Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Fuoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASHA HUSSEIN SALEH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi jioni hii ya leo kuweza kuchangia Ofisi ya Makamu wa Rais. Kwanza kabisa ninapenda kumpongeza Rais Samia, pamoja na Rais Mwinyi kwa kazi zao nzuri wanazofanya hakika mwenye macho haambiwi tazama. Ninapenda pia kumpongeza Waziri kwa hotuba yake nzuri aliyotuletea hapa leo yenye manufaa mazima ya mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie mambo matatu katika ofisi hii. Jambo la kwanza nitachangia katika sehemu ya Muungano, jambo la pili nitachangia mazingira na uchumi wa buluu na jambo la tatu nitachangia katika Mfuko wa Jimbo. Ni dhahiri kabisa ofisi hii ni ya kupongezwa katika suala la Muungano kama Waziri alivyosema kwamba ametatua hoja 22 katika hoja 25, jambo hili siyo dogo, ni la kupongezwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anastahiki kupongezwa zaidi kwa kazi kubwa alizozifanya kwani ameweza upeleka gawio katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar linalofikia shilingi bilioni 48.5. Gawio hili likijumuisha PAYE, likujumuisha misaada kutoka nje na gawio la Benki Kuu (BOT). Kwa kweli asilimia 48.5 hili ni jambo la kupongezwa kabisa kwa kuwasilishwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko hapohapo katika suala la Muungano. Vizazi vyetu vinavyokuja kusema kweli watakuwa wanaelewa Muungano, lakini hawatoelewa zaidi. Ni vema kama mwenzangu alivyosema ni kusomeshwa katika ule upande wa Zanzibar, sijui kwa upande wa Bara kama lipo katika syllabus suala la kusomeshwa Muungano, lakini kwa Zanzibar ni bora nalo likaingizwa sehemu ya Muungano ili vizazi vinavyokuja wakauelewa Muungano wetu na wakaweza kuudumisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi kwa Waziri la kuanzisha haya matamasha au makongamano ili wananchi watakapokwenda kutembelea katika yale maeneo ya maonesho, wananchi wakienda kutembelea katika yale maonesho wakiona kazi zilizofanywa za Muungano na zinazoendelea, basi tutadumisha huu Muungano na wananchi watazidi kuupenda Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nijielekeze Mheshimiwa Waziri amesema kwamba ametatua hoja 22 na zimebaki hoja tatu, basi aendelee na watendaji wake kufanya hili jambo zuri ili kuweza kumaliza hizi hoja tatu zilizobaki ikiwemo hii hoja ya kikatiba iliyokuwepo ya Mfuko wa Pamoja wa Fedha. Kwa hiyo atumie busara zake, hekima zake ili aweze kutatua pia hoja hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo kwenye suala la Muungano sasa nijielekeze katika suala la mazingira na uchumi wa buluu. Kwa upande wangu katika Jimbo langu, basi nimwombe Makamu wa Rais aweze kutembelea katika Jimbo la Fuoni ili aweze kujionea hali ya mazingira katika Bonde la Dangamizini, pamoja na kutembelea eneo la Fuoni Kibondeni akawaona wajasiriamali au wavuvi wadogowadogo wanaojikwamua kiuchumi, wanaokwenda kule baharini kwenda kuvua kaa, akawaona jinsi gani shida zao na tabu zao wanazozipata katika kujikwamua kiuchumi ili kuwapatia mafunzo, kuweza kuwapatia vifaa pia vya uvuvi pamoja na kuwapatia boti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze katika Mfuko wa Jimbo. Kama mwenzangu pale Mheshimiwa Haji alivyosema basi nimwombe tu Mheshimiwa Waziri kwa makusudi mazima kama hali hii ya Mfuko wa Jimbo na shida hizi zinazotukuta Wabunge katika huu Mfuko wa Jimbo, basi kwa busara zake na hekima zake, bora atuletee hapa tuje turekebishe au vifungu vya sheria vilivyopo turekebishe ili viweze kukaa sawa, nasi tuweze kwenda na wakati katika huu Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)