Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, na mimi ninakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira; ninakushukuru sana. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia siku ya leo nikaweza kusimama hapa katika Bunge letu hili Tukufu la Kumi na Tatu, ninashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nianze kwanza kwa pongezi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nimpongeze kwa namna anavyoendelea kutuongoza wananchi wake, lakini kwa namna anavyoendelea kutambulika katika nchi yetu kitaifa na kimataifa duniani. Hongera sana kwa Mama Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza pia Makamu wetu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi, lakini pia nimpongeze sana Waziri wetu Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, tunampongeza sana. Kwa kweli Waziri Mkuu anatutia moyo na anatutia nguvu kwa namna anavyoendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu. Hili ni fundisho, kwamba na sisi wasaidizi wake tukaze buti na tunamwahidi tutaendelea kuunga mkono jitihada hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mwenyekiti wangu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania, Mama Mary Chatanda. Nina kila sababu ya kumshukuru kwa sababu amenilea vizuri, ametufunza vizuri wanawake leo tumeweza kusimama hapa kuweza kuchangia hotuba hii ya bajeti. Ni upendo wa kutulea vizuri wanawake sisi, tukaweza kuisemea mema Serikali yetu kwa sababu ya inayoyafanya na hatubahatishi. Tunachangia hotuba hii ya bajeti kutokana ana kazi nzuri za Mheshimiwa Dkt. Samia. Ni lazima wanawake tuwe mstari wa mbele na tutaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri wangu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Waziri Hamad Masauni. Waziri Masauni ni msikivu na ni mwelewa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati hii, anatuongoza vizuri sana, tunakwenda naye vizuri kwenye hii Wizara. Amekuwa akichangia vizuri katika kuwasilisha hoja zake na sisi tumeweza kuzichangia vizuri kuisaidia Serikali yetu. Hongera sana Mheshimiwa Waziri na insha Allah Mwenyezi Mungu atamsaidia kwenye hili la kumsaidia Mama Samia. Anachokifanya ni haki yake kwa sababu anaitumikia nchi yake kwa utii, naye Mwenyezi Mungu atamsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu utakuwa na mambo mawili. Moja, suala la Muungano, lakini la pili suala la nishati safi na salama. Nianze mchango wangu kwenye jambo la nishati safi na salama. Nichukue nafasi hii nimpongeze sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara, lakini balozi namba moja kwa kutunza mazingira, lakini kwa kuongoza vizuri nishati safi na salama nchini. Dkt. Samia amekuwa wa mfano kwenye jambo hili na ndiyo maana sisi Wajumbe wa Kamati tumepata nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba, kutokana na nguvu zake zile za kuhakikisha kwamba nishati safi na salama inatumika kwenye nchi yetu, leo wamekwenda kufaidika mama lishe na baba lishe kwenye nchi yetu hii. Wajasiriamali walio wengi tayari wamenufaika na nishati safi na salama, wameweza kujinyanyua katika hali zao za kiuchumi kutoka walipokuwa na sasa walipo; tunamshukru sana Mheshimiwa Rais. Kwa kweli, Mheshimiwa Rais anatuwakilisha vyema na anatuendesha vyema kwenye nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema, kwamba nishati safi na salama kwenye nchi ni jambo muhimu. Tutaendelea kusema, kwamba ni mahali petu wananchi, sote tuunge mkono jitihada hizi za Mheshimiwa Rais na jitihada za Waziri wetu anazozifanya katika Wizara yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajasiriamali wengi, wakiwemo wanawake walikuwa na afya mgogoro kwa kutokutumia nishati safi na salama, lakini Mama Samia amekuwa mkombozi, leo akina mama wanauza biashara wakiwa wanang’ara, wanameremeta unaona raha kununua chakula chao. Hii ni jitihada ya Dkt. Samia, amemwezesha mwanamke wa Kitanzania, amemwezesha kijana wa Tanzania kufanya biashara zake katika hali ya afya njema na hali ya usafi. Ahsante Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuwa rahisi, watu walikuwa wakitumia matumzi ya kuni, ndipo aje afanye biashara zake. Vilevile wanawake wenzetu walikuwa wakikaa kwenye foleni hospitali kutokana na kuharibika macho; leo Mama Samia amekwenda kuwajengea uwezo, akawatoa walikokuwa. Tunamshukuru Dkt. Samia na wala hatuchoki, hatuchoki kumshukuru kwa mazuri na mema anayoendelea kutufanyia wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kabla sijatoa ushauri wangu kwa Serikali, ninaomba nilizungumzie jambo la Muungano. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa zile kero ambazo ameweza kuziondosha, zimebaki chache, tatu tu. Niseme kwamba, hakuna jambo rahisi, hata nyumbani kwako huyamalizi yote kwa wakati mmoja, itakuwa jambo la nchi? Tutaendelea kuulinda Muungano wetu, tutaendelea kuutetea Muungano wetu kwa gharama yoyote kwa bei yoyote hauvunjiki, na tuna kila sababu ya kusema hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge waende Kariakoo Dar es Salaam, tunaongoza Wazanzibari kwa biashara, tume-invest, halafu ndiyo unitoe kwenye Muungano? Haiwezekani! Muungano tutaendelea kuulinda kwa sababu ni tunu yetu tuliyoachiwa na wazee wetu wa CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kutoa ushauri kwa Serikali yangu sikivu na Tukufu. Tuna VETA kila wilaya katika nchi yetu. Sasa, kama itapendeza kwa Serikali yetu, ni vizuri vijana na wanawake wenzetu kupatiwa ujuzi wa kuzalisha majiko sanifu. Haya yatasaidia kuzalisha kipato kwao, lakini pia yataongeza kutoa fursa kiuchumi na kuondokana na maisha tegemezi ya kusubiri ajira za Serikali yetu peke yake. Kama Serikali yetu inavyotaka, inatoa fursa, sasa ni wakati vijana kujiajiri na pia wanawake wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. Ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)