Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia kibali na uzima kuweza kusimama ndani ya ukumbi wako kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi za dhati kabisa kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Itwangi, ni kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan. Mimi nimekuwa shahidi, nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Maji, miradi mikubwa imetekelezwa ndani ya nchi hii, ukifika unasema hakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anawatua akina mama ndoo kichwani. Miradi mikubwa ya fedha nyingi inatekelezwa ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, lakini pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji, kaka yangu Aweso, Naibu wako Waziri Engineer Kundo, Katibu Mkuu, Engineer Mwajuma na watalaamu wote wa Wizara ya Maji hakika mnaitendea haki Wizara ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Aweso kama namna ambavyo usemi wake siku zote anasema wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Itwangi lina vijiji 58, katika vijiji 58 vilivyopo ndani ya Jimbo la Itwangi vijiji tisa vina maji ya kisima, vijiji 14 vina maji ya Ziwa Victoria na vijiji 34 havina maji kabisa hata kidogo. Imani yangu kama mambo makubwa yameweza kufanyika katika nchi hii, hata wananchi wa Itwangi tunaamini vijiji 34 ambavyo havina maji vitakwenda kupatiwa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria umepita katika vijiji nane, bomba kuu limepita linakwenda Nzega mpaka Tabora lakini vijiji vyote nane vilivyopitiwa na bomba hakuna kitongoji hata kimoja ambacho kina maji na ndiyo maana nasema kwa kazi kubwa niliyoiona ninaamini kabisa yale makosa yaliyofanyika nyuma ya kupitisha bomba maji yanakwenda Nzega, yanakwenda Tabora, halafu wale wananchi wote wa Jimbo la Itwangi hawakupatiwa maji ninaamini ni wakati sahihi sasa wa Wizara ya Maji kuhakikisha vijiji hivi vyote nane vilivyopitiwa na bomba kuu vinakwenda kupatiwa maji na wao wasiwe watazamaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Itwangi vijiji vilivyopo ndani ya kilometa 12 kwa kila upande vyote havina maji, Wanaitwangi wana imani kubwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana ninakusihi sana imani kubwa waliyonayo wananchi wa Itwangi kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wanakwenda kupatiwa maji katika vijiji vyote 34 ambavyo havina maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mradi unaitwa Tinde Package wa awamu ya kwanza ya mradi wa maji uliokuwa unakwenda Singida, vijiji vyote 22 ni vijiji 14 tu ambavyo vimetekelezwa, vijiji vingine vyote havijatekelezwa. Ninaomba sana, ninakusihi sana Mheshimiwa Waziri twendeni tukawape haiwaki…
(Hapa kipaza sauti kilizimika)
MWENYEKITI: Mheshimiwa jaribu kusogeza pembeni hizo microphones…
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani muda wangu umeulinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji 22 vya Tinde Package awamu ya kwanza ya Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, mradi ambao umekwenda Nzega ni vijiji 14 ambavyo vimepelekewa maji, vijiji vingine vyote havijatekelezwa. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri akisimama hapa atuambie Wana-Itwangi ni mpango gani mkakati ambao umewekwa kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Itwangi wanakwenda kupata maji yaliyo safi na salama na siyo kuwa watazamaji wa kuangalia bomba linapita Jimbo la Itwangi linakwenda Tabora mpaka sasa linakuja Dodoma, lakini wao hawana maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine wakati tunasubiri Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana naipongeza Serikali kwa miradi mikubwa inayotekelezwa, ndani ya Jimbo la Itwangi nina shule za sekondari ambazo ni boarding, naziombea shule hizi ziende zikachimbiwe visima virefu ili ziweze kuondokana na shida kubwa ya maji iliyopo katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Kituli na Shule ya Sekondari Samuye hawana maji hata kidogo na shule hizi zina form one mpaka form six na zina mabweni mazuri ambayo yamejengwa na Serikali, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana chonde chonde, wakati tunasubiri Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria ninakuomba sana twende tukachimbe visima katika Sekondari ya Kituli na ya Samuye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria ungewanufaisha wananchi wengi waliopo ndani ya Jimbo la Itwangi iwapo tu vijiji vile 22 vitakwenda kutekelezwa ninahakika kwa asilimia kubwa tutakuwa tumegusa eneo kubwa la Jimbo la Itwangi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema yale yaliyopo kwa wananchi wangu wa Itwangi, naomba kuishauri Serikali ipeleke fedha za kuendeshea Ofisi za RUWASA, huo ndiyo ushauri wangu mkubwa kwa Serikali na ushauri wangu mwingine ni kuiomba Serikali na Wizara ya Fedha ihakikishe inapeleka fedha zote zilizotengwa kwenye bajeti kwa Wizara ya Maji ili miradi iliyokwama iweze kukamilika na miradi ambayo imesimama wakandarasi waende wakalipwe na miradi hii iwe yenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)