Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kibali cha leo cha kuweza kusimama Bungeni, nikitoa mchango wangu katika Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais shupavu kwa nia njema ya kuwakomboa Watanzania hasa kwenye jambo kubwa hili la upatikanaji wa maji nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumshukuru sana Waziri, Jumaa Aweso pamoja na mdogo wangu engineer Kundo kwa kazi nzuri wanazozifanya lakini wasaidizi wao; Katibu wa Wizara lakini nimshukuru engineer wangu wa Mkoa wa Tabora, ndugu yangu Kapufi pamoja na engineer wa RUWASA kule Kaliua ndugu yangu Mapambano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ulyankulu, lenye takribani wananchi 400,000, tunayochangamoto kubwa yam aji. Pamoja na kazi nzuri za kutuanzishia miradi saba inayotekelezwa kwenye jimbo hilo, yenye thamani ya shilingi 6,127,500,000 tunaishukuru Serikali kwa bajeti hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya majimbo ya Mkoa wa Tabora 12, Jimbo la Ulyankulu ni jimbo pekee ambalo halina mradi wa maji ya Ziwa Victoria, maji hayo yamekuja mapaka eneo la Ushetu yakavuka yakaenda Kaliua, yamezunguka yakaja Urambo na yakaja Uyui. Tunao mradi mmoja tu mkubwa wa Bwawa la Ichemba, lililotengewa fedha shilingi bilioni 3.883. Mradi huu unatakribani ya miaka 10 sasa, ulianza kutekelezwa mwaka 2015 mpaka sasa mradi huu una 10%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, mimi ninakuamini, ninakukubali kwamba ni mtu usiependa kuzinguliwa, lakini ninaona kama watu wa Ulyankulu ni kama unawazingua hivi. Nikuombe mdogo wangu Mheshimiwa Jumaa Aweso, tumezungumza na wewe, ongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu, hatuna mradi mwingine wenye matumaini kwa wananchi hawa. Wananchi wa Jimbo la Ulyankulu kwenye hizo kata mpaka sasa pamoja na masika hii dumu la lita 20 wananunua shilingi 1,000 ni jambo ambalo ni hatari sana, nikuombe Waziri uweze ku-support mradi huu uweze kutekelezwa kwa kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haitoshi, tunayo miradi ya Wizara ya Kilimo, tunayo miradi miwili kwenye Kijiji cha Konanne pamoja na Kijiji cha Mwendakulima eneo la Uyoa. Niwaombe ikikupendeza unganisha na wewe kwenye hiyo miradi ili kuipanua miradi hii iweze kwenda mashambani, lakini mingine iende kwenye mifugo na mingine itumike kwa ajili ya maji. Tunao uhaba mkubwa sana wa maji kwenye jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi Mto Igombe ambao unapeleka maji Ziwa Malagarasi kila wakati unapitisha maji mengi, sisi tunayaona kwa macho. Tuwaombe ikiwapendeza muone haja ya kukinga Mto Igombe ili sisi tuweze kupata maji ya kutosha yanayoweza kuhudumia jimbo zima kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi inayoendelea, nikuombe sana upo mradi unaotekelezwa kwenye Vijiji vya Seleli, Mwendakulima, Mwongozo, Uhindi, Kanindo, Kaswa, Sungwa, Ikonongo na Usigala. Mkadarasi alishafanya kazi yake, lakini changamoto ni malipo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, mkandarasi na baadhi ya wazabuni walipwe ili kazi ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Jimbo la Ulyankulu umeniahidi mimi mwenyewe kwamba baada ya Bunge tutakwenda pia. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, wewe na Naibu wako ujipange kwenye hili ili kwenda kutoa ufafanuzi vizuri juu ya suala la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Mawaziri wote; kumekuwa na changamoto kwenye wilaya moja yenye zaidi ya jimbo moja, jimbo ambalo halitoki makao makuu ya jimbo linasahaulika sana, aidha, kwa kutembelewa na kwenye bajeti. Ukiwa Tabora unanyooka na barabara moja inayokwenda Ulyankulu, nikuombe miaka mitano wananchi wamekosa kuona viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Mawaziri, eneo hilo sasa la Jimbo la Ulyankulu tufungue mlango sasa wa kupata taarifa za viongozi wa Serikali hasa Mawaziri na Naibu Mawaziri, ninawakaribisha. Ikumbukwe tu kwamba, Jimbo la Ulyankulu ndio jimbo lililopigania pia uhuru wa nchi hii, ukimsikia Mtemi Mirambo, ametokea pale ni kati ya watemi maarufu nchini.
Kwa hiyo, nikuombe na mimi mtambue tu kwamba na mimi ni chifu, utakapokuja Waziri na Naibu Waziri, nitakufikisha kwa Chifu Mirambo na kwangu kwa chifu mwenyewe ukashuhudie kazi nzuri zinazofanyika kwenye eneo hilo ukaweze kupata baraka hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vijiji ambavyo vilifanyiwa utafiti wa uchimbaji wa maji, lakini mpaka sasa havijafanyiwa uchimbaji wa maji kwa ukosefu wa fedha. Nikuombe Waziri, vipo vijiji 13, nikuombe sana kazi hiyo ya fedha zipatikane ili vijiji vikaweze kuchimbiwa; Kijiji cha Ilege, Usonga, Mwendakulima, Ulanga, Utantwamke, Ibambo pamoja Ikonongo na Sungwa yenyewe.
Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana uweze kutoa fedha kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia maji, maji ndio yamebeba kila kitu, maji ndio yamebeba kila kitu Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana katika miradi hii ambayo umetupa miradi saba, kasi ya maji ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sekondari 17, watoto wa shule wanatembea na vidumu kwenda shuleni. Tunazo shule za msingi zisizopungua 64, watoto kila wakati wanatembea na vidumu vya maji, wewe ndio mwarubaini wetu, tukuombe sana Mheshimiwa Waziri uone umuhimu wa kutu-support, lakini haitoshi tufikirie pia kwenye mpango wa Ziwa Victoria, kwa sababu Ulyankulu tumekaa kama ambavyo jengo hili la Bunge lilivyojengwa, sisi tupo katikati. Ukiizunumza Uyoa, ukiizungumza Uloa naizungumzia kama ambako walipo mwisho wa viti vya Bunge na upande wako kwa maana ya Kaliua. Sisi hapa katikati ndio tumebaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji, ninayoimani kubwa sana na wewe kwamba jambo hili ukisimama vizuri tunaweza tukayapata haya maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inayoendelea nimeiona, kuna mradi kwenye vijiji vya Sungwa, Ikonongo, Usigala yenye thamani ya shilingi milioni 957.1 kasi yake Mheshimiwa Waziri ni ndogo, tukuombe sana kasi iendelee kutekelezwa, mradi huo upo 15%. Ni kama ambavyo ulivyo mradi wa bwawa la Ichemba, upo 10% miaka 10, lakini cha kusikitisha Mheshimiwa Waziri, nimeangalia kwenye hotuba yako, mradi wa Bwawa la Ichemba sisi kwenye jimbo tunatambua utahudumia kata tisa na vijiji 27, lakini kwenye hotuba yako umeonesha kwamba utahudumia kata saba na vijiji 22, ninaomba wakati wa kuhitimisha hotuba yako uweze kuwaeleza Wana-Ulyankulu kwamba...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, lakini nikushukuru na kukupongeza Mheshimiwa Waziri, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi