Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye amenipa kibali na mimi kuwa mchangiaji kwenye bajeti yetu hii ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninatumia fursa hii kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo anaendelea kuweka nguvu zake kubwa kuwatumikia Watanzania hususani katika suala la utoaji wa fedha nyingi kwenye Wizara yetu ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninatumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Jumaa Aweso pamoja na Naibu wake. Kazi yao ni nzuri na kama kuitendea haki Wizara hii wanaitendea haki na wanastahili pongezi za dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wa Maji, nina imani Watanzania wengi wanamwombea, pamoja na kwamba anaombewa na Watanzania wengi, ninaomba aamini ya kwamba Mkoa wa Mwanza kwenye Jimbo la Nyamagana ndiyo Watanzania wanaoongoza kumwombea ili ahakikishe kazi aliyoianza kwenye Jimbo la Nyamagana inakamilika kama ambavyo imepangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti nimepata fursa ya kuisoma bajeti ya Wizara ya Maji na nimepata fursa ya kusikiliza wasilisho la Wizara hii ya Maji. Ninataka niseme ukweli, kama yale ambayo Mheshimiwa Jumaa Aweso ameyaweka kwenye bajeti hii yakitekelezeka. Ninataka niseme ukweli mbele za Mwenyezi Mungu kwa miaka mitano ijayo hali ya upatikanaji wa maji kwenye nchi yetu itakuwa imeboreka kwa asilimia kubwa sana tofauti na sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu ambao nimeusoma, yapo mambo ambayo binafsi mimi yamenigusa sana. Wizara ya Maji imekuja na mpango wa kuanzisha National Water Master Plan. Wizara ya Maji katika hili ninataka nitumie fursa hii kuipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utekelezaji wa plan hii ukifanyika kikamilifu, itatusaidia kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu, itatusaidia kukabiliana na ukuaji wa miji, lakini zaidi ya yote itatusaidia kwenye suala la maendeleo ya viwanda, kilimo pamoja na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili la master plan, nataka kumshauri sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, yamekuwepo manung’uniko ya muda mrefu ya Watanzania juu ya wananchi watumiaji wa maji kubambikiwa bill. Unakuta mwananchi hajatumia maji mwezi mzima lakini bill inakuja kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni shuhuda kwenye Jimbo langu la Nyamagana, kuna Watanzania wengi wenye malalamiko haya. Nakuomba sana kaka yangu Mheshimiwa Aweso, lichukue jambo hili kwa umuhimu wake, Watanzania wanahitaji haki katika kuhudumiwa na hili linaenda sambamba pamoja na suala la huduma kwa wateja. Kaka yangu Mheshimiwa Aweso nakuomba, kujifunza na kuiga mambo mazuri si dhambi, igeni kwa wenzetu wa TANESCO. Wenzetu wa TANESCO kwenye suala la huduma kwa wateja wako vizuri sana. Wao wanakutaarifu umeme kesho utakatika muda fulani, lakini Wizara ya Maji kidogo hapa hamjafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake inatokea Watanzania wakiamini kesho kuna maji yanakatika, tunawatoa kwenye reli. Kwa hiyo, nataka kukuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, yachukue haya mambo mawili ili tuweze kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge mwenzangu amezungumzia kuhusu mita hapa, na mimi nataka kukuomba, umuhimu wa mita za pre-paid, unalipia kabla ya kutumia ndiyo wakati wake muafaka kwa sasa. Mkifanya hivyo kwa haraka, tutasaidia Mtanzania alipie kwa anavyohitaji kutumia yeye na malalamiko ya kubambikiziwa bill hayatakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelekea mwishoni, nataka kumwambia Mheshimiwa Aweso, Jimbo langu la Nyamagana na Jiji la Mwanza, limezungumzwa Ziwa Victoria hapa. Kwenye Jimbo langu la Nyamagana ndipo liko Ziwa Victoria kwa ukubwa kuliko popote pale, lakini namna ambavyo wananchi wangu kwenye Jimbo la Nyamagana kwa miaka ya nyuma walivyokuwa wanaiona, walikuwa wanaifananisha na Mkoa wa Shinyanga ambao ulikuwa unaongoza kwa uchimbaji wa dhahabu, lakini ulikuwa ni mkoa maskini kuliko yote Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nyamagana, natolea mfano kwenye Mtaa wa Kisoko pale Lucherere, Mtaa wa Kisoko pale Lucherere kutoka ziwani haifiki hata meta 500. Tunavyozungumza, wananchi wa Mtaa wa Kisoko hawana maji. Nataka kumwomba sana Mheshimiwa Aweso kwa sababu nina imani naye kubwa sana, unapoenda ku-windup natamani wananchi hawa wakazi wa Jimbo la Nyamagana wapate matumaini kwa kile ambacho unaenda kuahidi utakwenda kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wanasema: “Asiyeshukuru kwa kidogo, hata akipewa kikubwa hawezi kushukuru.” Ninataka kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na msaidizi wake Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu wake, ndani ya kipindi cha miaka mitano Jimbo la Nyamagana, Mheshimiwa Dkt. Samia ameleta zaidi ya shilingi bilioni 140 ambazo zimehudumia miradi mbalimbali ya maji kwenye Jimbo la Nyamagana. Mwaka jana mwezi Machi Mheshimiwa Dkt. Samia alikuja kuzindua mradi wa chanzo cha maji pale Butimba wenye zaidi ya thamani ya shilingi bilioni 71 fedha za Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nilizungumza na kaka yangu Mheshimiwa Aweso, wananchi wa Nyamagana walikuwa wanalalamika, pamoja na chanzo hicho kukamilika, lakini hawakuwa na maji kwenye maeneo yao. Mheshimiwa Dkt. Samia kupitia kwa kaka yangu Mheshimiwa Aweso akaridhia, wametuletea shilingi bilioni 46 za ujenzi wa matanki makubwa matano kwenye Mkoa wetu wa Mwanza na kwa Nyamagana peke yake tunayo matanki matatu. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia kwa sababu yale aliyoyaahidi, Wanamwanza wanayaona sasa yanakwenda kutimia kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa matanki haya niliwahi kumwambia Mheshimiwa Aweso, malalamiko Nyamagana suala la maji bado yapo kwa sababu matanki yatakamilika lakini wananchi wanahitaji kuyaona maji kwenye maeneo yao…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako…
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na siyo kuyaona kwenye matanki…
MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika moja ninapohitimisha…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapohitimisha, nasema tu kwamba naunga mkono hoja, lakini kwa kaka yangu Mheshimiwa Aweso ingetokea mashindano ya dunia…