Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu kwenye bajeti hii muhimu kwa Watanzania, bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye kwa neema yake na rehema yake ametujalia na ametuwezesha tumendelea kuwepo kwenye nyumba hii kuifanya kazi ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi yetu. Yako mambo mengi ambayo ni ushahidi wa kazi kubwa na nzuri anayoifanya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye eneo la maji, niseme eneo moja tu. Mwaka wa fedha 2020/2021 bajeti ya maji ilikuwa ni shilingi bilioni 697.5; leo tunazugumza hotuba aliyosoma Mheshimiwa Waziri analiomba Bunge limwidhinishie fedha shilingi trilioni 1.12, ni ongezeko kubwa sana la fedha kwa upande wa Wizara ya Maji. Jambo hili pekee yake linaweza kutosha kuwa ushahidi wa kazi nzuri na nia na mapenzi makubwa aliyonayo Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania wa nchi hii. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji, kaka yangu Mheshimiwa Jumaa Aweso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso amekuwa miongoni mwa Mawaziri wasikivu, anayeifanya kwa dhati kazi ya Watanzania akizunguka maeneo yote ya nchi hii. Tumemwona yeye na timu yake, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, lakini na wataalamu wao kule Wizarani wakiwemo Wakurugenzi lakini pia Mkurugenzi wa RUWASA kwa sisi wa vijijini wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, kazi hii nzuri unayoifanya haihitaji jambo lingine zaidi ya kuungwa mkono na niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuipitishe bajeti ya Wizara ya Maji ili watu wa Wizara ya Maji wakaendelee kufanya kazi ya kuwapa huduma ya maji Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka ushahidi wa kitakwimu upo; mwaka 2006 vijiji vilivyokuwa na huduma ya maji vilikuwa ni vijiji 3,000; leo tunapozungumza vijiji vilivyofikiwa na huduma ya maji ni vijiji 10,758, bado vijiji 1,575. Mwaka 2006 hali ya upatikanaji wa maji kwa sisi wa vijijini ilikuwa 50%. Mpaka Desemba 2025 hali ya upatikanaji wa maji kwa eneo la vijijini ni 85.2%, lakini kwa upande wa mijini hali ya upatikanaji wa maji mwaka 2006 ilikuwa 73%; leo tunazungumza hali ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini mpaka Desemba, 2025 ni 92.5%. Takwimu hazidanganyi, kazi iliyofanyika ni kubwa. Tunawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimetoa takwimu za kitaifa, lakini pia nitakupa takwimu za ndugu zangu wa Wana-Korogwe Vijijini. Mwaka 2006 katika vijiji 118 vya Korogwe Vijijini tulikuwa na huduma ya maji imefika kwenye vijiji 31 tu, leo tunapozungumza Korogwe Vijijini katika vijiji 118, vijiji 93 vinapata huduma ya maji bado vijiji 25 na katika hivi vijiji 25 vijiji 16 kuna miradi inaendelea, bado vijiji tisa ambavyo nimeviona kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunawapongeza sana, tunawashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya. Ombi langu tu peleka fedha kule Korogwe tumalizie miradi iliyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani na pongezi nyingi nilizozitoa kwa Serikali na kwa Wizara, ninao ushauri kwenye maeneo kama manne hivi. Eneo la kwanza, pamoja na kazi nzuri wanayofanya watu wa Wizara ya Maji, tunakubaliana sote hali ya upatikanaji na upelekaji wa fedha bado siyo ya kuridhisha. Tunaiomba Serikali iendelee kutoa fedha ili miradi ambayo inawakandarasi wako kazini iweze kufanyika na iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee lazima tukubaliane vyanzo vya fedha tulivyonavyo kwa ajili ya shughuli za kupeleka huduma za maji vimeelemewa, kazi inayohitajika kufanyika ni kubwa na chanzo ni kidogo. Tuiombe Serikali, ni wakati sahihi wa kufikiri namna gani ya kuongeza vyanzo vya fedha ili tuongeze fedha kuwapelekea watu wa maji ili waendelee kufanya kazi hii nzuri kwa ajili ya kuwaletea huduma Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa nishauri, Mheshimiwa Waziri ninakushauri wewe na wenzako kwenye Wizara; ni kwenye eneo la uvunaji na uhifadhi wa maji. Lipo jambo la aibu ambalo lazima Mheshimiwa Waziri ukubali kumsaidia Dkt. Samia Suluhu Hassan aibu hiyo iondoke isitirudie tena. Haiwezekani nchi hii nzuri ambayo Mungu ametubariki wakati wa mvua tunalia na mafuriko, mvua ikikatika siku tatu tunalia na ukame watu hawapati huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukubaliane iko haja ya kufanya kazi kubwa ya kutafuta namna ya kuhifadhi maji ya mvua kwa sababu nchi yetu imebarikiwa kuwa na mvua nyingi na tunapata maji mengi. Leo tunapata mvua tunapata mafuriko, lakini siku tatu tunaanza kuhangaika ukame. Haiwezekani. Nimeona mmeanza kufanya kazi Bwawa la Kidunda, nimeona mmesema kuhusu Bwawa la Farkwa. Mheshimiwa Waziri nendeni mkatengeneze miradi ya kimkakati ya mabwawa. Tuwe na uwezo wa kuwa na mabwawa makubwa kwenye mabonde yote, tuhifadhi maji ili yasaidie vyanzo vingine tulivyokuwa navyo na Watanzania waendelee kupata maji tusirudi kwenye changamoto ya ukame kama ambayo imekuwa ikitusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ninaomba nimshauri Mheshimiwa Waziri ni eneo la usimamizi na uendelevu wa miradi ya maji hasa kwenye maeneo ya vijijini. Kwa historia huko nyuma tulikotoka maeneo yetu ya vijijini miradi ya maji ilikuwa ni mali ya vijiji na wananchi walikuwa wanaisimamia na walikuwa wanaitumia wenyewe kadiri wanavyoona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuja Bungeni hapa mwaka 2012 tukapitisha Sheria ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Sheria Namba Tano ya mwaka 2019. Kwenye sheria ile Mheshimiwa Waziri tulianzisha vyombo vya watumiaji maji (CBWSOs) na lengo lake ni kusimamia miradi ya maji ili wananchi hawa wasimamie miradi ya maji iwe endelevu na ndiyo maana pia kuna kazi ya kuchangia, kwamba wananchi wanatakiwa kuchangia fedha ili kuendesha miradi hii iendelee kuwa endelevu.

Mheshimiwa Waziri, ninakushauri ili vyombo vya watumiaji maji (CBWSOs) viweze kufanya kazi zake vizuri na miradi iwe endelevu isimamie vizuri hata ikiharibika waweze kukarabati ni lazima wawe na fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi waweze kuchangia lazima wawe na imani na vyombo hivyo. Mheshimiwa Waziri tuipitie upya sheria ile, sheria namba tano ya mwaka 2019, tukarekebishe ile composition ya wale members wa kile chombo cha watumiaji maji. Tuongeze ushiriki wa wananchi kwenye vyombo vile ili tuwafanye wananchi wetu vijijini wajione kuwa ni sehemu ya vyombo vile na waone vyombo vile ni vya kwao ili wawe na moyo wa kuvitumikia, waweze kuchangia fedha na waweze kusimamia miradi ya maji na mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninamshauri Mheshimiwa Waziri ni eneo la uhifadhi wa mazingira. Mara nyingi tumekuwa tukiacha kazi ya uhifadhi wa mazingira kama kazi ya kufanywa na wenzetu Ofisi ya Makamu wa Rais peke yake, jambo hili siyo sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaongezeka, ardhi yetu haiongezeki na mahitaji ya maji yanaendelea kuongezeka. Ni lazima tujitahidi kuwa na mikakati ya kutosha ya utunzaji wa vyanzo ya maji. Leo wenzetu wa Dar es Salaam kwa mfano, wanategemea Mto Ruvu na tunaweka nguvu kubwa sana kusimamia Mto Ruvu na kuna wakati tunajisahau pia tunausimamia zaidi wakati wa ukame tukiona maji yamepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ushauri wangu kwa Serikali, kazi hii Wizara ya Maji mshiriki na msaidie kuifanya vizuri na tusiishie kwenye kusimamia peke yake mito hii mikubwa, tukasimamie pia na mito midogo inayolisha hii mito mikubwa ili mito mikubwa hii tuipunguzie changamoto ya upungufu wa maji na iweze kuwahudumia watu wakati wote hata wakati wa kiangazi iweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ninaloomba nimshauri Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri tumeona katikati hapa wenzetu wa Dar es Salaam walipata changamoto, na ninyi mnajua Dar es Salaam ni uso wa nchi yetu, hata mimi wa Korogwe, Dar es Salaam inanigusa. Tuliona changamoto ilipotokea maneno yalikuwa mengi na kelele zilikuwa nyingi. Niwapongeze mlimasimama imara, mliifanya kazi kwa wakati mkarudisha huduma kwenye maeneo mengi ya mji wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kipekee niwapongeze wenzetu wa Mamlaka ya Maji Dar es Salaam chini ya usimamizi wa mtendaji wake Engineer Bwire. Engineer Bwire tulikuwa naye RUWASA sisi wa vijijini tunamjua. Tunaamini ni mtu mwema na anajua kufanya kazi yake vizuri na kwa kweli kazi aliyoifanya Dar es Salaam inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako umetwambia moja ya suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa maji Dar es Salaam ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Mimi ninakubaliana na wewe na ninaipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda ambayo mnaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mdogo tu, mambo haya yanapaswa kwenda pamoja. Wakati mnajenga Bwawa la Kidunda tafuteni fedha wapeni wenzetu wa Mamlaka ya Maji Dar es Salaam mkafanye upanuzi wa treatment plant ili wakati Bwawa la Kidunda linakamilika na mtambo wa kusafisha maji mkafanya expansiyon unalingana na ukubwa wa kazi ambayo inakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukaongeza ujazo wa maji lakini mtambo wa usafishaji wa maji bado ni ule ule ambao tuliu-design miaka mingi nyuma iliyopita. Ninajua inahitajika fedha nyingi lakini vizuri tuanze kutenga kidogo kidogo ili mambo haya yaende pamoja ili changamoto ya maji kwenye miji kama Dar es Salaam iweze kufikia mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri tuna miradi mingi inaendelea kule Korogwe ile 16 kuna mingine michache wakandarasi wangu wanadai, wapelekeeni fedha wamalize kazi watu wa Korogwe wapate maji. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante muda wako umeisha.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TIMOTHEO P. MZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana ninaunga mkono hoja. (Makofi)