Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumthibitisha Waziri Mkuu chini ya Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni ya 33 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumthibitisha Waziri Mkuu chini ya Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni ya 33 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. WILLIAM V. LUKUVI: Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima, ninapenda kukushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kabla ya yote, ninamshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha leo katika siku hii yenye nuru kubwa na upendo iliyotuwezesha kukutana hapa na kufanya kazi hii muhimu kabisa ya Kikatiba.

Mheshimiwa Spika, kwanza, ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha sisi Watanzania kufikia uchaguzi uliofanyika tarehe 29 na kukamilisha kwa amani na utulivu na kutuwezesha sisi Wabunge humu ndani kuweza kuchaguliwa na kuaminiwa na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, leo nimshukuru tena kwa kutimiza kazi nyingine ya Kikatiba ya kutuletea mwenzetu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ili tumthibitishe kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maelezo mengi yametolewa na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, na mimi ninayaunga mkono kwa sababu ninathibitisha yote aliyoyasema ni sahihi, na pengine ni kwa sababu ni mtu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wale Wana-CCM wenzangu niwakumbushe mengine ambayo ninadhani Mwanasheria Mkuu hakuyaandika. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba tumekuwa naye, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa miaka mingi. Amekuwa Mjumbe wa Kamati Mkuu ya Chama cha Mapinduzi kwa muda mrefu, na amekuwa Mjumbe wa Sekretarieti yetu ya Chama, lakini amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi. Ninawakumbusha Wana-CCM wenzangu kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakukosea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwanasheria Mkuu amesema hapa kwamba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ni Mchumi mbobezi. Ni kweli amesomea, lakini niwakumbushe tu, kabla hajajiunga na uongozi wa Chama na Ubunge, alitokea Benki Kuu, kuthibitisha kwamba Benki Kuu hawachukui watu hivi hivi tu, wanachukua watu wenye uwezo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu huyu ametoka Benki Kuu kabla hajajiunga na masuala haya ya siasa.

MHE. MUSSA A. ZUNGU - SPIKA: Mheshimiwa Lukuvi, malizia.

MHE. WILLIAM V. LUKUVI: Mheshimiwa Spika, kwa sisi tuliokaa Bungeni muda mrefu, tunajua uvumilivu alionao Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa mema na mishale mingi aliyopigwa, lakini hajatetereka, hajatetereka. Mafanikio tunayoyaona ndani ya nchi hii, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza miradi mingi sana iliyotuletea mafanikio, na sisi Wabunge leo tunajivuna na tumechaguliwa kutokana na hayo, lakini mkusanya ushuru ni huyu aliyowezesha mafanikio hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaunga mkono jambo hili na ningependa Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuliunge mkono kwa asilimia mia moja ili tumheshimishe Mheshimiwa Rais, lakini tumpe nguvu na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ili aanze kazi yake vizuri. Ninakushukuru sana. (Makofi)