Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Paschal Inyasi Chinyele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)

Kwanza kabisa na mimi namshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijalia uhai, lakini pia sisi Wana-Dodoma tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hali nzuri ya hewa mwaka huu, kwa kweli chakula tunacho, mahindi tunayo, uwele tunao, tumeshiba mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi hii ya maji, limetajwa Bwawa la Kidunda, napajua pale Kidunda na Dar es Salaam nimekaa najua shida wanayoipata wakati wa kiangazi. Kwa hiyo Mradi huu wa Kidunda, Mheshimiwa Rais amewatendea haki sana Watanzania. Nasema tu, hizi hatua za Mheshimiwa Rais siyo za bure, hizi hatua za Mheshimiwa Rais zina mkono wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema, kwa ndugu zangu Wabunge ambao mlipata bahati ya kuwepo wakati Mheshimiwa Rais anaapishwa pale Dodoma, kwa aliyekuwepo kama kuna kitu alikiona, yangeyange wale ndege weupe wakati anajiandaa kuapa Mheshimiwa Rais, wale ndege walisimama juu na waliondoka baada ya Mheshimiwa Rais kumaliza kuapa. Kwa hiyo, hatua za Mheshimiwa Rais zina mkono wa Mungu wa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mimi namshukuru sana Mheshimiwa Aweso na Naibu Waziri wake kwa wasilisho zuri ambalo lina matumaini makubwa sana kwa Watanzania lakini pia na wakazi wa Dodoma Mjini kwa namna ya pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafarijika sana, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia na kuweka msisitizo kwa upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma na hii si bahati mbaya. Hawa Wabunge waliopo walio wengi ni wakazi wa hapa Dodoma na wengine ambao ni Wabunge wameingia karibuni, nina hakika ni wakazi watarajiwa wa Dodoma ndiyo maana wanasema sana kuhusiana na miradi hasa Mradi wa Nzuguni, Nala pamoja na Zuzu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tunavyoongea, mradi mkubwa, tuseme mtambo mkubwa wa maji kwa Dodoma ni Mzakwe ambao unatupa lita milioni 88 kwa siku mpaka sasa. Lakini hii Miradi ya Nzuguni, Nala pamoja na Zuzu ikikamilika, pamoja na huu wa Mzakwe kwa pamoja, itazalisha kwa siku lita milioni 127, lakini mwaka jana mwezi wa Mei tarehe kama ya jana, Dodoma ilikuwa inahitaji lita za maji milioni 143 lakini kwa sasa mwaka mmoja baadaye, tunahitaji lita milioni 159.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini, maana yake ni kwamba ongezeko la watu katika Jiji la Dodoma ni kubwa kuliko maji yanavyopatikana. Kwa hiyo, naomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, unajua kuna mradi huu wa Farkwa na nimefarijika sana kila wakati tukikutana unaniambia Mradi wa Farkwa unakaribia kusainiwa, mimi nashukuru sana. Pamoja na huu Mradi wa Ziwa Victoria, yote ni miradi ambayo kwa kweli sisi tunadhani itakuwa ni mkombozi kwetu. Kwa sababu kama nilivyosema, ongezeko la watu katika jiji letu ni kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hii miwili, naomba tu kushauri Mheshimiwa Waziri, pia sisi Dodoma tuna bahati kwamba maji yako jirani. Ukipiga chini meta 150 unapata maji, kuna vyanzo vingi navyo hivyo vitasaidia kwa sababu ongezeko la watu, lakini na pia nafahamu Serikali ina miradi mingi ya maji kwa hiyo fedha ni changamoto.

Sasa ili kwenda sambamba na hali hii, tunapendekeza vyanzo vingine vitafutwe, visima vya maji vya kutosha vichimbwe. Mheshimiwa Waziri, mimi Jimbo la Dodoma lina vijiji pia ingawa …. lakini lina vijiji ambavyo havina kabisa huduma ya maji ya RUWASA ama DUWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo miradi ya maji midogomidogo itakaposisitizwa, inaweza kutusaidia sana sisi watu wa Dodoma kuendelea kupata huduma nzuri ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Dodoma sisi vijana wetu walio wengi, ikishafikia mwezi wa tatu, wa nne mvua zinakuwa zimekoma, kwa hiyo, hawana cha kufanya. Tunaomba sana miradi hii ya maji, na ninaendelea kusisitiza mara kwa mara, yajengwe matanki katika maeneo ambayo vyanzo vya maji vipo. Sasa hivi kuna mipango ya kujenga matenki katika bvilima katika kata zetu mbalimbali, Kata za Mpunguzi, Matunguru na kadhalika. Yajengwe kwa kiasi kikubwa ili kuwasaidia vijana hawa kupata cha kufanya wakati wa kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mvua hawa vijana wanalima bustani, wanalima nyanya, wanalima vitunguu, wanalima hoho, lakini mvua zikishakata hawana cha kufanya tena, wanakuwa wanakaa mitaani wanakunywa na kufanya mambo mengine ambayo hayafai. Tafadhali Mheshimiwa Waziri tusaidie vijana wetu waweze kupata cha kufanya na hawa naongelea vijana wetu ambao kwa kweli hawakubahatika kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema pia kuhusiana na umuhimu wa kuwasaidia ndugu zangu wa Kata ya Mbalawala. Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikiongea na wewe mara kwa mara kuhusiana na wasiwasi walionao ndugu zangu wa Mbalawala pamoja na sehemu ya Nala kwamba eneo wanaloishi wanaambiwa ni Bonde la Mto Wami-Ruvu na hawaruhusiwi kuendeleza kwa namna yoyote maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa naongea sana hili jambo kwa sababu kwa kweli inauma, ukienda wakazi wale wapatao 12,000 kila wakati wanakuuliza Mheshimiwa Mbunge vipi mbona sisi haturuhusiwi kupima maeneo yetu, haturuhusiwi kujenga, haturuhusiwi kuwekeza chochote, tunaambiwa ni bonde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Mbalawala na Nala vilikuwa ni vijiji toka mwaka 1971, vilipimwa kihalali. Ninaomba Mheshimiwa Waziri tulishaongea, lakini naomba tutakapomaliza kipindi hiki cha bajeti uende Mbalawala mimi na wewe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. PASCHAL I. CHINYELE: ... ukawape majibu ndugu zangu wa Mbalawala na Nala ili waweze…