzania hawapewi nafasi hizi bila ya Rais mwenyewe kuridhia na kusaini, hayo ninawaambia wazi.
Mheshimiwa Spika, Mtanzania aliyekuwa kwenye nafasi hata akifanyiwa interview inaulizwa nchi, kuna Mtanzania huyu amefanya kwa zile nafasi za interview, siyo hizi za akina Profesa Janabi za kura, hata zile za interview ni lazima nchi yake inaulizwa wanaita Country ama State Endorsement. Kama ulivyokuwa-endorsed wewe Mheshimiwa Spika kwenda IPU na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitawataja kama ifuatavyo:-
(1)	Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani. (Makofi)
(2)	Profesa Mohamed Yakub Janabi, Mkurugenzi Mteule hivi sasa wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika. (Makofi)
(3)	Dkt. Deo Mwapinga, Katibu Mkuu Jukwaa la Mabunge (ICGLR). (Makofi)
(4)	Dkt. Emmanuel Manase, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kimawasiliano Duniani (ITU) Geneva, yuko Geneva anachukua nafasi kama ile ya Janabi kwa Ukanda wa Afrika. (Makofi)
(5)	Dkt. Joyce Msuya, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura Duniani (Joyce Cleopa David Msuya). (Makofi)
(6)	Mheshimiwa Elizabeth Maruma Mrema, huyu ni Assistance Secretary General (Msaidi wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa) na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira Duniani. (Makofi)
(7)	Dkt. Neema Rusiba Maila Kimambo, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani ambaye yupo katika Ukanda wetu huu wa SADC Malawi. (Makofi)
(8)	Mheshimiwa Mariam Salim, Mwakilishi wa Benki ya Dunia yuko Eritrea Ethiopia ambaye pia anafanyia kazi South Sudan na Sudan yenyewe. (Makofi)
(9)	Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia akiongoza Kanda ya Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna sababu ya kutosha Tanzania kujivuania katika nafasi hizo na sijamaliza nimefikia robo tu, ninaomba uniruhusu nimalizie ili wananchi waweze kuwa na uelewa kupitia Wabunge wao. 
(10)	Mheshimiwa Dkt. Lalislaus Chang’a, Makamu Mwenyekiti Jopo la Wanasayansi wa Masuala ya Tabianchi Duniani.  (Makofi) 
(11)	Dkt. Pascal Waniha, Makamu Mwenyekiti Kamati ya INFOCOM ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani, wote wanatoka katika majimbo ya Wabunge. (Makofi)
(12)	Mheshimiwa Dkt. Mohamed Juma, Mkurugenzi wa Afrika kwenye Kituo cha Urithi wa Dunia cha Afrika.  (Makofi) 
(13)	Profesa Joram Mukama Biswaro, Mwakilishi Maalum wa Kamishna wa Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika Sudani ya Kusini.  (Makofi) 
(14)	Dkt. Richard Muyungi, Mwenyekiti wa Kundi la Wataalamu wa Afrika katika Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
(15)	Bi. Sara Mbago-Bhunu Mkurugenzi wa Division ya Mashiriki ya Kusini mwa Afrika kwenye IFAD, hawa ndiyo wanashughulikia kilimo, mbogamboga, mifugo, uvuvi na kadhalika.  (Makofi)
(16)	Mheshimiwa Jaji Imani Aboud, Rais wa Mahakama ya Haki ya Watu ambaye leo ametetewa sana katika jengo lake Mjini Arusha.  (Makofi) 
(17)	Wa mwisho anayeungana na orodha hiyo ni Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika Masuala ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inaashiria kweli hizi taarifa huwa hazitoki na wala hatuwi na uelewa wa Tanzania tunaelekea wapi, lakini tutajitahidi kupitia jukwaa hili pamoja majukwaa mengine ya habari kupitia Bunge lako Tukufu kufikisha taarifa hii. 
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo limezungumziwa pia ni kuhusiana na majengo. Hili la majengo limezungumziwa sana, lakini nitumie fursa hii kusema kwamba tutakwenda hatua kwa hatua. Tuna majengo 105, aliajiriwa yule anayetoa ushauri kuhusiana na masuala ya majengo na kwa mujibu wa uwezo wetu tutakwenda na majengo 10 kwa uwezo huu wa Serikali pamoja na Mashirika ya Umma. 
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kutoa wito kwa sababu Wabunge wengi katika maoni yao na michango yao wamesema kwamba tushirikishe pia sekta binafsi. Nichukue fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu, kuwaalika pia wale waliokuwa kwenye sekta binafsi kwa sababu haya majengo yako nchi mbalimbali duniani. Watoe expression of interest, waeleze hamu ama nia ama dhamira yao ya kutaka kuingia ubia na Serikali. Sisi tutapokea na tutafikisha kwenye vyombo husika kwa sababu hii michakato inapitia vyombo vingi ili kupokea. Mpaka sasa hivi tumepokea wawekezaji wawili kutoka sekta binafsi ambao wameonesha nia na dhamira kwa majengo yetu yaliyokuwa kule nchini Marekani katika uwekezaji, tumeyapokea na hivi sasa hivi yanafanyiwa kazi. 
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunatoa wito huo, kwa sababu haya majengo ni mengi hatuwezi kuyafanyia kazi mara moja. Juzi nilibahatika kutembelea Nchi ya Uganda na nimekuta jengo letu liko pembeni ya Ubalozi wa Marekani na hali yake siyo nzuri limeachwa miaka mingi na ninaamini Wajumbe wa Kamati wengine walitembelea lile jengo la Balozi Uganda. Liko sehemu nzuri sana, kwa sababu kuna-view pale Waingereza huwa wanaita One Million Dollar View ambayo iko pale inaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kila sababu, hoja na faida pia ya kuendeleza jengo lile. Kwa hiyo, tunakaribisha sekta binafsi kuja, utajiri tuliokuwa nao nje ya nchi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mkubwa sidhani kama kuna nchi nyingi duniani zenye majengo, mali yao 105 nje ya nchi zao, siyo nchi nyingi duniani, ninaamini tumo katika 10 bora. Kwa hiyo, tunakaribisha sekta binafsi kuja kuungana nasi na tutafanya kazi kwa karibu sana na Kamati yake Mheshimiwa Vita Kawawa pamoja na Wajumbe, kwa sababu wametoa maoni mengi katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana ripoti ya Kamati imekuwa ikijenga kwenye maeneo mengi sana. Wamezungumzia kuhusu bajeti ya maendeleo, wamezungumzia sehemu kubwa 70% tunatumia Ubalozini kwetu, lakini tija wakati mwingine na mrejesho unakuwa mdogo. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mchango wake ametoa ufafanuzi lakini ninaomba na mimi niweke msisitizo kwamba mara hii tunakwenda na zile KPI halisi kwa Mabalozi wetu wote. Kwa hiyo, watakuwa wanaulizwa kutokana na matokeo halisi. 
Mheshimiwa Spika, tutajihusisha zaidi na AFCON siyo letu moja kwa moja wengi hawalijui, lakini tutajihusisha zaidi. Tutajipendekeza, tutajishirikisha, tutajiingiza na sisi tuwemo katika hili la AFCON, kwa sababu ni maagizo hata ya Mheshimiwa Rais wakati anaapisha Mawaziri wakati ule alitoa maagizo hayo. Kwa hiyo na sisi tutajishirikisha zaidi kulibeba pamoja na wenzetu wanaolisimamia moja kwa moja. 
Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Zahor ameeleza mengi sana, lakini nipokee pongezi zake na niwahakikishie Waheshimiwa wote waliompongeza Mheshimiwa Rais atazipata pongezi zenu na sisi tutazipokea kwa ajili ya kuzifikisha. 
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ushiriki wa sekta binafsi, tumepokea. Nishukuru mchango wake kuhusiana na diplomasia ya uchumi kwa vitendo. Ninaomba kupitia Bunge lako tutawashirikisha pia Waheshimiwa Wabunge wote juu ya Mwongozo wa Diplomasia ya Uchumi ili kuwatumia wao kama fursa kwetu sisi kufikisha taarifa, elimu kwa wananchi wao kutoka maeneo mbalimbali, hilo tutalifanya. 
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Alfred Kimea, ninaomba nimwambie fursa Korogwe Mjini inaanzia leo, siyo kesho wala kesho kutwa. Fursa ya machungwa ya Korogwe ianzie hapa hapa kuna nchi zaidi ya tano nitamtambulisha nazo sasa hivi moja kwa moja pale juu, ambao wana mashine za kukamua na kufunga.  Ninawajua kwa sababu walishatuletea na mojawapo ni Saudia yuko pale juu Saud Arabia, wao wana uhitaji mkubwa sana. Kwa hiyo fursa hii tutaunganisha hapo hapo ili irudi kwa wananchi kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda kutoka Newala, yeye ni Mjumbe wa Kamati alichangia sana kwenye Kamati na atufikishie salamu zetu kule Pachoto kwetu. Hata hivyo, niseme kwamba, bado tunaendelea, tunaendelea na mara hii tunataka tuwashirikishe Wabunge pia. Tumewashirikisha Mabalozi, lakini katika hii Kampeni ya Royal Tour inayoendelea tunataka tuwashirikishe na Wabunge pia kwa uchache. Tutaanza na Kamati yetu halafu tutakwenda kwa wengine ili tuweze kutanua wigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikujulishe pia kama Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alivyokuwa ametuwekea mfano mzuri wa kuwashirikisha wafanyabiashara na sekta binafsi. Ninaomba nikujulishe kupitia Bunge lako na nimeanza programu hiyo ya kuwashirikisha wafanyabiashara na sekta binafsi katika kila safari ninayokwenda ambayo inakuwa na jukwaa la biashara, ili hii diplomasia sasa ishuke kwa vitendo, Diplomasia ya Uchumi. 
Mheshimiwa Spika, nimekwenda Mjini Vietnam ...
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ninadhani husikiki vizuri. 
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ninasikika sasa hivi?
SPIKA:  Ndiyo, endelea.
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI:  Mheshimiwa Spika, nimechukua wafanyabiashara wote jumla saba ambao tumeambatana nao na niseme tu wamefanya vizuri sana kwenye zao la kahawa; katani, kule Vietnam; kwenye zao la korosho, wonderfully performance na matokeo yalikuwa mazuri sana. Kwa hiyo, tunataka kuongeza wigo, bahati nzuri wao wanajilipia wenyewe hawachukui chochote kutoka kwenye bajeti ya Serikali. 
Mheshimiwa Spika, tiketi wanajikatia wenyewe, wengine wanakaa First Class, sisi tunakaa Business Class, kwa hiyo wanakuwa wamekaa mbele yetu kwenye ndege.  Kwa hiyo, hiyo ndiyo tija na faida ya biashara. Kwa hiyo, hilo wala hatuoni wivu tunasikia raha na fahari kwamba, mfanyabiashara akiwa amekaa hata mbele kuliko Serikali, kwa sababu mwisho wa siku ile kodi inarudi kwenu. Kwa hiyo, hilo tumeshajiisha, tunazidi kuwashajiisha na kupitia kwenu tunaenda kuwashajiisha wafanyabiashara zaidi ili kwenda nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana wale wote waliokuja leo kutuunga mkono pamoja na ndugu yangu Dkt. Abdulmajid Nsekela CRDB. Wao wamekuwa pia katika mstari wa mbele pamoja na wenzao wengine NMB; na benki nyingine zote wamekuwa mstari wa mbele sana. Ahsante sana ndugu yetu Abdulmajid Nsekela katika kutuunga mkono panapokuwa na fursa. Siyo hivyo tu, wamefungua branch kwenye nchi zote tunazopakana nazo ili Watanzania waweze kufanya biashara zao kwa urahisi zaidi na fedha zao ziweze kwenda zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema kwamba, hajaipata kutokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nina miezi 11 leo kamili katika Wizara hii, niko miezi 11 kamili. Haijawahi kutokea Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata zawadi na kutambuliwa duniani, Goal Keepers Award, UAE Award na zawadi ya Kimataifa, kwa kazi ya Clean Cooking kuwa Champion AU; kule SADC nyingi kama hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani nina orodha za hizi awards alizopata duniani nyingi sana kiasi kwamba siwezi kuzitaja, lakini nitawasilisha kwa maandishi. Mpaka kule kwenye mazingira; kwenye masuala ya COP; kwenye masuala ya Umoja wa Mataifa; pia kwa Bill Gate Foundation as well. Kwa hiyo, hayo yote yametokea katika kipindi hiki kifupi, ambacho Mheshimiwa Rais wetu ameonesha njia kubwa sana ya mafanikio ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na AICC tumepokea yote na wadaiwa sugu ni kweli ni Mashirika ya Serikali. Nimepokea mchango wa Mheshimiwa Grace Victor Tendega, juu ya kwamba tufanye kama sekta binafsi sasa hivi, hujalipa huingii, hujalipia ukumbi hufanyi shughuli yako pale. Kwa hiyo na sisi tutajitahidi kulifanya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Festo Sanga, Jimbo la Makete kuhusiana na mikoa ya jirani, mikoa iliyoko karibu na mipakani, tutaifanyia kazi yote na kuimarisha mawasiliano. Nimshukuru sana Mheshimiwa Ali Raza jimbo la Shaurimoyo kwetu huko kwa Mtiptip, juu ya ushawishi mkubwa wa kimataifa, kuimarisha umoja na mshikamano kati yetu. 
Mheshimiwa Spika, niseme tu siri kubwa ya mafanikio hata humu Bungeni, hata nyumbani kwako binafsi ni mshikamano, ushirikiano na upendo. Hayo mambo matatu na sisi ndiyo msingi wetu Wizarani inaondoa fitna, inaondoa hasadi, inaondoa chuki, inaondoa migongano. Mtu yeyote atakayekuletea fitina unamwambia hapana tukae tulijadili pamoja, kwa hiyo fitna zile ndogondogo nyingi zinaondoka hiyo ndiyo siri yetu ya mafanikio. Kwa hiyo tunapiga vita sana fitna. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza Mwenyezi Mungu ndiyo mpangaji. Mpangaji wa maisha yetu, pumzi zetu na nafasi zetu, wengine sisi hatukulalia, wala hatukuamkia lakini leo Mwenyezi Mungu ametujaalia mimi niko mbele yenu kwa mara ya kwanza kabisa ninasoma. Yeye kwa mara ya kwanza miaka tisa na nusu, mimi kwa mara ya kwanza katika miezi 11. Kwa hiyo, yote hayo anayepanga ni Mwenyezi Mungu na ninaamini Mwenyezi Mungu atatupangia mazuri zaidi kwa muda huu tunaokwenda nao, kwa muda ujao kuanzia Rais wetu mnamo mwezi Oktoba, pamoja na nyinyi nyote Waheshimiwa Wabunge. 
Mheshimiwa Spika, kwa Mtiptip, nimeona juzi anatangaza jimbo limebadilishwa jina, jimbo jipya na kadhalika na kwako pia nimeona na nimefuatilia kwa makini sana kwenye luninga. Kwa hiyo, nichukue fursa hii pia kukupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la conference tourism na Mali tourism hapa katika maono miongoni mwa maono makubwa ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huwa anatuambia sisi Waheshimiwa Mawaziri wake la kwanza kabisa kuliamini jambo, you have to believe in it kuwa litafanikiwa.  Kwanza kabisa jambo lolote lazima wewe mwenyewe uliamini kwa asilimia zote, usipoliamini haliwi na hata Mwenyezi Mungu haweki mkono wake usipoliamini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiliamini na Mwenyezi Mungu naye anakuwekea mkono wake yeye ameamini suala la kupunguza vifo vya watoto duniani, amepata Goal Keepers Award leo Tanzania inasifika duniani kwa kupunguza vifo vya watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ameamini kuokoa afya za mama na mtoto katika kifua, kuvuta pumzi kwa moshi wa kuni amefanikiwa leo amepata double champion amekuwa champion wa afya za akinamama na Watoto, lakini amekuwa champion wa mazingiza limegeuka lile la afya limekuwa la mazingiza dunia kwa sababu She believed in it alikuwa ameamini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ameamini katika kazi zetu sisi tunazozifanya tumefanikiwa baada ya Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kufariki dunia mwenzetu hapa Mheshimiwa Rais aliingia unyonge sana tukawa tunasema sasa hii nafasi ndiyo imetupotea Tanzania, lakini akaamini akasema yupo Mtanzania mwingine atasimama, Profesa akatutia maana na sisi tulikuwa tumeumia, tumevunjika moyo akatutia sisi nguvu za kiajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yupo yule Mheshimiwa Neema Lugangira na Mheshimiwa Elibariki Kingu, tumekwenda nao hawa wametutia nguvu kule tumefika Geneva tumepiga kampeni zinashindana na za CCM kampeni zile tumekuja na ushindi na ninaamini ushindi wa CCM nao utakuja, tumekuja na ushindi wa Profesa Janabi kuwa mshindi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kila jambo ni kuliamini na ninashukuru sana Mheshimiwa Kiongozi wetu Mkuu kwa sababu yeye ni mwana diplomasia namba moja ukiangalia katika mfumo wa Wizara hii, hii Wizara ya Mheshimiwa Rais kwa sababu yeye ni namba moja, wengine wote wanafuata huko. Kwa hiyo, maono yake ndiyo yaliyoleta mafanikio yote haya na sisi maono yake ndiyo yanayotupa nguvu, wakatupa sifa zote leo ni maono yake yanayotupa nguvu na imani yake ambayo sisi tumekuwa tukiifanyia kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niwashukuru wachangiaji wote pamoja na wale ambao sijawataja niwashukuru kwa michango yao. Sasa kwa sababu kengele zimeshapigwa kadhaa naona hapa na utaratibu huu ni mara ya mwanzo, wengine wageni hatutaki kuvunja utaratibu huu, tusije tukaonekana watu wa ajabu ajabu. 
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutumia ile lugha ambayo inatumika hapa, ninaomba kutoa hoja na kuunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Kombo wewe unatoa hoja tu wanaounga mkono ni hao waliosimama.
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa sababu nilijua nami Mheshimiwa Mbunge kwa hiyo naunga mkono. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya maelezo hayo, sasa ninaomba kutoa hoja. (Makofi)