Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
House of Representatives
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SAID ALI MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya ya kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza ndugu yangu, Mheshimiwa Waziri, ametuletea hotuba ya bajeti yake. Ninaomba nianze kwa kusema kwamba, tunaambiwa muasisi wa Muungano wetu, Baba wa Taifa, Hayati Nyerere, alikuwa tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika mpaka majirani zake wapate uhuru kwa pamoja, ili kuunda Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yenye nguvu (Federation of East African Countries). Hilo lilikuwa jambo zuri sana, lakini kwa sababu, halikuwa, sisi wa Zanzibar Mzee wetu, Mzee Karume akaamua tuanze na pengine wenzetu wangeweza kuiga. Bahati mbaya miaka 62 sasa hakuna hata nchi moja miongoni mwa jirani zetu aliyeraghbika kujiunga nasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri tujitahidi, kama waasisi wa Muungano, tuwashawishi, ili waweze kujiunga nasi kwa sababu, umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Wenzetu wa Jumuiya ya Ulaya Mwaka 1958 walianza na nchi sita, baadaye wakaanzisha European Union, sasa wana nchi 27. Sisi Muungano wetu wa nchi mbili wa miaka 62, wao miaka 68 tayari ziko nchi 27. Sasa huko ndiyo kufanikiwa kwa Muungano, unaanza na kidogo, lakini baadaye wengine wanaiga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninashauri kwamba, jitihada zifanywe na wenzetu watuige, wa-join katika Muungano huu; wenzetu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Msumbiji, Shelisheli na Comoro, tungekuwa na Muungano mmoja mkubwa na wenye nguvu sana. Kwa hiyo, hatujachelewa, jitihada zifanyike za kibalozi, ili kuona kwamba, tuna Muungano wa nchi hizi, lakini hatuwezi kufika hapo kwanza mpaka Muungano ambao tunao mafanikio yake yawe yanavutia wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Jumuiya ya Ulaya, nchi zile 27 zilijiunga kwa sababu, waliona mafanikio makubwa ya zile nchi sita zilizoanzisha. Kwa hiyo, na sisi tujitahidi kuleta mafanikio makubwa ya kiuchumi ndani ya nchi hizi mbili, ili tuweze kufika hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea na Mheshimiwa Waziri, amezungumza suala la Kero za Muungano. Paragraph ya 28 naona; zilikuwa 25, tayari 22 zimefanyiwa kazi, bado tatu, lakini kwa maoni yangu hizo tatu ndiyo wazee wa kero na hatuwezi kuendelea kuwa na Muungano huu tukiwa na kero za miaka mingi sana, zitazaa mgogoro na mgogoro ni hatari katika umoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii ambayo amesema Waziri, suala la mgawanyo wa mapato yaliyokuwa hisa za Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Hii kuanzia mwaka 1965 mpaka leo ni zaidi ya miaka 60, sisi Zanzibar nchi hii tuna uchumi mdogo, tungetegemea mapato haya yatusaidie sana kuendesha bajeti ya Serikali, lakini miaka 60 hisa, mapato, aah!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, hii inasikitisha na ninadhani hili linahitaji tuambiwe Serikali ina mpango gani? Maana hii lugha aliyotumia Waziri mimi si ya kwanza kuisikia, kwamba, bado tunaendelea na tupo mbioni, tutakamilisha! Hii si ya kwanza kumsikia Mheshimiwa Yussuf Masauni, kuna Mawaziri wengine wa Muungano, lugha hii hii tumeweza kuisikia. Sasa ninahisi hili, sisi wa Zanzibar, linatuumiza kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni lile ambalo, ninamshukuru sana Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alituongoza kwa muda wa miaka 21. Mwaka wa 20 kabla ya kung’atuka, katika Katiba, alifanya usia kwa maana ya kwamba, alianzisha Kifungu cha Katiba cha Kugawanya Mapato ya Muungano, Mfuko wa Pamoja, Akaunti ya Pamoja ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1984 sasa ni miaka 42, Serikali zilizofuata zimeshindwa kutekeleza hili! Sasa Baba wa Taifa tunahitaji kumuenzi kwa vitendo. Mzee alikuwa na nia njema kwa sababu, anajua mambo ya fedha, mambo ya mapato katika umoja yana mitihani yake, ndiyo maana akaanzisha Kikatiba. Ndani ya Katiba ya Muungano, kifungu hiki ili wanavyoacha madaraka, wanaofuata waweze kuendeleza ili twende na Muungano wetu.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Said Ali. Taarifa.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge anazungumzia mambo yanayohusu mapato na fedha. Anasema miaka 41 Serikali imeshindwa kupeleka fedha, lakini ni vizuri angetueleza miaka ya awamu ya ngapi, awamu ya ngapi! Mwaka fulani hazikwenda, mwaka fulani hazikwenda! Anapozungumza kwa ujumla hivyo, anaweza kuwa anapotosha mapato halisi yanayokwenda kule kwa sababu, hana uhakika na hayo mapato. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Said Ali, unaipokea hiyo Taarifa?
MHE. SAID ALI MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Ninachosema ni mzee wetu alianzisha Kikatiba kifungu cha kuanzisha Akaunti ya Pamoja ya Mapato. Tokea mwaka 1984 leo ni mwaka 2026, miaka 42 kifungu hiki hakijatekelezwa, ndiyo ninachozungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo sisi Zanzibar tuna imani, tuna dhana, tuna maoni kwamba, tunakosa mapato mengi ya kuendesha nchi. Kwa hiyo, ninashukuru Mheshimiwa Waziri amesema suala hili linatekelezwa, lini? Tubaki tu kusubiri tena miaka mingapi mingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali inaendelea kuzungumza, nina hakika mwakani Mheshimiwa Waziri atakuja na maelezo kama hayo. Kwangu ninaomba maelezo ya Mheshimiwa Waziri, kwa mwaka huu wa fedha, masuala haya yanayohusu mapato ya Zanzibar amekusudia kuyatekeleza lini na kwa kiasi gani cha fedha? Atuambie shilingi ngapi za fedha amezitenga katika bajeti hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala limalizwe kwa sababu, linatuathiri sana kwa maslahi ya upande wa pili wa Muungano.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Said Ali. Kwa hiyo, hujaunga mkono hoja?
MHE. SAID ALI MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaunga mkono mpaka nisikie majibu ya Mheshimiwa Waziri.