Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuchangia hotuba ya Waziri wa Maji.
Kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya na ajenda aliyonayo ya kumtua mama ndoo kichwani. Hakika Mheshimiwa Dkt. Samia ameyaishi maneno yake tangu akiwa Makamu wa Rais alisema mpango wake mkubwa ni kumtua ndoo mama kichwani na Mheshimiwa Dkt. Samia ameyaishi haya kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri katika Wilaya yetu ya Busega, mwaka 2021 upatikanaji wa maji safi na salama ulikuwa 30.9%, tunavyozungumza leo maji yanapatikana kwa 72.5%. hizi ni juhudi kubwa za Mheshimiwa Dkt. Samia kwa wananchi wa Tanzania na wananchi wa Busega. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Aweso, kwa kweli ndugu yangu Aweso unafanya kazi kubwa sana kwenye Wizara yako. Unanikumbusha kuna wine moja wanatengeneza watani zangu akina Mavunde, kadiri navyokaa siku nyingi, ndivyo inavyozidi kuwa sweet. Na wewe kadiri ulivyokaa siku nyingi kwenye Wizara ya Maji, ndivyo unazidi kufanya mambo makubwa na unazidi kuimarika kila siku. Nakupongeza sana kwa kazi kubwa unazofanya kwenye wizara yako ukisaidiana na Naibu Waziri Comrade Kundo pamoja na Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza Taarifa ya Kamati, lipo jambo moja Kamati wamezungumza kuhakikisha kwamba Wizara ya Maji inashirikiana na sekta nyingine katika Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Viwanda kuhakikisha kwamba wanafanya planning nzuri ya matumizi bora ya maji. Katika hili, ili tufanye vizuri katika suala zima la matumizi mazuri ya maji, lazima tukubaliane na mapendekezo ya Mheshimiwa Waziri ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na kitu kinachoitwa National Water Masterplan. Tukiwa na hicho kitu, ndicho kitu pekee kitakachotufanya tuwe na planning nzuri ya miradi tunayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi nini kinafanyika, tunakuwa na forces za mahitaji ya sasa. Mwananchi akitaka maji, Mheshimiwa Mbunge akisema maji, Mheshimiwa Mbunge akisema haya, tunafanya kwa sababu ndiyo mahitaji ya sasa lakini hatuna mahitaji, hatuna planning ya miaka 20, ya miaka 30 ijayo ambayo iko imeandikwa. Mimi naungana na wewe Mheshimiwa Waziri tuwe na National Water Masterplan na naomba Wizara ya Fedha wakupe fedha baada ya kuitisha bajeti yako ili tutengeneze National Water Masterplan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza tunapeleka sehemu kiwanda hamna maji, inashangaza tunapitisha sehemu barabara halafu baada ya miaka miwili tunasema hapa tunataka kuja kupitisha mabomba ya maji, tunabomoa barabara kwa kipindi tunapeleka maji. Tukiwa na masterplan ya maji, haya yote yatakuwa tayari yamekuwa yameelezwa kwenye National Water Masterplan. Tutajua vyanzo viko sehemu gani, tutajua hapa tutaweka kiwanda, tutajua hapa tutaweka mabwawa kwa ajili ya mifugo, tutajua kila kitu na zile wizara mtambuka mshirikiane kuhakikisha kwamba hili linaenda kufanyika vizuri ili miaka 50 ijayo, miaka 40 ijayo hata Mheshimiwa Profesa Kitila pale kashaleta habari ya Dira ya 2050, ni lazima sasa ili tuiishi, ni lazima sasa iwe accompanied na National Water Masterplan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono katika hili, fanya kazi, iandaeni na sisi, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tumpitishie bajeti Mheshimiwa Aweso kwa kishindo ili aende akatekeleze hili ambalo amelisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi mkubwa Mkoa wa Simiyu, mradi wa mabadiliko ya tabianchi, mpaka sasa uko katika 55%. Tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kufanya mahala hapa. Hakika sisi Wana-Simiyu tunachoomba mradi huu ukamilike kwa wakati, na ukikamilika kwa wakati kwa mfano pale kwangu Busega, wananchi wote watapata maji kwa 100% na tuna mabwawa mawili ambayo tayari yako kwenye phase ya pili ya mradi huu Bwawa la kule Rutubiga, Bwawa la kule Nyaruhande wananchi watatumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na wananchi watatumia kwa ajili ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa, tupeleke fedha kwa ajili ya miradi hii, mradi huu wa mabadiliko ya tabianchi ambao utakuwa pale Busega na kwa rafiki yangu Mheshimiwa Njalu, kule kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa Mheshimiwa Kadogosa mradi huu unapita. Ukikamilika kwa wakati, wananchi wanaenda kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa kupeleka maji kutoka pale Mkula kwenda Mwanalu utakaogharimu shilingi bilioni tatu. Ulianza kipindi lakini ulisimama kwa sababu ya fedha. Naomba Wizara ya Fedha sasa mpatieni fedha Mheshimiwa Waziri wa Maji ili mradi huu uliopo Busega mradi wa shilingi bilioni tatu kule Mwanale utaopeleka pia maji kule Chabutwa na maji huku Mwasamba pamoja na Mwangika, wananchi hawa na wenyewe wapate maji. Nakushukuru sana kwa sababu unafanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, lipo jambo la upotevu wa maji na Mheshimiwa Waziri, nimeiona Busega ni wilaya ya pili kwa kupunguza upotevu wa maji na umpe kijana wetu tu zawadi hata ya kumpigia simu. Amefanya kazi nzuri, alipokuja Mkurugenzi wa BUSEWASA pale Busega, upotevu wa maji mwaka 2023/2024 ulikuwa 19%, mwaka 2024/2025 ukaenda 13%, tunavyozungumza leo 2025/2026 umeenda 11%. Na mimi nimemwambia apambane mpaka afikishe single digit.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso, pambaneni kuhakikisha kwamba miundombinu ambayo ni mibovu tunaitengeneza ili upotevu wa maji uzidi kupungua. Maji yakipotea maana yake ni gharama. Tunaya-pump, tungeweza kuyauza kwa watumiaji wa maji, lakini kwa sababu yanapotea, yanaongeza hasara kwa Serikali, yanaongeza hasara kwa sehemu yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, na kazi nzuri imefanywa na Mheshimiwa Aweso na mimi nampigia makofi, kazi nzuri sana, ahsante sana. (Makofi)