Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JESCA Y. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Wizara hii nyeti, lakini awali ya yote ninaomba kwanza nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi hasa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua na kuweza kunipa ridhaa ya kwenda kwa wanawake kunipigia kura za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa kunipa kura nyingi za kishindo. Imani waliyonipatia nitakwenda kuilinda kwa kufanya kazi kwa bidii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza ninapenda nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa sana aliyoyafanya Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dodoma sote hapa ni mashahidi; Dodoma ile siyo Dodoma hii. Kama nyumba mama ameipamba kweli kweli. Tunampongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miundobinu mizuri Mkoani Dodoma. Sisi Wana-Dodoma tunamwombea sana mama yetu kwa kazi nyingi ambazo amezifanya Mkoa wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niipongeze Wizara hii ya Maji. Wizara ya Maji Dodoma kwa kweli wanatutendea haki. Wanafanya kazi kubwa, kubwa sana, 70% sisi Dodoma sasa hivi tunatumia maji ya kutosha. Niwapongeze sana kwa mipango mizuri na nimemsikiliza vizuri hapa Mheshimiwa Waziri wakati anaeleza asubuhi, ana mipango mpaka akawa anani-pre-empty. Kila anachokieleza ninakiona kwamba sasa ninaenda kuzungumza nini, Mheshimiwa kashafanya kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana kwa kazi nzuri na maono makubwa ambayo mmejipanga nayo kama Wizara. Tunawapongeza sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Asia Halamga.
TAARIFA
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumpa taarifa Mheshimiwa Jesca.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca tafadhali ukae wakati unapewa Taarifa.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumwongezea tu taarifa Mheshimiwa Jesca kwamba Wizara hii inafanya vizuri kwa ngazi ya Wizara na mikoani. Hata mimi mfano nina meneja wa mkoa ambaye ni mzuri sana, Ndugu yangu James, lakini pia meneja wangu wa wilaya ya Hanang. Mheshimiwa Waziri hongera sana kwa kuwasimamia watendaji wa chini. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. JESCA Y. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri ambayo yanafanywa na Wizara, lakini zipo changamoto kwenye Mkoa wetu wa Dodoma. Nikianzia hapa Dodoma Jiji uhaba wa vyanzo vya maji; jiji linakuwa, watu wanaongezeka. Mwaka 2022 takwimu zinaonesha kwamba watu walikuwa 3,000,000 lakini mpaka sasa wanaendelea kuongezeka, vyanzo vya maji viko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara sasa ijikite kwenye kuongeza vyanzo vya maji. Hii inasababisha mgao unakuwa mkali sana Dodoma.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. JESCA Y. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ulinde muda wangu.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Taarifa.
TAARIFA
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa ninaomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba; hotuba ya leo imeeleza hii National Grid inatoka Ziwa Victoria inakuja mpaka Dodoma. Ni hilo tu, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa ni Taarifa ya mwisho. Tunao Waheshimiwa Wabunge 80 wameomba kuchangia. Tusipozingatia muda maana yake tutawanyima nafasi Wabunge wengine.
Ninaomba Waheshimiwa Wabunge kengele ya pili ikigonga ujue muda wako umeisha ili tumpishe mchangiaji anayefuata. (Makofi)
Endelea Mheshimiwa Jesca.
MHE. JESCA Y. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na mzungumzaji kwamba ni kweli mradi huo utafika, lakini wakati tunajiandaa na mradi huo bado Wizara inayo nafasi ya kuongeza vyanzo hivyo kutokana na population ya watu inayoongezeka kwa sababu hii inasababisha mgao mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Chidachi, Chamwino hapo Chang'ombe watu wanapata maji kwa wiki mara moja na hii ni kwa sababu population ni kubwa, lakini vyanzo vya maji bado viko chini.
Kwa ushauri wangu, pamoja na kwamba mambo mazuri yote yanakuja, lakini bado Wizara inapaswa kuongeza vyanzo hivi vya maji kwenye Jiji letu la Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nielezee sasa juu ya maji vijijini. Mkoa wa Dodoma ikifika mwezi Juni, mwezi Julai wanawake vijijini wanapata shida sana ya maji. Kunakuwa kuna ukame mzito wa maji. Hata hivyo, tunashukuru sana Wizara imeweka matanki kule mazuri sana. Matanki mengine yana volt mpaka 500, 200, ni makubwa lakini wakati mwingine unakuta hayana usimamizi mzuri, umeme hautoshi. Kwa hiyo, wanawake wanajikuta wanaenda kuchimba maji chini. Sisi Wagogo tunaita masombolwa. Wanayachimba chini yale maji ili waweze kuyatumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu, ninaomba sana vijijini wapazingatie sana. Nimemsikiliza vizuri sana Waziri, alieleza vizuri juu ya mipango iliyopo vijijini, lakini ninaendelea kusisitiza wanawake wa vijijini hasa Mkoa wetu wa Dodoma wanapata shida sana ya maji. Kama ni matanki yanawekwa au visima vinachimbwa basi tuhakikishe na miundobinu yake ya maji inakaa sawasawa. Kwa mfano, tunapochimba hivyo visima au tunaweka matanki basi tuhakikishe miundobinu ya umeme, miundobinu ya mabomba inakaa vizuri ili kuhakikisha kwamba mwanamke wa kijijini anapata maji kama vile mwingine wa mjini anavyopata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ni uhaba wa vitendea kazi. Tunao watu wa RUWASA, utakuta una vitendea kazi kwa mfano magari bado havikidhi mahitaji ya watumishi kule kwenye wilaya zetu. RUWASA, Kongwa pale wana gari kuanzia mwaka 2010 mpaka leo ni gari moja. Wakiambiwa waende kutembelea miradi ya maji wanashindwa.
Kwa hiyo, ninaomba wizara hii kupitia bajeti hii wawakumbuke RUWASA na DUWASA katika vitendea kazi kama magari na pikipiki ili iweze kurahisisha upatikanaji wa huduma za maji kule wanakokwenda kuziangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja bajeti hii. Ahsante sana. (Makofi)