Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia fursa ili niweze kuchangia katika mada iliyoko mezani. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetujalia uzima na afya njema mpaka siku ya leo nimeweza kusimama hapa ili niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya; lakini pia wasaidizi wake wanaomsaidia akiwepo Makamu wa Rais, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu. Pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri wetu wa Wizara hii, kwa kazi nzuri nayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, vilevile ninampongeza kwa hotuba nzuri aliyoitoa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza moja kwa moja katika mchango wangu na nitaanza katika kuchangia katika suala la hewa ya ukaa. Biashara ya hewa ya ukaa katika nchi yetu ya Tanzania, bado haijawa wazi, ni kwa sababu Serikali bado haijatafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya kufanya biashara hiyo. Mfano sisi Wilaya yetu ya Tanganyika ndani ya Mkoa wangu wa Katavi tunafanya biashara hii na halmashauri nyingi nchini zimekuwa zikija kujifunza katika mkoa wetu wa Katavi Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba biashara hii bado haijawa na uwazi kutokana na kwamba masoko ya uhakika bado hayajapatikana. Hivyo niiombe sana Serikali yangu iweze kutafuta masoko ya uhakika kwa sababu hata sisi Wilaya ya Tanganyika inavyoonekana baada ya mimi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira, wale watu wanaofanya biashara ile ni middle man ambao kwa kweli biashara hii imesababisha kutokuwa na uwazi. Hata wananchi pia tumekuwa hatuna uelewa nini kinachopatikana kutokana na biashara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali ikitusaidia kupata masoko ya uhakika kupitia halmashauri zetu ambapo watu watafanya biashara hii tutakwenda kuwa wanufaika kwa sababu sisi Wilaya ya Tanganyika tayari ni mfano kupitia biashara hii. Tumeweza kujenga vituo vya afya vya kisasa na hivyo tunaamini katika nchi yetu ya Tanzania iko mikoa mingi ambayo ina misitu mizuri na wenyewe wanaweza kufanya biashara hii na wenyewe wakaweza kunufaika na wananchi wakapata jitihada za kuweza kutunza misitu hususan misitu ile ya asili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali vilevile iondoe kuchelewesha kutoa vibali kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara hii ya hewa ukaa. Mfano, katika msitu wetu wa Tongwe Wilaya ya Tanganyika, pia Msitu wa Nkamba ni misitu ambayo tulikuwa tunatarajia kufanya biashara hii ya hewa ukaa, lakini mpaka sasa vibali vimekuwa vikicheleweshwa, hivyo kusababishia halmashauri kupoteza mapato mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaokaa katika maeneo yale kwa kweli wamekata tamaa hata ya kutunza misitu ile ambayo ni ya asili. Tunatambua biashara hii inafanyika, lakini misitu yetu inaendelea kutunzwa. Badala ya watu kukata miti watu wamekuwa wakihamasika kuitunza misitu kwa sababu wameona sasa misitu ni fursa kwao ya kuwapatia kipato lakini kuleta maendeleo katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la NEMC. Tunaiomba sana Serikali iweze kuharakisha NEMC iweze kuwa mamlaka kamili kwa sababu tunatambua NEMC inafanya kazi kubwa na nzuri, lakini mpaka sasa NEMC imekuwa ikisuasua kutokana na kwamba bado haijawa mamlaka kamili. Sasa hatutaki NEMC iwe na visingizio. Sote ni mashahidi tumeendelea kushuhudia kwamba kuna ucheleweshwaji wa vibali katika kufanya biashara. Tunatambua kwamba biashara nyingi ili zifanyike ni lazima NEMC waweze kutoa vibali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano watu wanataka waanzishe petrol station lakini vibali vimekuwa vikisuasua. Tunachoiomba Serikali NEMC iweze kupewa mamlaka kamili ili itakapokuwa inafanya vibaya tuweze kuihoji, tuweze kuwauliza nini kinakwamisha kwa sababu tunatambua hata Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 mpaka 2050 inasema kwamba 70% itatokana na private sector. Sasa sekta binafsi wanakwamishwa mara nyingi na NEMC kutokana na kwamba…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava, taarifa.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa taarifa mzungumzaji. Pamoja na mchango wake mzuri, ninataka nimpe taarifa kwamba ni sahihi ili NEMC iweze kufanya kazi vizuri ni lazima iwe mamlaka kamili. Hata majirani zetu kwa maana ya nchi zote ambazo zinatuzunguka, vyombo vyao vya kusimamia mazingira kwa sasa ni mamlaka kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua mfano wa Kenya kupitia Sheria ya Usimamizi na Uratibu wa Mazingira Na.8 ya Mwaka 1999, Kenya wana mamlaka, lakini Rwanda hivyo hivyo wana mamlaka inaitwa REMA na Uganda the same wana mamlaka kamili ambayo inasimamia shughuli za mazingira kama ilivyokuwa NEMC kwa upande huu wa Tanzania. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Martha, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo. Tukiwezesha NEMC kuwa mamlaka kamili ni uhakika kwamba itakwenda kufanya kazi nzuri. Sote tumeshuhudia pia uharibifu katika maeneo mbalimbali. Mfano, katika sekta ya madini kule wachimbaji wamekuwa wakifanya uchafuzi katika mazingira, lakini NEMC wanashindwa kuwa na kauli moja kwa sababu bado haijawa mamlaka kamili kuna mwingiliano wa kimaslahi. Hivyo tunasema kwamba NEMC ikiwa mamlaka kamili itaweza kuendelea kuwawajibisha wale wote wanaofanya uchafuzi wa mazingira, lakini itafanya kazi zake vizuri. Hivyo ni muhimu sana NEMC ikawa mamlaka kamili ili iweze kufanya kazi zake ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na suala la mazingira. Hapa nichukue nafasi hii kumpongeza sana kinara namba moja wa mazingira katika Taifa letu la Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama yetu kwa kazi nzuri anayoifanya kuhakikisha kwamba anayatunza mazingira na ameonyesha mfano. Hata siku ya leo tumeona kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kukutana na mama lishe na baba lishe kwa ajili ya kuwapatia mitungi kwa ajili ya nishati safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli amekuwa kinara wa kuhakikisha kwamba nishati safi na salama inakuwa kipaumbele katika Taifa letu la Tanzania na kuhakikisha kwamba matumizi ya nishati chafu katika Taifa letu yanakwenda kukomeshwa katika Nchi yetu ya Tanzania na katika maeneo yetu na hata katika bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama huyu ndiyo kinara wa kuhakikisha kwamba nishati safi inafika katika maeneo yote. Pia, amekuwa akijipambanua kwa kuielezea na kwa kufanya vitendo na amekuwa akifanya hivyo kwa kukutana na makundi mbalimbali kuhakikisha kwamba suala la nishati safi ni kipaumbele kwani tunatambua kabisa waathirika wakubwa wa nishati chafu ni akina mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, akina mama waliokuwa wakitumia kuni kwenye kupikia ambao kwa kweli walikuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akaamua kufanya kwamba jambo la nishati safi liweze kuwa kipaumbele katika nchi yetu ya Tanzania. Hivyo tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini tunampongeza kwa kuifanya siku yake ya kuzaliwa kuwa siku ya upandaji wa miti. Hilo ni jambo kubwa sana ambalo linasaidia kuendelea kutunza mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)