Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Maji na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mahali hapa jioni ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaeleze Wabunge wenzangu kwamba miaka ya Bunge lililopita tuliwahi Wabunge sisi wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuishauri Serikali kutumia vyanzo vikubwa vilivyopo nchini kwa maendeleo ya kiuchumi na leo tunapoiona Serikali imesimama, imekuja na jambo la Gridi ya Taifa ya Maji. Jambo hili ni jambo letu, tunapaswa kulibeba na kulishika mkono na kulisemea kwa juhudi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuipongeze Serikali kwa namna ambavyo inaendelea kuwa sikivu, tunampongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo amekubali maoni ya Wabunge wa Bunge hili, lakini tunawapongeza sana watendaji wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri, namna ambavyo wameweza kutangatanga huku na kule kuhakikisha wanapata uzoefu mkubwa kuhusiana na jambo hili la Gridi ya Taifa ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewashuhudia Mheshimiwa Waziri wetu pamoja na Katibu Mkuu wakitangatanga kule China kwenda kutafuta jambo hili la Gridi ya Taifa ya Maji. Niwapongeze sana kwa kutangatanga kwenu, leo Mheshimiwa Waziri umesema sisi watu wa Tanga hatutangitangi, lakini katika kutafuta maendeleo kaka yangu Aweso umetangatanga, katika kutatua changamoto za maji katika Taifa letu Aweso na Mwajuma mmetangatanga. Tunawapongezeni sana kwa jambo hili ambalo mmelileta mbele yetu na ninaomba Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu Serikali inatekeleza maoni yetu tuna kila sababu ya kuliunga mkono jambo hili kwa asilimia zote, tusimame pamoja kuhakikisha kwamba Gridi ya Taifa ya Maji inatokea katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ndugu zangu kule China, limetekelezwa takribani miaka 50 iliyopita na Japani wametekeleza jambo hili tangu mwaka 1960. Ndugu zangu Gridi ya Taifa ya Maji ndio mwarubaini, ndio mwarubaini wa maeneo yote aliyoyataja Mheshimiwa Kiza kule Dar es salaam kwamba hayawezi kufikiwa na maji. Maji yanarasilimali tulizozipata ni ya Taifa zima, maji haya ya vyanzo vikubwa ya maji yanaunganishwa na kuweza kutolewa Ziwa Victoria na kuweza kufika maeneo ambayo hayana maji kama Dodoma. Yanaweza kufika mpaka Tanga kupitia kule Manyara na Arusha, yanaweza kutoka kule Ziwa Tanganyika na kuweza kufika Tabora, jambo hili ni jambo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wabunge wenzangu tuliunge mkono, ni sisi tuliyoishauri Serikali itumie vyanzo vikubwa vya maji kuleta maendeleo na mapinduzi ya kiuchumi ndani ya Taifa letu. Jambo hili ni la Wizara ya Mifugo, jambo hili ni la Wizara ya Kilimo, jambo hili ni jambo la Watanzania wanaohitaji maendeleo endelevu na Taifa letu liweze kunufaika kiuchumi, tunapokwenda kwenye Dira ya 2050. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme kwamba kwa jambo hili phase one imeombwa shilingi trilioni tano kwa kilometa 6200. Ndugu zangu Watanzania kama tuliweza kuishauri Serikali ikaweza kutekeleza SGR kwa matrilioni ya shilingi na tukaweza kutekeleza Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa trilioni za shilingi, jambo hili pia tuiombe Serikali yetu ilitekeleze ili tuweze kupata maendeleo endelevu yanayotokana na maji yetu ambayo Mungu ametubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani nilipokuwa kule Japan niliweza kufanya presentation kuhusiana na vyanzo vya maji kwenye Taifa letu. Nilipokuwa nikieleza Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, ziwa sijui wapi, wakasema your country must be rich. Maana yake ni kwamba bado kama Taifa hatujaweza kutumia vyanzo vikubwa vya maji kwa kuhakikisha tunakuza uchumi wetu, lakini Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama wa mapinduzi makubwa ameshalibeba jambo hili, tuiombe sana Wabunge tuliunge mkono, tulione ni la kwetu ili jambo hili liweze kutokea. Haiwezekani tuwe na vyanzo vyote vya maji, Wizara ya Maji iwe ni Wizara ya Maji ya kunywa tu. Tunahitaji vyanzo vya maji vichangie kwenye uchumi endelevu wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba kusema kwamba tunayo miundombinu ya maji kule mkoani Tanga na tunashukuru tumewekwa katika miradi ya kimkakati kama miradi ya Segera-Kabuku, kama miradi ya Duburuma-Songe, kama miradi ya kuboresha miundombinu ya maji Tanga Mjini, Muheza na Pangani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba miradi ile ikamilike, fedha ziende ili wananchi wa Mkoa wa Tanga waweze kunufaika na maji na rasilimali maji na kuweza kuendesha viwanda ambavyo Mheshimiwa Rais, ameahidi kuweza kuvifufua viwanda vyote vilivyokufa Jijini Tanga. Bila maji haya inamaana kwamba hayawezi viwanda vile kukua na kuweza kufanya kazi zake vizuri, tunaomba mradi huu wa maji wa Ziwa Victoria ambao utakuja Dodoma, utakwenda Manyara, utakwenda Arusha mpaka Tanga uweze kufanyika ili kule Tanga viwanda vyetu viweze kufanya kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema kwamba wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji nao wana-struggle kwa hali ngumu sana, wanadai fedha nyingi, hawajalipwa muda mrefu. Kwa mfano wakandarasi wanaofanya kazi Tanga RUWASA, peke yao wanadai shilingi bilioni 14.5 lakini wakandarasi wa Mamlaka za Maji wanadai shilingi bilioni 16. Bila kuiongezea Wizara hii fedha za kutosha na kuweza kutafuta vyanzo mbadala, inamaana bado jambo hili la maji litakuwa kwenye wakati mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niziombe Wizara nyingine zote zinazohusika katika jambo hili la Gridi ya Taifa ya Maji, tuungane kwa pamoja kuhakikisha jambo hili linatokea na hatimaye Tanzania yetu iendelee kukua kwa uchumi tunapoelekea kwenye Dira ya 2050. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe kusema kwamba tunao mradi mkubwa pale Mkinga, mradi wa shilingi bilioni 35. Mradi wetu ule tunaishukuru Serikali, lakini fedha zake zimekuwa zinakuja kwa kusuasua, tunaomba sana Serikali iweze kuhakikisha fedha zinakwenda katika mradi ule wa Mkinga ili tuweze kuumaliza mradi ule kwa haraka na wananchi wa Mkinga waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo basi ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)