Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu Waziri na Katibu Mkuu pamoja na wanaowasaidia kazi, lakini pia Mheshimiwa Rais. Ninakiri kwamba kazi kubwa imefanyika kwa ajili ya kuwapelekea wananchi maji nchi hii, lakini bado mahitaji nayo ni makubwa sana kwa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa Gridi ya Taifa inayoweza kutoa maji Ziwa Victoria kuja hapa Dodoma, lakini kumbuka kwenye vitabu vitakatifu vimeandikwa; “Kama vile Ayala aioneavyo shauku mito ya maji...”, vivyo hivyo Wana-Magu wanayaonea shauku maji ya Ziwa Victoria ambayo hawana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana Mradi wa Lugeye – Kigangama ambao utasaida vijiji saba, Kijiji cha Lugeye, Kitongo, Kigangama, Nyanguge, Kwa Bundilia, pamoja na Nyamahanga, Matela; mradi huu una shilingi bilioni saba. Mkandarasi amekwishalipwa shilingi bilioni 1.5, mradi uko 65%. Kazi ambazo amezifanya mkandarasi anadai shilingi bilioni 4.5. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwezi uliopita, Waziri, Naibu Waziri wa Maji aliahidi kwamba mwezi huu mwezi wa nne mwishoni watapeleka fedha kwenda kulipa mkandarasi ili aendelee. Nime-crosscheck bado hajalipwa mkandarasi. Ninakuomba sana Mheshimiwa Aweso, unasema anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Sisi Wabunge tunaotoka kwenye majimbo ndiyo tunajua matatizo ya wananchi. Ninakuomba sana Mheshimiwa Aweso, ninakuomba sana kazi nzuri uliyoianzisha tupeleke fedha ili miradi hii iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao Mradi wa Nyahanga – Isenyi, uko 85% na unahitaji shilingi milioni 700 tu ukamilike. Ni vijiji vinne, Isenyi, Nyahanga, Bohombe, pamoja na Nyashoshi. Tupatie shilingi milioni 700. Leo siyongelei miradi mipya ninaongelea miradi inayoendelea.
Mheshimiwa Waziri, ninakuomba sana Mradi wa Misungwi – Rumechi ambao uko 90%. Ninakuomba sana unahitaji shilingi milioni 400 tu ukamilike, lakini pia ninakuomba Mradi wa Sagani – Mwamabanza, ambao nao uko 90%; ambao utahudumia Mwamabanza, Salong’we, Sagani pamoja na Ng’walina. Huu mradi unahitaji shilingi milioni 500 uweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri ninakuomba Mradi wa Sola – Bubinza, uko 50%, una gharama ya shilingi milioni 840, mkandarasi amefanya kazi 50% hajalipwa hata shilingi. Ninaongelea miradi viporo, sitaki miradi mipya, lakini Waziri ninakuomba, Mradi wa Mahaha ambao una gharama ya shilingi milioni 400 umebaki shilingi milioni 200 tu wananchi wanakunywa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninakuomba miradi hii viporo ambayo imebaki, tumeenda nayo miaka mitatu leo ikamilike. Mheshimiwa Waziri ni aibu kwa Serikali yetu ambayo imefanya kazi kubwa sana, ambayo Mheshimiwa Rais tunajivunia pamoja na wewe msaidizi na wasaidizi wako. Mmefanya kazi kubwa, hebu tupeleke fedha hizi zilizobaki ili tuweze kumaliza miradi ya maendeleo. Ninakuomba tuone huruma. Sisi ambao tunatoka kwenye Ziwa Victoria maji tunayaona pale halafu wananchi hawana maji, tuone huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua nianzie miradi hii kiporo ili ujue kwamba kwa kweli ninahitaji kukamilishiwa miradi hii.
Ninakupongeza pia kwa kazi kubwa ambayo umeifanya. Mradi ule ambao unatokea Sawa kwenda kule Bujora, ninampongeza sana Meneja wa Maji Nelly. Mama yule amefanya kazi kubwa, umempa, umemsukuma namna ya kuweza kutenda kazi, tenki limekwishakukamilika. Chanzo pale mlikuja na Mheshimiwa Waziri Mkuu mkakizindua, chanzo cha Sawa. Mashine zimekwishakukamilika, ninaomba mashine zifungwe kwa sababu zimeshafika, yaanze kusukumwa maji kwenda kwenye Mji wa Bujora na Kisesa ambao utahudimia pia Kata ya Bukandwe, ili baada ya kufungwa tuanze kupata hayo hayo maji madogo ambayo mradi ni wa kizamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, tunaomba fedha kwa ajili ya kusambaza mabomba kwenye vijiji vyote vya Kata ya Bujora na Kisesa ili wananchi wetu waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara yako, haya mambo ya maji nimekwisha kuzungumza siku moja kwamba, asali ni tamu lakini watu wengi hapa hatuitumii, lakini mwanadamu kila siku lazima atumie maji. Awe mgonjwa lazima atumie maji, kwa chochote. Ninaomba sana kwamba kazi kubwa iliyofanyika tusaidie, Wanamagu tusaidie ili waweze kupata maji ambayo ni safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kisesa na Bujora kama ambavyo ninaeleza kila siku panastahili kuwa makao makuu ya wilaya. Hata Hayati Magufuli, wewe unaujua vizuri Mji wa Kisesa na Bujora, umefika na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mpango. Hata Hayati Magufuli alisema pawe wilaya. Ule mji unapanuka kwa kasi kwa sababu Mwanza imejaa, Nyamagana, Ilemela imejaa, watu wote wanakwenda Kisesa na Bujora kwenda Usagara. Kwa hiyo, ni mji ambao unatakiwa ufikiriwe kwa namna nzuri zaidi. tenki ambalo umeweka la cubic meter milioni tano ni mwarobaini. Shida ni kusambaza maji sasa kwenda kwa watumiaji. Ninakuomba sana jambo hili liweze kukamilika ili tuweze kuwasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyongelei miradi mipya, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)