Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kwa kunipatia nafasi niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia afya na uzima na kuweza kutukutanisha siku ya leo tukijadili hatma ya Watanzania kwenye suala zima la maji na tukiwa tunatambua kwamba maji ndiyo kila kitu, hata ili uweze siku yako ya mwisho imefika ili uende tukupeleke kwenye nyumba yako ya milele bila maji bado hayo mazishi yatakuwa hayajakamilika vilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa Watanzania hususan kwa wanawake wa nchi hii, dhamira yake na nia yake inaendelea kujidhihirisha dhahiri kwamba yuko tayari kuwakoa Watanzania wa nchi hii kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanapata maji salama na safi ya kunywa, lakini na kwa matumizi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana, mwaka jana wakati tunamaliza Bunge ama tunahitimisha Bunge nilikwambia sina hofu na Wana-Pangani watakurudisha, nami ninakwambia sina hofu Wana-Chemba wameniambia nitarudi kama msemaji wao na tumekutana mimi ndiyo msemaji wa Wana-Chemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wana-Chemba wamesikia hotuba yako kuhusiana na suala zima la Bwawa la Farkwa, wanakushukuru sana na wanaishukuru sana Serikali kwa hatua iliyofikia, lakini wameniambia niseme haya yafuatayo; kwamba Mheshimiwa Waziri tunamshukuru kwa hatua yake njema nzuri yenye matumaini makubwa, lakini mbona hajatuambia sasa tunasaini lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameomba mkataba huo na mkandarasi aliyepatikana, wanaomba usisainiwe Dodoma, ukasainiwe eneo la tukio kwa maana ya Kata ya Farkwa mradi unakokwenda kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tulipokutana pia nilikueleza changamoto ya maji kwenye Wilaya yangu ya Chemba na bahati nzuri ulinikabidhi kwa Katibu Mkuu. Ninamshukuru sana mdogo wangu Mwajuma, lakini na yeye alitoa maelekezo kwa DG - RUWASA. Ninamshukuru sana DG kwa kazi kubwa aliyopifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Wizara ya Maji kwa ushirkiano mnaonipatiia kwa ajili ya kuhakikisha tunakwenda sambamba na ninyi kutatua kero za wananchi wangu wa Wilaya ya Chemba. Ninawashukuru sana, Mradi wa Chandama ulikaa miaka 15 jana RM wangu ameenda kumkabidhi mkandarasi site kwa shilingi milioni 100 na zile shilingi milioni 60 zilizobaki ninaomba mnisaidie, lakini angalau tumeanza hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina vijiji viwili ambavyo tayari mashine ziko. Kijiji kimoja tayari Chekanao, lakini tunaenda Gongachini. Tangu dunia imeumbwa wale watu hawajawahi kupata maji. Ni upendo wa kipekee Wizara ya Maji mlioonesha kwa Wanachemba na wanawashukuru sana kwa dhamira na nia njema ambayo mnaendelea kuwapatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, Mradi wa Miji 28; Chemba tunakwenda vizuri, lakini tuliambiwa mradi huu tungekabidhiwa tarehe 30 Aprili, mpaka sasa bado, na bahati nzuri nilizungumza na yule mkandarasi akasema hawajaingiza pump, hawana transformer lakini na viungo kwa jili ya kuunga mabomba. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, leo kesho ukimaliza hebu tunakuomba fika pale, twende site tukajue huyu mkandarasi shida ni nini. Tunatamani Mradi wa Miji 28 ukamilike ndani ya Wilaya ya Chemba pale mjini na viunga vyake vyote viweze kupata maji, kwa sababu ule mji sasa unakuwa na ongezeko kubwa la uhitaji wa maji unazidi kuwa mkubwa. Tukiendelea kumlealea mkandarasi kidogo atatuangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Mji wa Chemba sasa unakua na tunakaribia kwenda kuitwa manispaa, ninakuomba sana utakapokamilika ule mradi tupatiwe tupate mamlaka ya maji ili tuwe na uwezo wa kusimamia na kuhakikisha huduma ya maji itapatikana kwa urahisi na utaweza kusimamiwa vizuri. Mheshimiwa Waziri ninaomba nikuletee kwako pamoja na timu yako miradi ya maji ya Wilaya ya Chemba ambayo imekaa zaidi ya miaka 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wana-Chemba wameomba niwasemee miradi hii. Mheshimiwa Waziri, mradi wa kwanza ambao mkandarasi alishapatikana tunasubiri kusaini tu kaka yangu, ni Mradi wa Mrijo Juu na Mradi wa Mwailanje. Wakandarasi wako tayari tunasubiri kusaini tu. Turuhusuni tusaini watu waanze hii miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini miradi inayosubiri kutangazwa iko miwili. Mradi wa Humekwa na Mradi wa Kumbunko. Ninaomba Mheshimiwa Waziri tupeni kibali tutangaze ili watu hawa waende wakapate maji, wana adha na shida kubwa ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vingine ambavyo navyo vimekaa kwa muda mrefu kwenye bajeti bila ya kutekelezwa viko 11. Mheshimiwa Waziri ni hivi vifuatavyo; kijiji cha kwanza Kijiji cha Piho, Kijiji cha pili Ndoroboni, Ombiri, Mpendo, Tandala, Wisuzaji, Baaba, Jiogolo, Gungi, Chioli pamoja na Majengo Mapya. Viko 11 Mheshimiwa Waziri, vimekaa kwenye bajeti zako, kwenye vitabu vyako kwa muda mrefu, tusaidie. Bajeti ijayo ninajua wewe kwa usimamizi wako na watendaji wako namna mlivyokuwa na mapenzi mema na Wana-Chemba, mnaenda kutusaidia hivi vijiji ili viweze kupatiwa maji na wananchi wetu wa Wilaya ya Chemba waweze kuwa na furaha na tabasamu la mama liweze kuwafikia.
Mheshimiwa Waziri ninaomba niseme Jiji la Dodoma, kwa sababu pamoja na Chemba lakini niko Dodoma. Mheshimiwa Jiji la Dodoma na wewe ni mkazi wa Dodoma, hali si shwari. Tusaidieni Wana-Dodoma tuwape fedha ili waweze kukamilisha miradi uliyoiainisha Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yako. Umeisema miradi yote sihitaji niirudie, lakini miradi hii Mheshimiwa Waziri kuitaja bila kuipelekea fedha bado tutakuwa ni kazi bure.
Kwa hiyo, ninakuomba wasaidieni Jiji wapate fedha watu wa DUWASA ili waweze kutekeleza hiyo miradi na Wana-Dodoma waweze pia kuwa na neema na tabasamu la Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja, na hongera sana kaka yangu. Kila la heri, Mwenyezi Mungu awatangulie. (Makofi)