Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Nancy Hassan Nyalusi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua kwamba maji ni uhai na sisi hapa wote Waheshimiwa Wabunge hamna mtu ambaye hajatumia maji kwa siku ya leo. Kwa umuhimu huo huo ulivyo muhimu kwa wananchi wa vijiji 1,575 ambao hawana maji, wala hawana miundombinu yoyote, wala miradi yoyote inayoendelea katika vijiji vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Iringa tuna vijiji 44 ambavyo havina maji, wala hakuna miradi yoyote ya maji ambayo inaendelea katika maeneo hayo ukiachana na vijiji 44 miradi mingi imekwama, wakandarasi hawajalipwa na tayari wameshaondoka site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Mradi wa Maji wa Mbalamaziwa, Mradi wa Maji wa Kihesa Mgagao, Mradi wa Maji wa Ng’ang’ange – Mdeke. Hii miradi tayari imeishafika mwishoni lakini mkandarasi hajalipwa kwa hiyo ameondoka site, tunakuomba Mheshimiwa Waziri umlipe mkandarasi ili wananchi waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni Mradi wa Maji wa Pawaga. Tunaishukuru sana Serikali ilitupatia shilingi milioni 700 tumeweza kujenga chujio, tumeweza kujenga matenki, mabomba tayari yameshaletwa lakini sasa kinachotokea mabomba yale yameletwa yameachwa barabarani yanazagaa ambayo inapelekea wananchi wanapata hasira na kutamani kuyachoma yale mabomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia chanzo hakijajengwa, mkandarasi tayari ameshaondoka site kwa sababu hajalipwa. Watu wa Pawaga wanakunywa maji machafu ambayo yanapelekea magonjwa ya mlipuko katika eneo hilo kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunakuomba utufikirie na utusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni Mradi wa Itimbo, mradi umeshafikia 45% mkandarasi ameondoka site, hakuna kinachoendelea. Mradi mwingine ni Mradi wa Ifwagi – Halimba, tulisaini huu mkataba mwaka 2023 kwa furaha kubwa na shangwe, lakini mpaka sasa mradi umefika 11% hakuna kinachoendelea mkandarasi ameondoka site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ambao unatutia huzuni sisi wananchi wa Iringa ni Mradi wa Miji 28 wa Mafinga Mji. Huu mradi tulisaini na miji mingine 28 ambao wenzetu tayari wameishafika 80%, wengine wameishafikia 90% na wengine tayari wanapata maji, lakini sisi Mafinga Mji mpaka sasa hivi tuna 20% mkandarasi hayupo site, hamna mtu anatuelewa, Mafinga hakuna mtu anatusikiliza kwa sababu ya maji na hali ni mbaya, watu wanakunywa maji machafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama utuambie ni lini utawalipa wakandarasi na ni lini miradi hii itakamilika ili wananchi waweze kupata huduma ya maji na tunaweza kufanya maamuzi Waheshimiwa Wabunge, tufanye maamuzi. Tulifanya maamuzi kwenye umeme tumefanikiwa, tufanye maamuzi pia kwenye maji najua kwamba tutafanikiwa kwa sababu hali ni mbaya madeni ni makubwa na kuna vijiji na kuna watu ambao hawajapata maji na kuna miradi ambayo tayari inaharibika, miundombinu inaharibika ambayo inahitaji marekebisho kwa hiyo tufanye maamuzi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Maji ni lazima uongezewe pesa, Mfuko wa Maji ni lazima uongezewe pesa lakini pia pesa ambazo zinakusanywa zipelekwe kama ambavyo zilivyopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusema hayo yote kwa heshima kubwa naomba sana niishukuru Serikali kwa miradi ambayo imekamilika katika Mkoa wetu wa Iringa, tuna miradi minne ambayo imekamilika ya kiasi cha shilingi bilioni 8.14; tunaishukuru sana Serikali miradi hiyo itaenda kuhudumia wananchi 33,531 watapata maji safi na salama, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana viongozi wangu MD na RM kwa ushirikiano mkubwa ambao wanatupatia, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri tuna imani kubwa na wewe, tunajua kwamba unahangaika, tunaona mapambano yako na tunajua kwamba hii kazi utaimaliza wananchi wote tutapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)