Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Prof. Pius Zebhe Yanda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais. Nitajikita zaidi kwenye upande wa Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamazingira namba moja, hilo linaonekana wazi kwa kuwepo kwa Dira ya 2050. Kama haitoshi nguzo namba tatu ni nguzo mahsusi kwa ajili ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, haya ni maono yake yaliyowezesha kuwa na nguzo ambayo ipo dedicated kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo pia linaonekana wazi kwamba, hiyo ni nguzo muhimu kwa sababu jambo lolote lile linalofanyika kama ni la kimaendeleo kwa vyovyote vile ni lazima kuwe na checks and balances ambayo ni masuala ya mazingira kuhakikisha tuna maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekti, ninaomba pia niipongeze Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kazi kubwa ambayo inaifanya kuhakikisha kwamba misingi ya usimamizi bora wa mazingira inawekwa sawa. Ofisi imeandaa miongozo mbalimbali ambayo inasaidia usimamizi wa mazingira. Pia ninaomba kwa namna ya pekee nimpongeze Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni kwa hotuba nzuri ambayo inaakisi Dira ya 2050 na ni mwanzo mzuri katika juhudi za kuweza kutekeleza nguzo Namba Tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba pia nirejee kwa nini mazingira ni muhimu. Uhifadhi wa Mazingira ni msingi wa ustawi wa Watanzania wote, tukumbuke kwamba inabidi tutembee kwenye kauli mbiu inayosema tunza mazingira, yakutunze. Hilo ni muhimu na lazima tukumbuke pia kwamba mazingira tumeyarithi kwa mababu na mabibi zetu, sisi ni wasimamizi tu, kwa lugha ya Kiha tunaita custodians lakini kesho na keshokutwa ni lazima vizazi vijavyo viweze kutumia mazingira kama yalivyo kwa ajili ya maisha yao. Kwa hiyo, tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba mazingira yanasimamiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikirudi kwenye uharibifu wa mazingira. Tunashuhudia mfumo wa mvua unabadilika, tunaona mafuriko zaidi, tunaona ukame, lakini pia tunaona mmomonyoko wa udongo na mambo mengine yote, hayo yote ni matokeo ya uharibifu wa mazingira katika ngazi mbili. Kwenye ngazi moja tunazungumzia mabadiliko ya tabianchi ambayo binadamu wametoa mchango mkubwa sana na ndiyo maana tunaathirika na athari tunazoziona sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yanayotuzunguka na shughuli zetu tumetoa mchango mkubwa sana katika matatizo tunayoyaona sasa hivi, tumezungumzia suala la uharibifu wa Barabara, kwa nini tuna mafuriko makubwa sasa hivi ukilinganisha na siku za nyuma, kwa nini tunaona vyanzo vya mito vinaanza kukauka hasa wakati wa kiangazi. Hayo ni mambo ambayo inabidi tuweze kujiuliza na bahati nzuri sisi wenyewe tunayo majibu kwa sababu ndiyo tumechangia katika hayo matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo ninaomba niseme jambo moja kwamba, pamoja na juhudi ambazo zimefanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais, katika kuandaa mikakati, kuandaa mipango, miradi na hata kuweze kutafuta fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili, lakini bado inaonekana wazi kwamba hili tatizo ni kubwa. Hiyo imedhihirika wazi kwenye hotuba ya Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais wakati anawasilisha bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo ambalo lipo wazi ni suala la uratibu, kwamba ni kweli tunajua sekta mbalimbali, Wizara mbalimbali zimeweza kuhuisha masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Kwenye upande wa sera na upande wa mipango na mikakati kila kitu kinaonekana vizuri lakini uhalisia ni kwamba utekelezaji hauko sawa. Sasa tujihoji kwa nini haya yanaendelea hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta sasa kila sekta inafanya mambo yake kwa lugha ya wenzetu tunaita in silos, kila Wizara inafanya mambo yake, tunasahau yale ambayo tumesema tutatekeleza kwa kadri ya miongozo inayotoka Ofisi ya Makamu wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakuja kutuletea jambo moja kwamba sasa kunahitaji kuwe na ufuatiliaji wa karibu, tuone compliance wa kila sekta kuhakikisha kwamba mazingira ni part and parcel ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika nchi hii. Tunalifanyaje, hili ni jambo ambalo tunahitaji tujadiliane, jambo la msingi zaidi ni kule chini ambako tunafanya utekelezaji, tuhakikishe kwamba kuna mikakati mahsusi kila utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi tuweze kuzingatia suala la usimamizi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika, kila sekta ina component ya usimamizi wa mazingira, kwa nini tusiwe na coordinated efforts, uratibu wa karibu kwenye ngazi za Halmashauri ili kwamba hizi nguvu zote ziweze kuwekwa kwa pamoja. Tuangalie kwamba pia isije ikawa utekelezaji wa shughuli za sekta moja unaathiri sekta nyingine au unaishia kuathiri mazingira. Kwa hiyo, hayo yote yangeweza kuchujwa kwenye planning level kwenye ngazi ya wilaya ninafikiri haya yote tunaweza tukayatatua, kwa sababu kwenye ngazi ya kitaifa sera zipo, miongozo ipo, sasa ni nini kinaleta shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Ofisi ya Makamu wa Rais ni tufanye kazi ya ziada, tuone ni jinsi gani kuwe na vertical coordination pia na horizontal coordination. Nikimaanisha turatibu juu lakini tuweze kuwa na uratibu wa kutoka juu kwenda chini mpaka kwenye level ya halmashauri. Tukiweza kufanya hivyo nina uhakika tutaweza kupunguza au kujitahidi kupunguza hizi athari tunazoziona sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)