Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mimi nianze na kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa kunipa kibali kuweza kusimama siku ya leo, lakini nimeipitia bajeti ya Wizara ya Maji na Mheshimiwa Waziri wa Maji, kaka yangu Mheshimiwa Aweso mimi sina tatizo na wewe. Ninatambua namna ambavyo unafanya kazi kwa ajili ya Watanzania, ninatambua juhudi za Serikali ambazo zinafanywa kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji, lakini ni ukweli usiyopingika kwamba maeneo yetu mengi bado yana changamoto kubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ndio uhai, lakini kuna Mbunge mmoja pale kaka yangu kutoka Mwanza amesema hakuna kitu kinachouma, unaona kitu ambacho kipo jirani yako kinakwenda sehemu nyingine wakati wewe unakihitaji na unateseka kwa sababu ya hicho kitu.

Mheshimiwa Waziri wa Maji, kaka yangu Aweso, Mkoa wa Kigoma tuna Ziwa Tanganyika, lakini inasikitisha katika Jimbo la Kigoma Kaskazini yapo maeneo ambayo toka tumepata Uhuru, dunia kuumbwa kuna vijiji havijawahi kupata maji kwenye mabomba.

Mheshimiwa Waziri, kuna Kijiji ambacho kinaitwa Kiziba, Kiziba kipo kwenye Kata ya Kagunga kama unakwenda Burundi mpakani. Wale watu yaani wanapanda dakika tano kwenye majumba yao wanalitazama Ziwa Tanganyika lakini wale watu hawajawahi kupata maji na nimefuatilia kwa watu wa RUWASA kule mradi wao unahitaji shilingi milioni 330 wananchi waweze kupata maji na watoke kwenye shida ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waziri wa Maji ninakuomba sana, ninarudia tena najua utendaji wako wa kazi, wasaidie watu wa Kijiji cha Kiziba shilingi milioni 330, mnaweza hata mkapunguza matumizi yenu, hata magari mkaacha mkatumia gari za kawaida ili hiyo pesa iende ikawasaidie wananchi, lakini miaka yote wamekaa watu hawana maji na kuna Ziwa Tanganyika, kiukweli siyo sawa. Kama tumeweza kutoa maji Ziwa Victoria Mwanza tumeyaleta Singida halafu kuna mtu yupo kwenye Kijiji ziwa Tanganyika, dakika tano hajapata maji kuanzia Uhuru kiukweli hatuwatendei watu hawa.

Mheshimiwa Waziri, mimi leo sitakuwa na mengi sana lakini nimesimama hapa kutaka kukuomba katika Jimbo la Kigoma Kaskazini yapo maeneo kwa mfano Mwandiga, nilipozaliwa ni mji mdogo, lakini Mheshimiwa Waziri, watu wanakaa mwezi mzima hawana maji kwenye mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna maji ya Ziwa Tanganyika kutoka mjini na manispaa yanaishia pale Ntovye pale kwenye Sokwe. Tusaidieni watu wa Mwadiga maji yapande pale juu, watu watumie maji. Mimi nimezaliwa pale mpaka leo mama yangu anabeba maji, hatuna maji tuwasaidie kinamama. Kama kweli tunasema tunamtua ndoo mama kichwani, tuwasaidie hawa akina mama ambao mimi nimezaliwa nabeba maji mtoni, mpaka umri huu ninakwenda kuzeeka akina mama wanabeba maji, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Kigoma Kaskazini, kuna Mradi wa Kiziba nimeusema, lakini kuna Kaseke - Nyamori ambao tunahitaji kama shilingi 131,620,000 wananchi waweze kupata maji. Tuna sehemu ya Zashe, Kagunga tunahitaji kama shilingi milioni 200; lakini tuna Mkongoro tunahitaji kama shilingi milioni 150 Mheshimiwa Waziri. Tuna Mtanga hii Water Supply Scheme tunahitaji shilingi milioni 40 tu wananchi wanaweza kupata maji, lakini tuna Mwamgongo - Bugamba tunahitaji kama shilingi milioni 39 wananchi wanapata maji lakini tuna Mkongoro II.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kigoma Kaskazini kuna miradi mikubwa ya maji; Mkongoro I na Mkongoro II ambayo inahudumia wananchi wengi sana, lakini miradi Mheshimiwa Waziri imetelekezwa, tunaomba mtupatie pesa tuweze kutatua changamoto hii ya maji, lakini tuna uchimbaji wa kisima katika Kata ya Kalinzi, Kijiji cha Mkabogo Mheshimiwa Waziri watu hawana maji, ninakuomba sana kaka yangu wasaidieni watu wa Kigoma tuweze kupata maji na sisi tuone fahari ya Ziwa Tanganyika. Hatuwezi kuwa na Ziwa Tanganyika karibu lakini leo tunalalamika maji miaka 60 ya Uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Mheshimiwa Waziri, ninakuomba sana kuna ujenzi wa visima katika Vijiji vya Kizenga, Nyamuhoza, Mkongoro, Milinzi na Mkabogo tusaidieni tuweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine katika Wizara ya Maji ni suala zima la bill; na ninakuomba Mheshimiwa Waziri, lichukue kaa na jopo lako la watu wa maji, wananchi wanalalmika wanabambikiwa bill za maji. Anakuja mtu anasoma, hamshirikishi mwenye nyumba, anatuma message unadaiwa kiasi fulani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, ninakuomba sana hilo pia ulichukue muweze kulifanyia kazi, wananchi walipe bill kulingana na matumizi yao na kusiwe na ongezeko lolote la bill.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na Kigoma kuna maeneo mengine Mheshimiwa Waziri yanachangamoto yam aji. Hapo hapo Dar es salaam ambapo tunaita jiji, ambayo ndio sura ya nchi, lakini kuna maeneo Mheshimiwa Waziri, maji ni changamoto: mfano wale wanaokaa Goba wanajua, Kimara, Mbezi watu wanakaa zaidi ya wiki kadhaa hawapati maji kwenye mabomba.

Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Aweso ninajua jitihada ambazo unazifanya, lakini ninakuomba sana katika bajeti hii pesa ambazo mmeziomba zifike kwa wakati kwa sababu kuna ucheleweshaji wa pesa za miradi. Wapelekeeni pesa DUWASA, wapelekeeni pesa watu wa RUWASA ili wafanye kazi waweze kutatua changamoto zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala zima la vitendea kazi katika jimbo langu, Wilaya yangu ya Kigoma Kaskazini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Muda wako umeisha.

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru. (Makofi)