Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ninaomba nianze kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, kwanza tumeona tangu juzi, jana amekuwa na wageni kutoka nchi ya Rwanda, kumpokea Mheshimiwa Rais wa pale Rais Kagame, halafu akampokea Rais William Ruto, na leo amekuja kutuhutubia hapa na nimevutiwa sana na mahusiano mazuri Rais wetu aliyonayo na viongozi wenzake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili zote zinaonyesha viongozi wenzake katika eneo hili wanamheshimu sana, sana, sana na hii inatuonyesha kwamba Tanzania tuna kiongozi imara, thabiti anayeheshimika. Piga mstari anayeheshimika. Kwa hali hiyo basi tunawajibika kumpa kila aina ya msaada na ushirikiano ili aweze kuipigania Tanzania na watu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, majadiliano ambayo tumeayaona kwa Mheshimiwa Ruto na nimevutiwa sana na lile suala la ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mafuta, bidhaa za petroli. Ninataka niseme kitu kimoja, tarehe 2 Aprili kwa kupitia swali namba 15 nikiwa hapa Bungeni niliuliza Serikali juu ya refinery. Leo tumepata majibu, ahsanteni sana Tanzania. Ninaamini hiki kitu kinakwenda kuijenga nchi yetu na kuipa heshima zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nichangie kwenye hotuba. Nianze kwanza kwa kumpongeza ndugu yangu Waziri wa Maji. Hakika ni mtu, yeye pamoja na wasaidizi wake wanahangaikia sana. Ni kama vile kamusi fulani la maji anatembea nayo kichwani, na ninaamini kabisa Wizara hii ameifanyia kazi njema, anajua anafanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii mimi ninapenda nimpongeze yeye, lakini vilevile ninaipongeza DAWASA pale Dar es Salaam. Mheshimiwa Engineer Bwire na timu yake yote, hakika wanafanya kazi vizuri sana. Tunaweza tukasema tuna shida Dar es Salaam, lakini hawa watu wanahangaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuhusu Dar es Salaam ninataka kidogo nizungumzie Dar es Salaam kwa sababu Jimbo la Kinondoni liko pale Dar es Salaam na kwa dada yangu Kibamba na kwingineko, kiukweli Dar es Salaam tuna shida. Maji yanapatikana ndiyo, lakini kuna shida. Nitaje kata ambazo tunaopata shida, Mzimuni, Kata ya Tandale, Kata ya Ndugumbi, Kata ya Hananasif, Kata ya Makumbusho, Kata ya Mwananyamala, Kata ya Kigogo, Kata ya Magomeni na pale kwenye Kata ya Kinondoni pamoja na Kijitonyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, DAWASA wanafanya kazi vizuri sana ila lazima Serikali iwasaidie. Mheshimiwa Waziri isaidieni DAWASA. Bila kuisaidia DAWASA itakuwa ni uongo. Hebu tuangalie takwimu; maji ambayo yanahitajika Dar es Salaam takribani ni lita milioni 772.7 kwa siku, lakini yanayozalishwa ni lita milioni 553.7 kwa siku. Lakini kuna upungufu wa lita milioni 219. Sasa hata hiyo ambayo inazalishwa lita 553.7 haifiki yote Dar es Salaam.
Mheshimiwa Waziri unafahamu upotevu wa maji, Wabunge wengi wanaosimama wanazungumza juu ya Non-Revenue Water. Hakuna mapato ambayo yanaweza kuonekana bila hesabu, hesabu zinaonesha karibu 49% ya maji yanayozalishwa yanapotea. Mitambo yetu imechoka, Alhamdulillah Serikali imeleta pump za kufunga, lakini mpaka leo ninaambiwa Juni ndiyo itafungwa. Ninaomba utusaidie uhakikishe DAWASA wanamaliza kazi ya kufunga pump zile ili maji mengi yaweze kusukumwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafanyaje kuondokana na tatizo hili? Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, mmetengeneze utaratibu ambao kweli utaonesha ni jinsi gani mnakwenda kupambanua na kuondoa hili tatizo la upotevu wa maji kutoka 49% angalau tufike 25%, maji yaweze kwenda. Kinyume cha hapo tutakuwa tunagombana bure na DAWASA na wewe tutakuwa tunakupa shida kila wakati kukutafuta.

Mheshimiwa Waziri ninaomba zitafutwe fedha vilevile ili mifumo chakavu muibadilishe. Dar es Salaam mifumo ile tangu mwaka 1960 wakati wa ukoloni ndiyo imejengwa. Haiwezi ikaendelea, na mingine ni ya chuma yamejaa kutu mle ndani. Tutaanza kusumbuana bure, wakati kumbe uwezo wa kubadilisha tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute fedha hata kama ni kukopa, watu wa Dar es Salaam wapate maji. Hakuna mbadala wa maji, maji ni dini. Kuna watu wanabatizwa kwa kupitia maji. Sisi waislamu hatuwezi kuswali na kupata udhu bila ya maji. Maji ni siasa, maji ni maisha, maji ni kila kitu na mwenyewe umesema Mheshimiwa Waziri, maji hayana mbadala. Hangaikieni na tutengenezeni miundombinu ambayo ni chakavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Kidunda; Mheshimiwa hili bwana utanisamehe, itabidi mimi nishike shilingi, na nitaishika na ukifanya mchezo ninakwenda nayo Kinondoni. Kwa sababu Bwawa la Kidunda tumpongeze Mheshimiwa Rais, kalianzisha mwaka 2023. Juzi na lilikuwa limalizike Juni, 2026 mwaka huu, tumefanya extensiyon mpaka Disemba. Sasa Mheshimiwa Waziri, kazi iliyofanyika ni 47%, miezi iliyobakia ni miezi minane. Hivi kweli kwa miaka mitatu tumefanya kazi ya 47%, asilimia 53 kweli tunaweza tukaifanya mpaka Disemba?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi ninaunga mkono hoja lakini tutakutana wakati wa shilingi. Ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)