Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kunipa nafasi hii ili na mimi nitoe mchango wangu kwa Wizara ya Maji chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Aweso na Naibu wake Engineer Kundo na timu nzima ambayo inamsaidia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ya shilingi trilioni 1.12 ikisimamiwa vizuri italeta mapinduzi makubwa sana kwa upande wa huduma za maji. Hii inadhihirisha kwamba Mheshimiwa Rais zile kauli zake za kumtua mama ndoo kichwani hataki ziwe maneno matupu, anataka ziunganishwe na vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemwona Mheshimiwa Waziri na Naibu wake namna ambavyo wanahangaika katika ziara mbalimbali. Ni rai yangu kwamba speed hiyo ingerithiwa na viongozi wote wa mikoa kuhakikisha kwamba wanajua maeneo yao, wanajua historia za maji, upungufu wa maji na namna ya kutatua. Hii itasababisha utendaji wao uumane kama timu ya mpira wa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uzoefu wangu wa humu ndani hakuna siku ambayo Wizara ya Maji inakosa swali. Kila siku Wizara ya Maji utakuta inaulizwa swali hapa. Kwa hiyo, maana yake ni Waheshimiwa Wabunge michango wanayoitoa ni michango muhimu inayopaswa kuzingatiwa na Wizara ili iweze kusaidia kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anazungumza hapa amezungumzia habari ya magari. Magari yaliyonunuliwa na Serikali bado mapya na amesema kwamba sasa hivi anawaagiza watendaji wake waondoe gharama zisizokuwa za lazima ili kuyafanya magari haya hata sisi Wabunge tuweze kuyatumia kwa kutumia pesa kidogo ya Mfuko wa Jimbo tuweze kuchimba visima vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni la muhimu sana na mimi ninakuomba Mheshimiwa Waziri, mimi nilishawahi nimeshatenga tayari shilingi milioni 15 ya mafuta, nipatie gari na milioni 15 za Mfuko wa Jimbo tukachimbe katika Kijiji cha Chinugulu ambako Mheshimiwa Rais aliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri apitie ziara nzima ya kampeni ya Mheshimiwa Rais, mahali pote ambako Rais aliahidi maji tuweke kipaumbele, tumalize hizi ahadi za kiongozi wetu, kuliko kila ukifanya ziara utakutana na swali hilo. Unaulizwa Mheshimiwa Rais aliahidi, tuondoe hivi vitu kwa kutumia hiyo ya kutupa magari, sisi tutie mafuta tuchimbe maji yapatikane wananchi waendelee kutumia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo lingine la kuzungumza hapa. Kuchelewa kukamilika kwa miradi kunaongeza gharama, kwa mfano, tuna mradi wa Kata ya Handali. Mradi ulikuwa umetengewa zaidi ya shilingi milioni 600 lakini ukienda sasa kutokana na vita ya Iran na Israel na Marekani utakuta gharama zimepanda na mradi ulikuwa ukamilike kabla hata ya vita. Sasa tuangalie ni miradi mingapi katika Taifa ambayo imecheleweshwa na mpaka sasa hivi gharama zake zinakuwa maradufu. Huko Mheshimiwa Waziri nenda uwake ili watendaji wetu wafanye kazi kwa speed miradi yote iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe, ukiangalia namna ambavyo TANESCO wanafanya kazi, ukiangalia namna ambavyo TARURA wanafanya kazi, ukiangalia namna ambavyo Zimamoto wanafanya kazi, tunawapongeza ma-MD wengi wa mikoa wanachakalika, lakini nikuombe wale ambao bado wazembe wazembe wa wilaya na baadhi ya mikoa ambao unawaona peleka JKT. Mpe Nyansaho hapo akawapige miezi mitatu wakitoka huko watakuwa na morali wa kufanya kazi ya miradi ya maji kama jeshi. Hii itatusaidia kukimbiza maendeleo ya huduma za kwenye wilaya kuliko maji yaonekane yamedorola katika utendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazidi kusisitiza kwamba kwenye maeneo tunayopeleka miradi mipya tutumie kitabu cha sensa. Kitabu cha sensa kitatuonesha idadi ya watu wa eneo husika. Kwa hiyo, tutajenga matanki makubwa kulingana na eneo husika. Kwa mfano, idadi ya watu wa Tarafa ya Mpwayungu unaangalia Kata ya Manda ina watu wangapi, 19,000. Watu 19,000 unahitaji ujenge tanki kubwa kiasi gani ambalo linaweza kuwafaa wale watu? Ukija hivyo hivyo unakuta kuna Kata ya Mlowa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenzenu wa vijijini ni tofauti na wa mijini, wa mijini wanazungumzia population kubwa kwenye maeneo yao. Sisi majiji yetu kule Wabunge wa vijijini ni makao makuu ya tarafa, makao makuu ya kata zenye watu wengi. Sisi ndiyo majiji yetu ambayo tunataka yajengwe matenki makubwa na yale ya zamani madogo yakiunganishwa yatatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka sasa hivi sera ibadilike, badala ya kujenga tanki la lita 90,000 sasa tujenge matanki ya lita 300,000 kwenye kata zenye watu wengi. Tukifanya namna hiyo tunaondoa usumbufu kabisa kwenye maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaomba nimshauri Mheshimiwa Waziri; ushirikishwaji wa kuunganisha kata na kata kwenye Miradi ya RUWASA, kuna baadhi ya maeneo haukuwa mzuri. Tumeunga kata A na B na C, kata moja haina huduma ya maji kabisa. Sasa matokeo yake wenzao wananufaika na maji, wao hawapati maji lakini wako kwenye mradi mmoja. Hii inakuwa siyo sawa. Tungeomba Madiwani washirikishwe. Je, historia ya kata hii inaweza kuungana na kata hii katika mradi wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkifanya hivyo mtaunganisha watu ambao wamezoea kuishi pamoja kuliko unaichukua kata B ambayo iko mbali, tamaduni yake na kata A iko tofauti unawaweka wote chini ya mradi mmoja wa maji. Hii inakuwa haiwezekani, unakuwa umeleta kero badala ya kuondoa tatizo kwenye eneo lile.

Kwa hiyo, tunaomba sana ushirikishwaji wa wananchi na hasa Waheshimiwa Madiwani ili wajue kata yako inaungwa na kata fulani, kijiji fulani tunakiunga na kijiji fulani kwenye mradi mmoja wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ya msingi sana ambayo nilitaka niyazungumze, lakini jambo moja la muhimu sana, mita za maji. Tumesema tunaleta mita za kidigitali. Ni jambo zuri kuwa na mita za kidigitali, lakini mita zenyewe zipimwe na Mamlaka ya Vipimo ya Taifa ili tuwe na uhakika kwamba mita hizo nazo hazitatuletea bili za uongo. Kwa sababu hivi vyombo ni vya kidigitali vinaweza vikakataa vile vile. Unaiona mita nzuri lakini vilevile ikaleta mahesabu tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kengele ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana sasa Mheshimiwa Waziri, kabla ya kumaliza Bunge twende tufanye ziara tumalize matatizo ya Mradi wa Maji wa Handali, tumalize tufungue Mradi wa Maji wa Mvumi Missiyon, tumalize tufungue Mradi wa Maji wa Manda, twende tuangalie kujenga matanki makubwa katika Kata ya Mpwayungu na baada ya hapo tuvitembelee vijiji ambavyo vina maji ya chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivyo tulishamwomba Mheshimiwa Rais na wewe ulikuwepo kwenye ziara. Mheshimiwa Rais akasema siyo lazima maji yatumike ya pale Manzase. Tunaweza tukachukua maji sehemu nyingine tukawapelekea watu wa Manzase wakapata maji safi na salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo ninaunga mkono hoja. Mungu awabariki sana. (Makofi)