Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Peramiho
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuifikia siku hii ya leo. Pia niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa ushindi mkubwa ambao ameupata katika uchaguzi wa mwaka huu, tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikupongeze na wewe pia kwa kukalia Kiti hicho. Tunakupongeza sana na tuna imani kubwa na wewe utatuongoza ili kufanikisha ndoto na maono ambayo tunayatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kabla sijaendelea ninaomba nitamke kwamba ninaunga mkono hoja ya uteuzi wa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaomba niseme, sifa zilizosemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni stahiki na ni sahihi kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kupata madaraka hayo na kuweza kusimamia nafasi hiyo kubwa ya uratibu ndani ya Serikali, ili tuweze kufanikiwa kuyafikia malengo, na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa hizo nyingine ambazo zimesemwa na Mwanasheria Mkuu, ninaomba niongeze sifa chache. Kwanza, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ni mtu wa maono. Anayo maono ya kujua Taifa letu linataka kwenda wapi? Pia, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba anajua vipaumbele vya nchi hii. Nini ambacho kinatakiwa kufanyika kwa sasa katika Taifa letu la Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini ninasema hivyo? Kwanza, muungaji mkono aliyetangulia ameeleza vizuri mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, hakika yasingeweza kupatikana kama tungekuwa na Waziri wa Fedha ambaye hakutekeleza vizuri majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote tunafahamu mapato ya ndani katika nchi yetu ya Tanzania kupitia TRA iliyokuwa chini ya Wizara ya Fedha, yameendelea kuongezeka na kusababisha mageuzi makubwa ya maendeleo katika nchi yetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, Mheshimiwa Rais wetu ametueleleza kupitia Ilani ya Uchaguzi, lakini ndani ya siku 100 anayo maono yake na malengo yake ambayo yanakwenda kumgusa Mtanzania mpaka wa hali ya chini. Maono hayo yanamhitaji Waziri Mkuu kama Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ili yaweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwa huduma hizo za afya, ujenzi wa uchumi, mabadiliko ya kimfumo ndani ya Serikali yetu, usimamizi wa Serikali, kwa sifa alizonazo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, niwahakikishia maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yatakwenda kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ninaomba uniruhusu niwashawishi Wabunge na kuwahakikishia uwezo wa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba katika nafasi hiyo, unatokana pia na kazi kubwa aliyoifanya, na akishirikiana na Mawaziri wengine na yeye akiwa miongoni mwa Mawaziri ambao wametengeneza Dira ya Taifa tutakayokwenda nayo mpaka mwaka 2050. Kwa hiyo, tunakwenda kupata Waziri Mkuu anayelitazama Taifa mpaka miaka ya 2050. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba ninafahamu Dkt. Mwigulu Nchemba alikuwa ni miongoni mwa wajumbe walioandaa Ilani ya Uchaguzi ya 2025/2030. Tumepata, tumeletewa Waziri Mkuu ambaye alikuwa ni mmoja wa waandaaji wa Ilani, kwa hiyo anaifahamu ilani hiyo na atakwenda kuisimamia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Dkt. Mwigulu Nchemba ni jasiri na msimamizi wa mambo. Anataka mambo yatokee, kwa hiyo, bila shaka tumuungeni mkono katika nafasi hii, tumepata chaguo sahihi na tutakweda kusimama naye kutekeleza majukumu yetu kwanza kama Wabunge, lakini tutakwedna kumsaidia Mheshimiwa Rais na Serikali kuyafikia malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono azimio hili na ninamtakia kila la heri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba katika kazi yake hii mpya ya Uwaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)