Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jamal Ramadhan Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbwini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia jioni ya leo kwa kupata nafasi hii kuzungumza. Pili, nichukue nafasi kuwashukuru viongozi wote wa kitaifa akiwemo Mwenyekiti wa Chama changu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mara ya kwanza ninachangia, pia ninashukuru viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wa Chama changu Cha Mapinduzi Wilaya pamoja na wananchi wote wa Jimbo la Bumbwini kwa kunipa ushirikiano, kwa kunipa nafasi hii ili kuja kuwatetea wananchi wa Jimbo langu la Bumbwini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri kwa kuanza vizuri katika bajeti muhimu sana ya nchi yetu, yenye uti wa mgongo wenye maslahi ya Taifa letu, yenye msingi wa dira yetu, yenye umoja, mshikamano na ari kubwa ya maendeleo yetu. Tukiwa tuna miaka 62 sasa ya Mapinduzi yapo mambo yamefanyika, tunayapongeza yale yaliyofanyika mazuri, lakini kuna mambo mawili, matatu tunaomba Waziri ayatazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kule kwetu Zanzibar tuna kituo cha bahari kuu cha uvuvi ambacho kimejengwa Fumba. Kile kituo kwa sasa hakionekani kama kinawasaidia sana Wazanzibari kwa sababu kimekosa taaluma na Wanzibari kujua nini umuhimu wake kabisa. Sasa tunamwomba Waziri katika hilo aangalie sana ili kuweza kupata maslahi wananchi na kujua na taaluma ielekezwe zaidi ili kuweza kupata manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kwa sababu tunaelekea katika uchumi wa buluu (blue economy). Waziri katika bajeti yake mwaka huu kaona, imekuja katika mwaka wa kwanza huu tunaona vizuri sana, tuipongeze Serikali kwa kuliona hili jambo muhimu sana. Wananchi wa kwenye maeneo matatu haya ni mambo muhimu, kwanza hiyo blue economy tukiitizama hasa katika ile tunazungumza kwenye Kaboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiitizama kaboni ya buluu inayotokana na Bahari, hilo ni jambo muhimu sana na ukitizama kwenye mitandao unaona hasa jambo hili lina thamani kubwa na linaingiza fedha nyingi katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tuna Muungano na Zanzibar tumejaaliwa kabisa kutumia bahari ipasavyo vizuri sana, sasa tunaona akija Waziri hebu atuambie kati ya kuanzisha hili suala la biashara ya kaboni na Zanzibar kwa sababu tuna Wizara ya Mazingira ushirikiano kati Bara na Zanzibar upoje, katoa mchango upi na Zanzibar inanufaika vipi na ushirikiano upoje. Mheshimiwa Waziri akija atuambie ili tuone, tujue kwamba sasa tunakwenda vizuri katika kuutekeleza Muungano wetu na maslahi yanapatikana kwa wananchi wote wa pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, tunapozungumzia Muungano wa miaka 62. Muungano huu sote tukiuzungumzia tunajua na kila mmoja aliyesimama hapa anatoa historia, lakini tumpongeze Waziri pale alipokuja na hoja kwamba sasa tunaenda kujenga kituo ambacho kitatuelezea historia yetu na makumbusho ya Muungano. Mheshimiwa Waziri jambo hilo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaulizana kule ukienda sasa, watu wetu wakienda pale Kisonge pana mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi, lakini Muungano wetu mzuri na sifa nzuri tunazozitaja hakuna kituo kinachoainisha, hicho kituo kikiwepo kitatusaidia sana na kitakuza utalii, watalii wetu watakuja kusoma historia ya nchi yetu ilivyo tutaondoka na hilo deni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuunge mkono Rais wetu Samia wa Jamhuri ya Muungano, hiki kituo kikijengwa akiwa anaongoza yeye katika huu utawala kitaleta tija sana na fahari kwetu. Mheshimiwa Waziri anapaswa alisimamie jambo hili na kuhakikisha tukija bajeti ya mwakani, basi atuambie tumefikia wapi na kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni elimu kwenye Mazingira. Mazingira tunayapigia mfano, sote tunahitaji mazingira, uhai wetu sisi ni mazingira, lakini bado katika eneo hili hatujafanya vizuri. Sasa tunaomba Waziri aone mkazo katika hili eneo tuweze kufika mahali. Kwa nini, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika siku ya kuazimisha sherehe yake ya kuzaliwa anakwenda anaonekana kwa dhahiri kabisa ameelekeza suala hili la kupanda miti, lakini hii Serikali kuna Wizara nyingine inatoa vibali vya kukata miti na huku tuna mipango ya kuanzisha biashara ya kaboni. Tunaomba walitizame hili jambo, Wizara hizi zikae zijue asili, tujue hii tofauti iko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo ni la muhimu sana, tunapoangalia mazingira tunayaangalia vipi, yapo mazingira yanachafuka, lakini kwenye eneo la kuweka sana rasilimali za fedha hasa kwenye suala la madini, eneo hili tuwekee sheria maalum na tupate tozo ambazo zinatoka kwenye madini kwenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Mazingira kama ni faini kati ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo tumeliona na Waziri amelitaja lakini Mwenyekiti wa Kamati amelitaja ni kuhusu suala na NEMC, hebu hii NEMC sasa tumalize hili tatizo, tumwombe Waziri aje na sheria sasa tumalize ili tuipe meno hii taasisi iweze kufanya vizuri ili mambo yetu yaende vizuri kabisa, tufike mahali sasa tumalize tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la elimu kwenye mazingira, tunasema huko zamani wazazi wetu, wazee na shuleni kwetu mazingira yalikuwa yakifundishwa. Sasa kwenye eneo hili kwenye elimu haliko vizuri, tutafute njia sasa kuona sasa mtaala wa kufundisha mazingira ili nchi yetu ifike salama baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, ninaipongeza sana bajeti yake. Mimi kwa niaba ya wananchi wa Bumbwini ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)