Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ushindi mkubwa alioupata kwa 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Waziri Mkuu Mteule, Mheshimiwa Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba ambaye azimio limesomwa hapa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili sisi Wabunge tuweze kumthibitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninasimama hapa kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na kuwaomba kwamba kwa kweli hatuna sababu ya kutokumthibitisha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kura zetu zote. Sifa zake zimeelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini pia zimesemwa na wasemaji waliotangulia. Hakuna shaka juu ya usomi na ubobezi alionao Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Hakuna shaka juu ya uzoefu wa uongozi alionao kuanzia kwenye chama na kwenye Serikali, kwamba, ameshika Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Fedha na Uchumi na baadaye Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameshiriki katika uongozi wa Wizara ya Fedha katika mazingira magumu na tata tukitoa kwenye Covid 19. Pia, tulikuwa na miradi mikubwa ya kimkakati ambayo hakuna hata mmoja uliosimama, yote imeendelea kutekelezwa kwa sababu alikuwa katika kutafuta fedha akimsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninataka niseme, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ni Waziri Mkuu wa kipindi hiki ambaye anastahili na mwenye sifa zote. Bunge hili 90% kama sikosei ni watu wenye umri chini ya miaka 50. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa uzoefu walionao wa kukaa humu Bungeni na uzoefu wa uongozi, atatuunganisha vizuri sisi wazee na vijana waliokuja. Maana moja kati ya majukumu yake ni kusimamia shughuli za Serikali humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nimalizie kusema sifa chache ninazozifahamu za Ndugu yangu Waziri Mkuu Mteule Mheshimiwa Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba. Unachokiona usoni kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ndicho kilichopo moyoni mwake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtu yeyote akienda kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anahisi kama anaenda kumwona mtu wa chini sana. Ni mtu wa kujishusha na mtu ambaye hajikwezi. Pia, moja kati ya sifa nyingine kubwa ambayo ninaamini imemsukuma sana Mheshimiwa Rais, ni uhodari wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tupo hapa Bungeni, sisi wengine muda mrefu tumewaona Mawaziri wa Fedha mbalimbali; Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba atashuka Airport kwenye ndege atakuja moja kwa moja Bungeni hapa, siyo kitu chepesi. Atatoka nje ya nchi, ataingia Dar es Salaam, atakuja Dodoma, atakuja Bungeni hapa hata kwa dakika 15 yupo tayari kuja Bungeni hapa kwa sababu anajua Bunge ndiyo chombo kinachowawakilisha wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninataka niseme kwamba, ninawaomba sana wenzangu Waheshimiwa Wabunge ili tumjengee heshima Waziri Mkuu wetu anayekuja lazima tumpe kura zote za ndiyo. Ili tujenge heshima kwa mamlaka iliyomteua, ni lazima tumpe kura zote za ndiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono Azimio la kuthibitisha Waziri Mkuu. Ahsante sana. (Makofi)