Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makunduchi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara yetu hii, Ofisi ya Rais, Muungano. Kwanza, kabla ya yote ninampongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, kuweza kulijenga Taifa letu hili na kutuletea maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Nchimbi, akiwa kama ni Mtendaji Mkuu katika Wizara yetu hii, Ofisi ya Rais, Muungano. Tatu, ninampongeza Waziri wetu Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni kwa namna ambavyo anafanya kazi zake hizi za Ofisi ya Rais, Muungano. Tatu, ninawapongeza watendaji wote wa Wizara hii, wakifuatia Makatibu Wakuu wote, Manaibu Katibu Wakuu, pamoja na kurugenzi zake zote zilizopo katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika mchango wangu, hasa kwa upande wa Muungano. Tukiwa tunajadili Hotuba ya Wizara ya Muungano na Mazingira, ninajikita zaidi kwa upande wa Muungano. Tukija kwenye historia ya Muungano wetu wa Tanzania, sisi Watanzania tunasema kwamba, tumebahatika, tuna Muungano ule wa kimaumbile. Ninasema kwamba, tuna Muungano wa kimaumbile kwa sababu, kabla ya Muungano huu tulikuwa tuna mahusiano ambayo ni ya kidamu, tuna mahusiano ya kibiashara na tuna mahusiano ya mambo mbalimbali kabla ya kuja kwa Muungano wetu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri kuja kwa waasisi wetu wawili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, wao wakaanzisha na kuimarisha rasmi Muungano wa Tanzania kwa kuziunganisha nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, kuwa kitu kimoja. Nikasema kwamba, viongozi wetu wawili hawa, wao ndiyo waliokuja kuuimarisha Muungano na nikasema kwamba, wamekuja kuuimarisha Muungano kwa sababu, Muungano wenyewe upo kimaumbile. Sasa wao wakaamua kwa dhamira ya pamoja kwa mujibu wa sera za vyama vyao; Sera ya Chama cha TANU pamoja na Sera ya Afro-Shiraz Party, kwa umoja wao wakatuunganisha na kwa makubaliano yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hivyo, maana yake kabla ya kuunganisha vile vyama, waliunganika wao kama nchi na bahati nzuri nchi zetu sisi pamoja na kwamba, zimeungana kimaumbile, lakini baadaye nchi zetu hizi zikaja zikaungana kwa mujibu wa surface zetu zote mbili kwa kuchukua mchanga wa Tanganyika na mchanga wa Zanzibar na kuuchanganya mahali pamoja. Kitu ambacho wakati mwingine ninawaambia watu, mtu yeyote yule ambaye anataka kuvunja Muungano labda akazibague zile chembe za mchanga, achukue chembe za Zanzibar moja moja, pamoja na zile za Tanzania Bara, upande wa Tanganyika, aseme hizi tayari ninazibagua, kitu ambacho hakitawezekana katu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tuna ile tafsiri ya kuzungumza, kuimarisha Muungano. Katika nadharia yangu ninasema kwamba, katika kizazi chetu hiki tulichonacho sisi hatuimarishi Muungano, tunatakiwa kuboresha Muungano kwa sababu, tayari umeimarika. Kitu ambacho kimeimarika, maana yake husemi sasa unakiimarisha, kitu kilichoimarishwa unasema hiki sasa hivi tunakiboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, sisi sote kwa sasa hivi, maana yake Watanzania, hatuimarishi ila tunaboresha Muungano. Ninazungumza hivyo kwamba, tunaboresha Muungano, siyo kuimarisha kwa sababu, utasikia kuna kitu kinachoitwa changamoto. Kwa kweli, Watanzania sisi hatuna changamoto, in such, isipokuwa tuna ule uboreshaji wa Muungano na kila kitu ambacho kina hitilafu, kinatakiwa kuboreshwa na maboresho yetu ndiyo yatakayoweza kutuweka mahali pamoja. Ndugu zangu, viongozi wenzangu, Wabunge wenzangu, Muungano ni Tunu ya Taifa na Muungano ndiyo umoja wetu Watanzania. Hakuna hata mmoja kati yetu sisi atakayesema mimi sitaki Muungano kwa sababu ya faida ambazo zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la Muungano lina faida nyingi tu ambazo zipo. Kuna faida za kiuchumi za moja kwa moja, kuna faida za kisiasa na kuna faida za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia suala la kisiasa, maana yake ni kuviunganisha vyama vyetu viwe vya kitaifa na tuwe tunafanya mambo yetu pamoja. Nini maana yake kwenye upande wa kisiasa? Maana yake ni Muungano wetu unaimarika siku hadi siku katika mazingira ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida za kiuchumi ni kwamba, tunafanya biashara kwa pamoja na tunatembeleana kila mahali. Suala la fedha, tuna fedha za pamoja na kila kitu chetu kinakuwa ni cha pamoja. Hiyo yote maana yake nikasema katika masuala ya kiuchumi tunatumia sarafu moja, tuna bandari moja na tunakusudia kuwa na mfumo mmoja wa bandari, TRA na mambo mengine maana ni ya pamoja. Ni kitu ambacho kinaweza kuimarisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala la Muungano, nije kidogo katika suala la Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar. Kwa upande wa Zanzibar, Wizara hii ya Muungano na Mazingira ndiyo ambayo answerable kwa Mfuko ule wa Jimbo. Tumekaa vikao karibu viwili, kati yetu sisi na Viongozi wa Wizara, kwa ajili ya kujadili suala la Mfuko wa Jimbo. Ninashauri tu kwamba, katika Mfuko wa Jimbo yapo mapungufu katika ule Mfuko na hii Wizara maana yake ndiyo ambayo inatakiwa kutusimamia sisi kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ambayo imekuwepo ni kwamba, zile fedha zina mlolongo mkubwa sana mpaka sisi Wabunge kuweza kuzipata. Sasa ni vyema tubadilishe ile Sheria ya Mfuko wa Jimbo, tupunguze ule mlolongo, pamoja na kwamba kule kuna waratibu, lakini ni vyema, wakaratibu wenyewe kama ni jukumu lao mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na huo Mfuko wa Jimbo kuwepo, pia ninaishauri Wizara kwamba, kwa wakati ambao tumefika kwa sasa hivi kule Zanzibar, ni vizuri zaidi tukajenga ofisi ambayo itakuwa inajumuisha shughuli zetu zote za Kimuungano zitakazosimamia masuala ya uratibu na mengine, ambayo yatakuwa kule Zanzibar, ili kurahisisha hii milolongo yote ambayo imekuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, ninamwangalia Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuniangalia sana, ninaunga mkono hoja. Ninasema ahsante sana na ninaipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri na hotuba yao nzuri, ambayo wameileta hapa. Ahsante. (Makofi)