Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika hoja iliyopo mezani inayohusu Wizara yetu ya Maji na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja Wizara hii, maana mambo mengi makubwa na mazuri Waziri wangu amesoma asubuhi, na mimi ningefikiri kama utaratibu ungekuwa unaruhusu, basi baada ya Mheshimiwa Waziri kumaliza kusoma Bunge lingeweza kuunga tu mkono na kupitisha bajeti tukawa tumemaliza. Kwa sababu kila kitu amekieleza pale na kweli kilikuwa kizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru Makamu wangu, Mheshimiwa Profesa Pius Yanda kwa kusoma taarifa ya Kamati, unajua mahali pale ni madhabahu ya Bunge, kwa hiyo, huwa pana uzito wake, lakini tunamshukuru amesoma vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kwanza kwa kuishukuru Serikali, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mazuri sana kwenye Wizara ya Maji. Ongezeko la fedha limekuwa kubwa, wakati tunaanza Bunge hili hasa lililopita tulikuwa tunakaribia shilingi bilioni 640. Leo hii tunazungumza hapa ni karibu shilingi trilioni 1.2. Mnaweza kuona dhamira ya kweli ya Mheshimiwa Rais ya kutaka kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya maji, lakini tunafahamu kwamba changamoto za Maji ni kubwa sana katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Mheshimiwa Waziri alivyosoma asubuhi, ameonesha mikakati mbalimbali hasa kwenye maeneo makuu, iko miradi ambayo wakati Waziri wangu anasoma asubuhi, imeonesha ilianzishwa tangu miaka ya 1970. Nikisoma mojawapo, kwa mfano ule wa Orkesument ulianzishwa mwaka 1977, na aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Marehemu Sokoine, ukawa umesimama. Rais wetu akaja akauibua; lakini nikiangalia ule mmoja wa kutoka Musoma - Kiabakari, kuja huku Butiama, ule ulikuwa ni mradi ulioanzishwa ili kupeleka maji kwa Mwalimu Nyerere. Ulikuwa ni moja ya miradi saba ya kimkakati katika nchi hii. Daktari Samia amekuja kukwamua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokwenda kule Same, Mwanga, Waziri wangu pia alisoma, miaka karibu 19 mradi ulikuwa umelala na Mheshimiwa Marehemu Cleopa Msuya, moja ya vilio vyake vikubwa ilikuwa ni kutaka watu wake wapate maji. Tunamshukuru Mungu kabla hajalala, alienda kushuhudia mradi huo ukizinduliwa, na mimi nilibahatika kuambatana na Waziri wangu, sawa amekuwa akinialika mara nyingi kuambatana naye kukagua miradi, nilijionea mkakati mkubwa wa Kiserikali ambao unalenga kwenda kutatua changamoto za Watanzania. (Makofi)
Kwa hiyo ninapongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na nia yake ya ukweli ambayo imedhihirika katika matendo. Tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo makubwa ambayo yamefanyika, ninaishukuru Serikali kwa kuwa na mpango wa kabambe wa kitaifa wa maji. Kwa nini tunaishukuru Serikali? Unajua maji yameendelea kupungua sana duniani. Nilikuwa kwenye mkutano wiki iliyopita Misri, tulikuwa tunazungumzia idadi ya watu na maendeleo. Moja ya changamoto kubwa ambazo kila Mbunge aliizungumza pale, ongezeko la watu kwa Afrika linasababisha umaskini, lakini pia limesababisha matatizo makubwa ya maji. Inakusudiwa kwamba watu zaidi ya milioni 20 sasa wanahamahama kwa sababu ya kukosa maji. Ndio maana Serikali yetu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ikaona ni muhimu kuhakikisha kwamba tunaleta mpango wa kabambe ili maji yaweze kusimamiwa, maji yaweze kugawanywa kwa mpangilio. Maji kiasi gani yanakwenda kwenye kilimo? Maji kiasi gani yanakwenda kwenye mifugo? Maji kiasi gani tunakwenda kutumia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali na wenzangu, tuunge mkono hoja hii, kwa sababu tusipounga mkono, tukawa na matumizi holela ya maji, tutaanza kupata matatizo makubwa. Mbunge mmoja kutoka Uganda, akasema kwamba kwenye jimbo lake la Karamojong watu zaidi ya 2000 wamekuwa wakifa kwa sababu ya kukosa chakula ambacho kinatokana na uhaba wa maji. Kwa hiyo, mnaweza kuona suala la Maji ni suala mtambuka. Kwa hiyo ni lazima tuunge mkono Serikali katika mipango yake ya kuhakikisha tunasimamia na kudhibiti matumizi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sambamba na hilo, ulinzi kwenye vyanzo vya maji ni suala ambalo halihitaji kufanyiwa michezo wa aina yoyote na ndugu zangu Watanzania tunafahamu, mito mingi imeendelea kukauka, kwa hiyo watu wengi wameendelea kusogea sogea kwenye vyanzo vya maji kwa kisingizio cha kutafuta mahali pa kulima. Jambo hili halitaweza kukubalika na Serikali isiruhusu kwa sababu ya furaha ya muda mfupi kwamba mtu atalima apate mwaka huu, miaka mitano ijayo Watanzania wakose maji, hilo halitawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo sasa, tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inaongezea nguvu haya mabonde yetu ili yafanye kazi ya kuhifadhi vyanzo vya maji kwa maana tuwape uwezo wa vitendea kazi, uwezo wa rasilimali watu (watumishi) ili kuhakikisha kwamba vyanzo vinalindwa, lakini suala la kulinda vyanzo vya maji siyo la Wizara ya Maji peke yake, ni la Watanzania wote na mimi ninatamani kwamba jambo hili wakati mwingine hata kwenye vyombo vyetu vya dini, kwa mfano makanisa na misikiti iwe ni suala la imani ili hata huko lisemwe watu liwaingie ndani kwa sababu tukicheza nalo dunia inakokwenda siko. Inakadiriwa ifikapo mwaka 2050 zaidi ya watu milioni 140 watakuwa wakihamahama kuhangaika kutafuta maji. Kwa hiyo, sisi tuanze kujiandaa mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezumgumzwa habari ya upotevu wa maji, hata Waziri wangu alisoma katika taarifa yake. Suala la upotevu wa maji lina sababu nyingi; kwanza, uchakavu wa miundombinu. Upo uchakavu wa miundombinu lakini maeneo mengine pia wizi wa maji unaofanywa na baadhi ya watumishi ambao siyo waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye eneo hilo la uchakavu, miradi yetu mingi ilijengwa zamani. Ni kweli tumebakiza vijiji 1,575 lakini huko nyuma tulikotoka bado tunakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya zamani, ndiyo maana pamoja na fedha nyingi ambazo Rais wetu ametupatia, zaidi ya shilingi trilioni moja, utashangaa kwa nini Kamati inasema tuongezewe fedha, mbona hawa watu wanatamaa sana? Hapana, ni kwa sababu miradi mingi ya zamani mabomba yake yamechakaa, lakini watu wameongezeka. Unakuta eneo lilijengwa wakati kijiji kina watu 5,000 saa hizi kijiji kina watu 12,000. Kwa hiyo, unaweza ukaona watu wameongezeka mahitaji yanazidi kuwa makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Serikali iendelee kutuunga mkono tunaposema tunahitaji kuendelea kuboresha huduma ya maji na tunahitaji bajeti, hizo ndizo sababu. Waziri wangu ameeleza hapa, tuna changamoto pia ya maji katika majiji makubwa. Ameeleza Dodoma, sasa mahitaji kwa siku ni milioni 150, sasa tunazalisha karibu milioni 85.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi ambao utatuletea karibu lita milioni 15 huu wa Nzuguni wa shilingi bilioni 5.5 lakini bado mahitaji ni makubwa katika Jiji la Dodoma pamoja na juhudi zote.
Kwa hiyo, tuiombe pia Serikali tuendelee kuangalia katika majiji makubwa yenye sura zile za kimataifa; Dodoma, Dar es Salaam na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, pengine kwenye gridi ya maji, tunaipongeza Serikali kwa kuanzisha hii gridi ya maji...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)