Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiyo muweza wa yote katika ulimwengu wetu. Pia, ninakishukuru Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi thabiti wa Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia, nivishukuru vikao vyote ambavyo vimekaa vya uteuzi hadi kupitisha jina kufika Kamati Kuu na kuweza leo kuwa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu ambao wapo sehemu mbalimbali katika nchi hii Wilaya zote za Nchi hii ya Tanzania. Ni ahadi yangu kwamba yale ambayo nimeahidi nitaendelea kuyatekeleza kwa ambavyo Mwenyezi Mungu atanijalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, sasa nitumie fursa hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na timu yake yote ya Mawaziri waliohudumu katika Ofisi hii ya Rais, Muungano na Mazingira ambapo sasa hivi yupo ndugu yetu, Mheshimiwa Hamad Yusuph Masauni pamoja na timu yake yote ya watendaji katika Ofisi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kama ambavyo Kamati imeeleza mafanikio yamepatikana sina haja ya kuyarejea. Kazi iliyofanywa ni kubwa, changamoto 25 kuondolewa zikabaki tatu, siyo kazi ndogo. Hatuna budi kuipongeza Serikali kwa juhudi hizi inazochukua kuboresha au kulinda na kuudumisha muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kabisa maono ya viongozi wetu wote kuanzia Awamu ya Kwanza hadi hii ya Sita wana uelewa, wanathamini na kutambua umuhimu wa muungano wetu ikiwa ni tunu pekee na muungano pekee ambao unaheshimiwa na kuthaminiwa Barani Afrika na duniani kwa ujumla, ndiyo maana jitihada hizi zilifanyika kuanzia Awamu ya Kwanza hadi ya sasa hivi ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani hiyo itujengee Watanzania na sisi tuweke mindset zetu vizuri Watanzania wote na kuthamini, kuuenzi na kuuheshimu Muungano wetu ikiwa Bara la Afrika na dunia kwa ujumla inatambua Muungano wetu ni muungano wa kipekee ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 60 ukiwa umedumisha Taifa moja lenye amani, utulivu na mshikamo. Je, sisi Watanzania kwa nini tusijivunie na Muungano wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika siku hii ya leo ninaomba niishauri Serikali yetu sikivu, pamoja na maoni mazuri yaliyotolewa na Kamati ya kuunda vituo, Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma, ninaongeza mchango wangu ili kuboresha kama si bajeti hii, lakini ninajua tunaweza kupata njia mbadala ya kutafuta fedha. Tushirikiane na Wizara ya Elimu, tuhakikishe kama ambavyo tunafundisha Somo la Historia kwa mambo mengine ambayo mara nyingi tumekuwa tukishauri katika Bunge letu, suala la uraia, uzalendo, maadili ya Taifa letu sambamba na suala la Muungano wetu lihusishe katika mitaala ya elimu kwa kiwango tutakachoona inafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu haiwezekani kwamba Bara letu la Afrika nje ya nchi yetu, duniani kwa ujumla waelewe kama ni Muungano wetu ambao umeunda nchi mbili huru na kupata dola moja, muungano wa pekee duniani ambao umedumu kwa muda mrefu kuliko muungano wowote duniani, iwe sisi Watanzania hatuuelewi na kuuthamini, uthaminiwe na nchi za nje. Itakuwa ni jambo la ajabu na aibu kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri huu ninauelekeza tushirikiane na Wizara ya Elimu tulifanye hili jambo liwe mahsusi kwa Taifa letu. Kama ambavyo tunamuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume wa Zanzibar na thamani ya Muungano wetu ambao umeanzishwa na waasisi hawa iendelee kudumu vizazi na vizazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tupo mahali si pabaya sana, lakini kutoendelea kuelewa thamani ya muungano wetu namna ambavyo umeundwa na ambavyo unaendeshwa kwa kizazi kilichopo ambacho hakijazaliwa wakati wa muungano kunaweza kwenda kuhatarisha muungano wetu miaka ya mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri huu mdogo ambao ninahisi ni muhimu sana kwa siku ya leo ninaomba wauchukue na kuufanyia kazi. Vinginevyo mimi ni muumini wa muungano na nitaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu hadi mwisho wa uhai wangu muungano huu udumu miaka hata elfu ikiwezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)