Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwanza kabisa ninapenda kuipongeza Wizara hii kwa kazi kubwa inayofanya katika kuhakikisha mazingira ya nchi yetu yanahifadhiwa, lakini pia kwa kusimamia shughuli zote zinazohusu Muungano. Ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninajielekeza kwenye upande wa mazingira. Juhudi kubwa zinafanywa katika kuhifadhi mazingira ya nchi yetu, pia kukabiliana na matatizo ya mabadiliko ya tabianchi. Ninachoomba na kusisitiza hii Taasisi ya NEMC ifanyiwe haraka kupewa mamlaka ili iwe nguvu ya kusimamia mazingira na mabadiliko ya tabianchi, iwe na nguvu za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo ninashauri kwamba Mfuko wa Mazingira utafutiwe vyanzo vya uhakika ili kuwe na fedha za uhakika katika kukabiliana na matatizo ya kimazingira na matatizo ya mabadiliko ya tabianchi, tuwe na fungu la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyoona sasa hivi mabadiliko ya tabianchi yanaathiri mambo mengi, yanaathiri miundombinu na yanaharibu rasilimali za nchi hii. Kwenye mabadiliko ya tabianchi lazima twende sambamba na kuhifadhi uoto wa asili. Ukataji wa miti umekuwa ni mkubwa sana na kuharibu uoto wetu wa asili, ambapo huu uoto wa asili tunauhitaji kwa mambo mengi yakiwemo utafiti na mambo ya kujua dawa zetu za asili lazima tuwe na hifadhi ya uoto wa asili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali mbaya ya kimazingira inachangia kuharibu nchi yetu kwa misingi kwamba, kwa mfano, maeneo ya Pwani ya Tanzania sasa hivi bahari inakuwa na inakwenda kula nchi kavu, inatoka inapanda, inashuka chini. Yaani inatoka baharini inashuka chini na baadhi ya maeneo tayari yameshaanza kuathiriwa na mabadiliko haya ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mifano duniani, kuna baadhi ya visiwa havipo tena kwenye ramani ya dunia, vimeshafukiwa na bahari. Kwa hivyo, ni lazima tuangalie kwamba tuna Tanzania iliyokamilika pamoja na visiwa vyake vinabaki kuwa urithi wa Taifa hili na tusije tukavipoteza visiwa hivi kutokana na matatizo ya kimazingira, ibaki Tanzania na uhalisia wake kama ilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwenye upande wa upandaji miti. Serikali inafanya juhudi kubwa, inatenga fedha nyingi katika upandaji miti, lakini sasa lazima tuhakikishe tunaotesha miti. Kwa sababu kuipanda ni suala lingine na kuiotesha ni suala lingine. Kuiotesha ni kuisimamia ile miti ikakua na ikatoa faida. Ninashauri hapa, ikiwezekana kuwe na mashindano katika vijiji na halmashauri, waliootesha miti ikakua na hapo ukubwa wake na kuihifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili iwe changamoto vijiji vyetu na halmashauri na taasisi nyingine ziwe na ari ya kupanda miti ili Tanzania iwe Tanzania ya Kijani. Ukitua kwenye ndege uone miti green badala ya kuona mabati yamepangana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninajielekeza kwenye Muungano. Tumebakisha siku tano tu kutimiza miaka 62 ya Muungano wetu. Ni safari ndefu, tumeanza mbali, tumepitia misukosuko mbalimbali, tumepitia changamoto mbalimbali, lakini bado Tanzania ipo imara, Watanzania wapo imara, Taifa lipo moja lenye upendo, lenye mshikamano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu umeasisiwa kwa misingi yake, misingi ya undugu, upendo, mshikamano, maridhiano na kustahamiliana. Ninawapongeza viongozi wote wa awamu zote kuanzia Waasisi wa Muungano huu hadi kufikia leo kuhakikisha kwamba muungano huu unadumu, Taifa linakuwa moja lenye umoja, juhudi zao, maarifa yao, ustahamilivu wao, viongozi wetu hao ndiyo leo wametufikisha hapa pamoja na sisi Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ni tunu ya Taifa hili na muungano huu ndiyo unatufanya tuwe na tunu kubwa ya amani na utulivu. Kwa hivyo, kuna kila sababu na kila haja ya kuutetea na kuulinda kwa vitendo muungano wetu ili tuendelee kuwa na tunu hizi za taifa ambazo zinatupa umoja na mshikamano wa kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu ninakubaliana na wazo la Wizara na Kamati hizi. Kuna changamoto kubwa ya Ofisi za Muungano kwa upande wa Zanzibar. Ninaishauri Serikali iendelee kutenga bajeti ili kuweza kujenga zile ofisi za sekta za muungano kwa upande wa pili wa muungano ili kuwe na majengo yenye heshima na yenye hadhi ya sura yenyewe ya muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ukomavu wake, maono yake, kwa kusema kwamba kwa awamu hii au mwaka huu Sherehe za Muungano zisifanyike na badala ya fedha zile kutumika kwa sherehe zikatengeneze miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa zilizojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwa Mheshimiwa Rais wetu ni mapenzi kwa wananchi wake na ni mapenzi kwa nchi yake kuona wananchi hawapati tabu, hawapati changamoto zozote na wanaishi kwa furaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, linguine, ninawapongeza kwamba turejeshe ile ligi ya muungano. Ligi ile vijana wanaipenda na wanaifurahia sana ambayo kwa miaka mingi kombe lile la muungano halikuwepo, sasa hivi linaendelea kufanyiwa kazi na mashindano yanaendelea.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)