Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AMOUR SEIF ABDALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza kabisa ninampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa yeye ni kinara namba moja katika kuhakikisha haya masuala ya mazingira yeye anakuwa ni mfano kwa kufanya kwa vitendo. Sote ni mashuhuda yeye ndiye anakuwa ni mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba anapanda miti kwa vitendo na anafika hadi site kwa ajili ya kuwahimiza wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii ya masuala ya Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulika na masuala ya Muungano na Mazingira, ninataka nichangie kwenye masuala ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya mazingira Tanzania sisi tumepiga hatua kubwa sana. Kwa kuthibitisha hivyo ni kwamba juzi tu Mheshimiwa Masauni hapa amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais katika Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa. Asingechaguliwa huyu Mheshimiwa kama Tanzania haijafanya vizuri katika masuala ya mazingira. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Hamad Masauni kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais katika Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme katika hotuba hii ya masuala ya Mazingira pamoja na Muungano pia nimependa katika hotuba hii dira yake inavutia kabisa inayosema, “Tanzania yenye Muungano imara lakini vile vile endelevu katika mazingira salama, endelevu, uchumi wa bluu na uchumi jumuishi wa bluu.” Kwa hiyo, nimependa sana dira ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii ya mazingira na katika hotuba hii ya bajeti, ninaomba nichangie katika mazingira. Hata katika Jimbo la Wete ni muhanga wa masuala ya mazingira kwa Bandari yangu ya Wete, katika ile sehemu ambayo ni uchumi wa bluu ambayo imo humu kwenye hotuba katika gati ya wachuuzi na wavuvi wa Jimbo la Wete. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mazingira ya pale ni mazingira ambayo yameshababishwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ya bahari. Sasa inapelekea pale katika bandari ya wachuuzi watu hawafanyi kazi zao kwa inavyotakiwa kwa sababu mazingira si mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira ya Bandari ya Wete; bandari pale ni bandari ya pili ya ukusanyaji wa mapato kwa TRA na ZRA kwa Zanzibar. Hata hivyo, licha ya kuwa mazingira ya ile bandari si rafiki watu wanafanya kazi vizuri, lakini endapo kama Wizara hii itakwenda kuangalia vizuri katika mazingira ya ile gati kwa sababu imepelekea kutokana na hii tabianchi ya mabadiliko ya bahari imesababisha kina cha pale kuwa kidogo hadi inasababisha vyombo vingine vinashindwa kwenda pale. Vyombo hivyo vikishindwa kwenda katika Bandari ya Wete kutokana na mazingira mabovu tutakosa mapato mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Wizara hii iende ikaangalie pale, ikapeleke wataalam mahususi kabisa kwa ajili ya kuangalia Bandari ya Wete mazingira yake na mazingira ya Gati ya Wete, lakini vilevile na ile sehemu ya wachuuzi na wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu Bandari ya Wete ndiyo uti wa mgongo wa Kaskazini Pemba. Hivyo, mazingira yanasababisha hata maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Pemba na maendeleo katika Jimbo langu la Wete yanasuasua kwa sababu ya bandari kuwa ndiyo uti wetu wa mgongo pale hatuna kitu kingine ambacho kinasababisha uchumi wa Kaskazini ukue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Wizara hii na namwomba Mheshimiwa Waziri waende wapeleke wataalam pale wakaangalie hili suala ni la muda mrefu sana kwa sababu pale tunategemea channel nne katika ile bandari endapo kama mazingira yataboreshwa vizuri kabisa ile bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna channel ya Mombasa, pale tunategemea sana Bandari ya Mombasa, tunategemea sana Bandari ya Tanga, tunategemea sana Bandari ya Unguja pamoja na Dar es Salaam. Hivyo, mazingira kwa sasa siyo rafiki, ndiyo maana inasababisha mapato ni mengi, lakini hayatoshelezi. Hivyo, ninaiomba Wizara hii iende pale ipeleke wataalam ili uchumi wa mtu mmoja mmoja pale Wete ukue; lakini vilevile na kipato cha TRA na ZRA kizidi kuongezeka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa haya mambo mazuri ambayo yameelezwa katika hotuba hii ya Makamu wa Rais, Mzingira na Muungano, ni mambo mazuri, ambayo yana dira nzuri, yameelezwa hapa na Mheshimiwa Waziri. Nami sina budi kusema kwamba ninaunga mkono hotuba hii kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)